Titan (mwezi)

Titan (kutoka Kigiriki: Τῑτάν)[1] ni mmojawapo kati ya miezi ya sayari Zohali wenye ukubwa wa sayari ndogo. Kipenyo chake kwenye ikweta ni kilomita 5,150 km[2][3][4] na inasogea kwenye mzingo wenye umbali wa kilomita 1,221,865 km kutoka Zohali. [2] Titan ilitambuliwa mwaka 1655 na mwanaastronomia Christiaan Huygens kwa kutumia moja ya darubini za kwanza iliyoboreshwa. Titan ni mwezi mkubwa wa Zohali na mwezi mkubwa wa pili katika mfumo wa Jua letu. Hata ni kubwa kuliko sayari Utaridi.
Muundo

Zamani Titan ilikadiriwa kuwa mwezi mkubwa katika mfumo wa jua. Lakini safari ya Voyager 1 ilipita Titan mwaka 1979 na vipimo vya kipimaanga hicho vilionyesha ya kwamba uso wa Titan unafichwa na angahewa zito lenye unene wa kilomita 900 . Kwa hiyo imejulikana ya kwamba Ganymedi, mwezi wa Mshtarii, ni kubwa zaidi.
Ikiwa Titani ni kubwa kushinda Utaridi inajulikana ya kwamba masi yake ni ndogo. Kwa hiyo inaaminiwa ya kwamba unaundwa hasa na barafu ya maji. Hata uso wa mwezi ni hasa barafu ya maji ambayo ni imara kama mwamba kutokana na baridi kali ya 180 C° usoni mwake. Chini ya ganda imara hilo kuna uwezekano wa kuwa na bahari ya maji.
Kiini cha Titan ni silikati na metali. [5] Graviti ya Titan ni ndogo; mtu anayeweza kuruka mita 1 juu ya uso wa dunia angeweza kuruka mita 7 juu ya uso wa Titan.
Mwendo
Titan inapita obiti yake katika siku 15 na saa 22 ikizunguka sayari yake Zohali mara moja. Muda huo unalingana na mzunguko wa Zohali kwenye mhimili wake au muda wa siku 1 ya Zohali.
Mzingo wa Titan unafanana na duara ingawa si duara kamili.
Angahewa
Pamoja na Dunia yetu ni mahali pa pekee penye angahewa zito la gesi. Lakini haifai kwa binadamu kwa sababu ni baridi sana na gesi zake ni nitrojeni pamoja na hidrokaboni kama methani. Pamoja na Dunia ni pia mahali pa pekee katika mfumo wa Jua penye maziwa na mito lakini hii si ya maji bali na methani kiowevu.[6][7]
Angahewa la Titan lina shinikizo mara 1.45 kuliko Dunia; densiti yake ni mara nne densiti ya angahewa la Dunia. Tabia hizo, pamoja na kiwango kidogo cha upepo na graviti iliyo ndogo kuliko duniani, zinaaminiwa kuruhusu upelelezi wa mwezi huo kwa njia ya vyombo vya hewani. Mamlaka ya usafiri wa anga ya Marekani inaandaa mradi wa Dragonfly itakayopeleka helikopta hadi Titan kwenye mwaka 2037[8].
Cassini-Huygens

Tarehe 1 Julai 2004 chombo cha angani Cassini–Huygens iliingia katika mzingo wake kuzunguka Zohali. Sehemu ya Huygens iliachana na Cassini na kufika usoni pa Titan 14 Januari 2005 ambako iliweza kutuma data kwa dakika 72. Data hizo zilihusu zaidi angahewa la mwezi huo na kuwepo kwa viowevu. Cassini inaendelea kuzunguka Titan na Zohali pamoja na miezi mingine ya Zohali. [9] Cassini ilithibitisha kuwepo kwa maziwa makubwa ya hidrokaboni karibu na ncha ya kaskazini. [10] Ziwa kubwa lenye eneo kama Bahari ya Kaspi duniani ilipewa jina la Kraken Mare.[11]
Kurasa nyingine
Soma
- Lorenz, Ralph; Jacqueline Mitton (Mei 2002). Lifting Titan's Veil: Exploring the Giant Moon of Saturn. Cambridge University Press. ISBN 0-521-79348-3.
Marejeo
- ↑ (2002) Pocket Oxford Classical Greek Dictionary. Oxford University Press, 365. ISBN 9780198605126.
- ↑ 2.0 2.1 Harvey, Samantha (2011-03-04). NASA: Solar System Exploration: Planets: Saturn: Moons: Titan. NASA. Jalada kutoka ya awali juu ya 2011-03-23. Iliwekwa mnamo 2011-03-13.
- ↑ (2010) Wonders of the Solar System. HarperCollins, 94-95. ISBN 9780007386901.
- ↑ (2010) How it Works Book of Space. Imagine Publishing, 63. ISBN 9781906078829.
- ↑ G. Tobie, O. Grasset, J. I. Lunine, A. Mocquet, C. Sotin (2005). "Titan's internal structure inferred from a coupled thermal-orbital model". Icarus 175 (2): 496–502. doi:10.1016/j.icarus.2004.12.007. [1].
- ↑ The lakes of Titan. Nature. Retrieved on 2011-03-13.
- ↑ Cox, Brian. BBC: Science: Space: Solar System: Moons: Titan: Methane rain on Titan (Video). BBC. Jalada kutoka ya awali juu ya 2011-03-16. Iliwekwa mnamo 2011-03-13.
- ↑ After Ingenuity's successful Mars flight, NASA plans to fly a huge rotorcraft on Saturn's moon, tovuti ya Salon.com, tarehe 20 Aprili 2021
- ↑ Pence, Michael (9 Machi 2006). NASA's Cassini Discovers Potential Liquid Water on Enceladus Archived 3 Machi 2008 at the Wayback Machine.. NASA Jet Propulsion Laboratory. Retrieved on 8 Julai 2007.
- ↑ Rincon, Paul (2007-03-14). Probe reveals seas on Saturn moon. BBC. Iliwekwa mnamo 2007-07-12.
- ↑ NASA reveals first-ever photo of liquid on another world. CNN (18 Desemba 2009). Iliwekwa mnamo 2009-12-20.