Nenda kwa yaliyomo

Mto

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mito)
Mto Nile nchini Misri.

Mto ni mwendo asilia wa maji yanayofuata njia yake kwenye mtelemko hadi mdomoni wake.

Chemichemi

Chanzo cha mto mara nyingi ni chemchemi au ziwa au maungano ya vijito vidogo. Mto hufuata mwendo wake kwa mtelemko hadi mwisho wake baharini au ziwani au kwa mto mwingine. Kama mto ni mdogo huitwa kijito. Mto mkubwa sana kama Kongo au Nile unaweza kuitwa mto mkubwa au jito.

Lalio chini ya mto

[hariri | hariri chanzo]

Njiani mwake mto huwa umechimba lalio linalofanana na mfereji kati ya udongo au mawe ya kingo zake. Nguvu ya kusogeza maji mtoni ni uvutano wa dunia.

Mdomo na delta

[hariri | hariri chanzo]
Delta ya Mto Nile inavyoonekana kutoka angani - picha ya NASA.

Mwisho wa mto huitwa mdomo. Mdomoni kwa kawaida mto huishia katika gimba kubwa zaidi ya maji, ama mto mkubwa au ziwa au bahari. Mdomo huo unaweza kuwa mpana kama kijazio hasa baharini ambako bahari inapanuka wakati wa maji kujaa.

Mito mingine inaonyesha mdomo wa delta kama imegawanyika mdomoni kuwa na mikono mingi inayoelekea bahari kwa umbo la pembetatu.

Matawimito na majina

[hariri | hariri chanzo]

Njiani mito mingi inaunganika kuwa mito mikubwa zaidi. Ni desturi kutumia jina la mto ulio mkubwa zaidi mahali pa kuungana kwa ajili ya sehemu inayofuata ya mto uliopanuka.

Kwa mfano mito ya Ubangi na Kongo inakutana kwenye mji wa Mbandaka. Huko Kongo ni mto mkubwa kushinda Ubangi; hivyo baada ya Mbandaka kuelekea bahari mto unaendelea kuitwa "Kongo".

Wakati mwingine ni swali la uzoefu tu jinsi ya kutaja mto; Kongo inaitwa Lualaba hadi mji wa Kisangani. Wataalamu wengine wanasema ya kwamba mto Kagera ingestahili kuitwa "Nile" kwa sababu ni mto uleule unaopita tu kwenye ziwa Viktoria Nyanza.

Kuna pia uzoefu ambako jina la mto mdogo linaendelea kutumika. Mto Ruvuma unatoka Songea na kufuata mpaka wa Tanzania na Msumbiji. Unakutana na mto Lujenda ambao ni mkubwa zaidi; inawezekana kusema ya kwamba Ruvuma inaingia Lujenda lakini jina la Ruvuma linatumika hadi mdomoni.

Mto mdogo zaidi unaojiunga na mto fulani mkubwa huitwa tawimto.

Ramani ya beseni kubwa kwenye bara la Afrika (tahajia ya Kijerumani).

Jumla ya eneo ambako matawimito yote hadi vijito asilia kabisa vinaanza na kupokea maji yake huitwa beseni. Sehemu kubwa ya Tanzania ya kaskazini-magharibi pamoja na Kenya magharibi ni sehemu ya beseni la Nile kwa sababu matone ya mvua kama yanafika mtoni yote huelekea ziwa Viktoria Nyanza na kuingia mto Nile kwenda bahari ya Mediteranea.

Sehemu kubwa zaidi ya Afrika ya Mashariki inapeleka maji kwenda mabeseni ya Rufiji, Ruvuma, Ruaha Mkuu au mto Tana ambayo yote inaishia katika Bahari Hindi.

Mipaka kati ya beseni huitwa tengamaji. Tengamaji kwa kawaida ni eneo la juu ambako upande mmoja maji hutelemka kuelekea beseni moja na upande mwingine kwenda beseni tofauti. Kwa mfano tengamaji kati ya mabeseni ya Ruaha Mkuu na Mto Zambezi (kupitia Ziwa Nyasa) inafuata milima ya Uporoto na milima ya Kipengere.

Mito katika dura ya maji duniani

[hariri | hariri chanzo]

Mito inabeba kiasi kikubwa cha maji ya mvua ikirudi baharini katika dura ya maji duniani.

Maji ya mtoni ni maji matamu, tofauti na maji ya chumvi ya baharini. Hii ni sababu ya kwamba mimea, wanyama na watu hupenda kukaa karibu na mito.

Watu huona faida zaidi kwa sababu mito mikubwa na majito inafaa pia kwa usafiri. Kihistoria mito ilikuwa kati ya njia za kwanza kabisa za mawasiliano kati ya maeneo ya mbali.

Mito kumi mirefu duniani

[hariri | hariri chanzo]

Kadirio ya urefu wa mto hutegemea jinsi ya kuhesabu matawimito yake. Orodha inayofuata ina tofauti na orodha inayokadiria kwa namna nyingine.

  1. 6.671 km - Nile: Luvironza-Ruvuvu-Ruvusu-Kagera-Nile Nyeupe-Nile - (Afrika)
  2. 6.387 km - Amazonas: Apurimac-Ene-Tambo-Ucayali-Amazonas - (Amerika ya Kusini)
  3. 6.380 km - Yangtse (Cháng Jiāng) - (Asia)
  4. 6.051 km - Mississippi-Missouri - (Amerika ya Kaskazini)
  5. 5.940 km - Yenisei-Angara - (Asia)
  6. 5.410 km - Ob-Irtysch - (Asia)
  7. 5.052 km - Amur-Argun-Kerulen - (Asia) - (pekee wakati wa mvua nyingi)
  8. 4.845 km - Huang He - (Asia)
  9. 4.500 km - Mekong - (Asia)
  10. 4.374 km - Kongo - (Afrika)

Mito nje ya dunia

[hariri | hariri chanzo]

Mito inaweza kupatikana pia kwenye sayari nyingine zenye kiowevu. Maziwa na mito imegunduliwa kwenye mwezi Titan wa sayari Zohali. Angahewa ya Titan haina maji, ni karibu yote nitrojeni. Kiowevu ya maziwa na mito yake inaaminiwa kuwa methani na hidrokaboni nyingine zinazotokea duniani kama gesi lakini kwenye baridi ya Titan hupatikana kama kiowevu. Chombo cha angani Cassini ya NASA ilituma picha ya mto wa Titan wenye urefu wa kilomita 400. [1]

Mito mirefu ya Afrika

Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.