Tohara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Tohara inavyofanyika.
Hii ndio kabla na baada ya tohara
Uenezi wa tohara duniani.

Tohara (kutoka Kiarabu طهارة tahara - safi, tahiri) ni upasuaji mdogo wa kukata na kuondoa govi, yaani ngozi inayofunika kichwa cha uume.

Wakati mwingine ukeketaji huitwa "tohara ya mwanamke".

Inaweza kufanyika katika umri wowote na kwa sababu za kiutamaduni, za kidini au za kiganga. Mara nyingi desturi za kutahiri zinachanganya sababu za kidini na kiutamaduni. Kwa mfano, Waislamu wa Misri huamini ya kwamba wanatahiri watoto wao kama amri ya kidini lakini Wakristo Wakopti wa nchi hiyo hutahiri watoto vilevile. Ukweli ni kwamba tohara inajulikana ilikuwa desturi ya Wamisri tangu kale.

Tohara inafanyika hasa mara baada ya kuzaliwa kwa mtoto au wakati wa kubalehe.

Kufuatana na Shirika la Afya Duniani takriban 30% za wanaume wote duniani wametahiriwa, wengi wao wakiwa Waislamu.

Tohara ya kiutamaduni[hariri | hariri chanzo]

Katika makabila mengi ya Afrika mvulana anatahiriwa ili kuingizwa katika kundi la wanaume wanaopaswa kuwajibika katika jamii.

Desturi hiyohiyo inaonekana pia kati ya watu wa Pasifiki k.mf. Wapolinesia wa Samoa, Tonga na Niue, vilevile kati ya Wamelanesia wa Fiji na Vanuatu.

Wakazi asilia wa Australia huwa pia na tohara ya wavulana.

Tohara kama amri ya kidini[hariri | hariri chanzo]

Uyahudi[hariri | hariri chanzo]

Kwa Wayahudi tohara ni ishara ya agano lao na Mungu na inapaswa kufanyika siku ya nane baada ya mtoto wa kiume kuzaliwa ili kumwingiza mapema katika taifa la Mungu.

Kufuatana na habari za Biblia Ibrahimu alikuwa mtu wa kwanza aliyepokea amri ya kutahiriwa kama alama ya agano (Mwanzo 17).

Ukristo[hariri | hariri chanzo]

Yesu mwenyewe alitahiriwa siku ya nane kama Wayahudi wote wa kiume. Tohara ya Yesu inakumbukwa kwa sikukuu maalumu katika makanisa mengi duniani hasa Waorthodoksi.

Agano Jipya inaonyesha jinsi gani suala la tohara lilikuwa motomoto mwanzoni mwa Kanisa, wakati Wakristo wengi walitoka katika Uyahudi.

Kufuatana na kitabu cha Matendo ya Mitume (15:23-29) Mtaguso wa Mitume uliofanyika Yerusalemu uliamua Wakristo kutoka mataifa wasilazimishwe kutahiriwa.

Hasa Mtume Paulo alisisitiza kwamba jambo hilo si muhimu tena, cha maana ni kuwa watu wapya kwa imani.

"Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya" (Gal 6:15).

"Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili" (Fil 3:3).

Hata hivyo Wakopti wa Misri na Ethiopia wameendelea kutahiri watoto wao.

Uislamu[hariri | hariri chanzo]

Katika Uislamu tohara hufundishwa kama wajibu wa kidini kwa kila mwanaume.

Hakuna amri katika Kurani kuhusu tohara lakini inatazamiwa kama sunna ya mtume Muhamad. Kwa imani hiyo ni ishara ya mitume ya kwamba walizaliwa bila govi katika hali ya kutahiriwa tayari.

Utekelezaji wa tohara huwa ni tofauti kati ya nchi na nchi; mara nyingi mtoto mdogo hutahiriwa kwa umri kati ya miaka 5 hadi 10. Katika mazingira ya mjini wazazi wanawahi siku hizi kutahiri mapema.

Tohara kama hatua ya kiafya[hariri | hariri chanzo]

Yasiyo ya upasuaji wazima tohara.

Siku hizi hata mataifa yasiyokuwa na desturi hiyo yanaanza kuijali kwa sababu za usafi na afya.

Ni kwamba tohara inapunguza hatari ya mtoto kupatwa na fimosis.

Imethibitishwa kuwa inapunguza uwezekano wa kuambukizwa ukimwi pamoja na hatari ya magonjwa mengine kama kansa ya uume.

Katika nchi kadhaa sehemu kubwa ya watoto wa kiume wanatahiriwa mara baada ya kuzaliwa kwa sababu hizi za kiganga. Kwa mfano, huko Marekani asilimia 56 za wavulana wote waliozaliwa mwaka 2005 walitahiriwa katika hospitali walikozaliwa. Hata hivyo katika nchi hiyo kuna kampeni dhidi ya tohara kutokana na hoja ya kwamba mara nyingine upasuaji hauendi vizuri na kusababisha madhara ya kudumu kwa viungo vya uzazi.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]