Mkondo wa Ghuba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mkondo wa ghuba)
Mkondo wa Ghuba

Mkondo wa Ghuba (kwa Kiingereza gulf stream) ni mkondo wa bahari unaopita katika Atlantiki kuelekea kaskazini.

Mkondo wa Ghuba ni sehemu ya utaratibu wa mikondo ya bahari inayozunguka dunia yote.

Njia ya mkondo wa Ghuba[hariri | hariri chanzo]

Unaanza katika ghuba ya Meksiko, unapita katika mlango wa bahari wa Florida kufuata pwani ya mashariki ya Marekani, halafu unavuka Atlantiki kuelekea Ulaya.

Kabla ya kufikia visiwa vya Britania unajigawa, na mkono wa kusini unapita pwani za Hispania / Ureno hadi Afrika ya Magharibi. Mkono wa Kaskazini unapita funguvisiwa ya Britania (Ueire, Britania) na Bahari ya Kaskazini hadi Skandinavia. Mkono huu wa Kaskazini huitwa "Mkondo wa Atlantiki ya Kaskazini".

Vipimo vyake[hariri | hariri chanzo]

Mkondo ya Ghuba husukuma katika kila sekondi milioni 30 - 80 za maji - ni mara mia jumla ya mikondo ya mito yote duniani.

Mkondo una upana wa km 80–150 na kina cha m 800–1200. Mwendo wake ni hadi 2 m/s.

Athari kwa tabianchi ya Ulaya[hariri | hariri chanzo]

Mkondo wa Ghuba husukuma maji vuguvugu Kaskazini, hivyo ni kama jiko kwa ajili ya tabianchi ya Ulaya ya Kaskazini. Kwa njia hi tabianchi ya Ulaya ya Kaskazini na magharibi si baridi jinsi ilivyo katika Amerika kwenye latitudo ileile. Kwa mfano latitudo ya Norwei inalingana na sehemu za Kaskazini za Kanada lakini tabianchi ni ya kupoa: Norwei hakuna baridi kali jinsi ilivyo Kanada ya Kaskazini. Maji ya mkondo wa ghuba husababisha bandari za Ulaya ya Kaskazini hadi Murmansk kuwa bila barafu hata wakati wa baridi.

Tabianchi ya Ulaya inaruhusu kustawi kwa mazao ya kutosha kulisha watu wengi - wakati huohuo maeneo ya Kanada katika latitudo ileile hazina watu kutokana na vipindi virefu vya baridi na muda mfupi wa kustawi wa uoto. Katika Kanada kwenye latitudo ya 60 hakuna miti tena kwa sababu ya kipindi kirefu cha baridi - kumbe Ulaya miji mikubwa kama Sankt Petersburg, Helsinki, Stockholm na Oslo iko kwenye latitudo ileile.

Hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani[hariri | hariri chanzo]

Kuna dalili ya kwamba mkondo wa ghuba umeanza kubadilika kutokana na kuongezeka kwa halijoto duniani. Wataalamu wengine wanahofia ya kwamba kuyeyuka kwa barafu kwenye ncha ya kaskazini kunaweza kuvuruga mwendo wa mkondo. Hii ingeweza kusababisha mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa hasa Ulaya, kwa kuongezeka kwa baridi na kupunguza mno kiasi cha chakula kinachokua katika bara hii.