Nenda kwa yaliyomo

Muhammad

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mtume Muhamad)
Mtume Muhammed jinsi alivyotengeneza Kaaba huko Makka - picha mnamo mwaka 1315 kutoka Asia ya Kati
Mtume Muhammed jinsi alivyosali mbele ya Kaaba - (katika picha za Kiosmani uso wa mtume hufichwa mara nyingi tangu karne ya 16 BK)

Muhammad (kwa Kiarabu "Mwenye kusifika sana"; jina kamili kwa kirefu ni
محمد بن عبد الله بن عبد ﺍﻟﻤﻄﻠﺐ ﺍﻟﻬﺎﺷﻤﻲ Muhammad bin 'Abd Allāh bin 'Abd al-Muţţalib al-Hāshimī) anaaminika katika dini ya Uislamu kuwa ni mtume wa mwisho wa Mungu (Allah) kwa binadamu.

Utoto wake

Muhammad alizaliwa yatima kwani baba yake alifariki kabla yeye hajazaliwa. Hakuishi sana na mama yake (Amina), kwa kuwa naye alifariki dunia Muhammad akiwa na umri wa miaka sita.

Baadaye akachukuliwa na babu yake Abdul Muttalib na kuishi naye kwa muda wa miaka miwili, kisha babu yake naye akafariki.

Kazi ya kumlea Muhammad ilimwangukia ami yake Abu Talib ambaye ndiye aliyeishi naye mpaka ukubwa na kumuoza na kumpa himaya wakati alipoanza kazi ya kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu.

Kadiri ya hadithi za Kiislamu, ilipokua karibu atadhihiri Mtume mapadri wa Kinasara na makuhani wa Kiyahudi waliokuwa wakikaa Bara Arabu walikuwa wakiwatahayarisha majirani wao wa Kiarabu waliokuwa wakiabudu sanamu, wakiwaambia: “Karibu ataletwa Mtume katika nchi yenu hii, abatilishe hii ibada yenu mbovu ya sanamu”. Walipoambiwa hivi wale Waarabu waliwauliza jina la Mtume huyo, wakawajibu kuwa jina lake litakuwa Muhammad. Kwa hivyo kila mwenye kusadiki hayo alimwita mwanawe Muhammad.

Lakini hayakusikilizana majina haya ila kwa baadhi ya Waarabu waliokua wakikaa Shamu tu na Najran (Yaman) ambako mapadri wengi walikaa, na vilevile katika Madina ambayo nusu ya wakazi wake walikuwa Wayahudi.

Hata lilipoanza kutangaa jina la Mtume, waliokuwa wamekwisha kuitwa kwa jina hilo walikuwa wachache tu Bara Arabu nzima.

Inasemekana Mtume aliinukia tangu utotoni kwake juu ya sifa zake nzuri na ukomavu wa akili ya kiutu uzima, hakupata kufanya vitendo vya utoto umri wake, wala kuazimia kuvifanya ila mara mbili tu, ambazo mara mbili zote hizo Mwenyezi Mungu alimhifadhi navyo.

Kitendo chenyewe alichokiazimia kukifanya mara mbili zote hizo na Mwenyezi Mungu akamhifadhi nacho ni kutaka kwenda kukesha katika ngoma za arusi mbili za marafiki wake waliooa katika mji wa Makka.

Lakini Mungu alimpa usingizi mkubwa katika masiku yote hayo mawili hata hakuweza kufumbua jicho, wala kunyanyua miguu kwenda mahali. Hajapata kuhudhuria hata mara moja katika ibada za kuabudu sanamu wala kula chakula kilichochinjwa kwa ajili yao. Moyo wake ulichukizwa na hayo na mambo mengine yaliyo mabaya.

Tangu udogo wake Mtume aliondokea na sifa nzuri ambazo hapana hata mmoja katika hirimu zake aliyekuwa nazo zote. Kila sifa zinazohesabiwa kuwa ni njema na Waislamu ndizo alizokuwa nazo tangu utoto wake.

Mkewe Aisha alipoombwa kutaja kidogo sifa za Mtume, alisema hivi: “Sifa zake ni zile sifa nzuri zinazosifiwa na Qurani” na katika Qurani zimetajwa chungu ya sifa zilizo nzuri.

Mtume mara nyingi alikuwa akisema: “Sikupata kufanya hata siku moja yale mambo waliyokuwa wakiyafanya makafiri”. Kwa hivyo yeye hakupata kuabudu sanamu, kulewa, kuzini, kucheza kamari wala hakumdhulumu mtu kitu chake na kama haya.

Lakini alikuwa msemakweli, mwaminifu, mpole na mwenye haya na sifa nyingi nyinginezo bora kama hizi. Watu wa Makka walikuwa wakimsifu kwa tabia zake, hata wakampa jina la Muhammad Al-Amin (mwaminifu). Alikuwa hatajikani ila kwa jina la Al-Amin.

Wakubwa na wadogo walikuwa wakimheshimu na kumpa amana zao kuwawekea, hata baada ya utume.

Hali yake kabla ya kupewa utume

Makureshi ni watu wa biashara, kila Kureshi alipata kufanya kazi hii.

Safari moja baadhi yao walipokuwa wakienda Yaman katika biashara zao, baba yake mdogo wa pili Bwana Zubeyr alimshauri ikiwa atapenda kusafiri. Mtume aliridhia akenda naye mpaka Yaman, wakakaa huko muda wa siku tatu tu kisha wakarejea, wakati huu Mtume alikuwa mtoto wa miaka tisa.

Hata alipotimia miaka 12 mwaka 582, alisafiri tena pamoja na baba yake mdogo mwingine, Bwana Abu Talib; safari hii waliazimia kwenda Shamu, lakini walipofika Busra – mji wa kusini kabisa katika nchi ya Shamu – walikutana na padri jina lake Bahyra ambaye alimkataza asisogee na mwanawe zaidi kuliko hapo, akamwambia: “Mtoto huyu namwona ana alama zote za Mtume aliyetabiriwa kuwa atakuja, basi naona ni hatari kubwa akienda Shamu, asije akauawa na Wayahudi huko. Nakusihi sana urejee naye, au umpe mtu mwaminifu arejee naye, nawe uende katika biashara zako”. Abu Talib alimpa mtu arejee naye Makka naye akaendelea na safari yake.

Huyu padri Bahyra alikuwa mwanachuoni wa Kinasara, na alimbashiri Mtume lakini hakuwahi kumwamini alipoanza utume, ila mwanafunzi wake Salman Al-Farsy Mwajemi mara alipopata habari ya kupata utume wake alisilimu, na aliusaidia Uislamu katika mambo mengi.

Baada ya kutimia miaka 15 Mtume aliingia katika kufanya biashara ndogondogo yeye na mwenziwe Saib bin Yazid, lakini biashara yao walikuwa wakiifanyia katika miji iliyokuwa karibu na Makka tu. Alipata sifa kubwa ya uaminifu na ukweli katika biashara zake hizi. Mshirika wake huyu alisilimu siku ilipotekwa Makka, na Mtume alifurahi sana kwa kusilimu rafiki yake huyu.

Kuanza utume

Sehemu ya mfululizo wa makala juu ya

Uislamu

Imani na ibada zake

Umoja wa Mungu
Manabii
Misahafu
Malaika
Uteule
Kiyama
Nguzo za Kiislamu
ShahadaSwalaSaumu
HijaZaka

Waislamu muhimu

Muhammad

Abu BakrAli
Ukoo wa Muhammad
Maswahaba wa Muhammad
Mitume na Manabii katika Uislamu

Maandiko na Sheria

Qur'anSunnahHadithi
Wasifu wa Muhammad
Sharia
Elimu ya Sheria za KiislamuKalam

Historia ya Uislamu

Historia
SunniShi'aKharijiyaRashidunUkhalifaMaimamu

Tamaduni za Kiislamu

ShuleMadrasa
TauhidiFalsafaMaadili
Sayansi
SanaaUjenziMiji
KalendaSikukuu
Wanawake
ViongoziSiasa
Uchumi
UmmaItikadi mpyaSufii

Tazama pia

Uislamu na dini nyingine
Hofu ya Uislamu

Muhammad hakuwa akihudhuria sikukuu za Wapagani tangu kufahamu kwake. Alikuwa akipenda kukaa peke yake. Kufanya haya kulikuwa kukimwonjesha raha kubwa kuliko kutoka mbele za watu akaona yale mambo yao mabaya aliyokuwa akiyachukia. Kila usiku ukicha alikuwa akizidi kuyachukia. Lakini alikuwa hajui la kufanya.

Hata alipotimiza miaka 38 hakuweza tena kustahimili kuona zile ibada za sanamu na tabia mbovu walizokuwa nazo wenziwe, ilivyokuwa hana la kufanya katika kuzizuia, alifanya shauri kuuacha mji wa Makka na kwenda porini kukaa.

Akapata pango zuri katika Jabal Hira Kaskazini ya Makka, inapata maili 3 toka huko Makka. Akawa akikaa huko kwenye Jabal Hira kwa muda wa wiki nyingi, kisha hurejea Makka kuja kumtazama mkewe, wanawe na jamaa zake wengine, na vile vile kwa ajili ya kuchukua chakula kinapokuwa kimekwisha.

Wakati mwingine akikaa siku nyingi sana huko porini hata humpasa mkewe Khadija kwenda kumsikiliza na mara nyingine alikuwa akifuatana naye, pamoja na watoto wao.

Alidumu katika hali hii muda wa miaka miwili na kitu.

Baadaye alisimulia kuwa katika mwezi wa Ramadhani 17, Jumatatu katika mwaka wa 40 unusu wa umri wake alimuona mtu kamsimamia mbele yake bila ya kumuona wapi katokea, akamwambia: “Soma”. Mtume akamjibu: “Mimi sijui kusoma kwani sijapata kujizunza”. Akaja, akamkamata, akambana, akamwambia tena: “Soma”. Mtume akamjibu jawabu yake ileile. Hata mara ya tatu akamwambia: “Soma – Iqraa Bismi Rabbik - ” akamsomea sura ya 96 mpaka kati yake, kisha Mtume akaisoma kama alivyosomewa. Hii ndiyo sura ya kwanza kushuka katika Qurani, ingawa haijawekwa mwanzo.

Mara yule mtu (malaika) akaondoka machoni pake asimwone kaenda wapi, naye akarejea kwake hofu imemshika.

Alipofika nyumbani, Khadija alidhani ana homa, akamfunika nguo gubigubi akakaa mbele yake akimsikiliza anavyoweweseka. Homa ilipomwachia alimweleza Khadija yote yaliyomtokea, naye akamtuliza moyo wake, akamyakinishia ya kuwa hapana lolote baya litakalomzukia.

Mara Bibi huyu akaondoka akaenda kwa jamaa yake Waraqa bin Naufal akampa habari yote iliyompata mumewe. Naye akamwamrisha amwite, na Mtume akaenda akamweleza habari yake yote. Bwana Waraqa akamwambia: “Huyo ndiye Jibril aliyemshukia Nabii Musa na Nabii Isa. Basi jibashirie kuwa wewe ni Mtume wa Umma huu! Nami natamani kuwa hai nikuone unavyosimama kuwatengeneza jamaa zako, Inshaalla nitakuwa mkono wako wa kulia!”.

Wakarejea kwao hofu yote imemtoka Baada ya kuazimia kuwa hatakwenda tena kule pangoni.

Pale pale akaondoka akenda pangoni mwake ili aonane na malaika tena, ingawa alikaa huko muda mrefu.

Siku ile ya kupata Utume inawafiki mwezi wa Desemba 610.

Huyu Waraqa hakuwa akiabudu dini ya sanamu bali alikuwa Mkristo, alipokuwa akisoma vitabu aliona kutatokea Mtume mwingine, ndiyo maana alipohadithiwa habari ile mara moja akaamini kuwa aliyemjia Mtume ni Jibril.

Maisha yake Makka

Muhammad aliishi Makka kwa muda wa miaka 53, arubaini (40) katika hiyo akiwa ni mtu wa kawaida kabla ya kupewa utume, na 13 akiwa ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.

Maisha yake Makka yalikuwa ya taabu tangu utotoni mwake, kwani alizaliwa yatima kisha alipokuwa katika ujana wake alikuwa akifanya kazi ya kuchunga mbuzi na kondoo wa watu wa Makka kwa vijipesa kidogo mpaka alipofika umri wa miaka ishirini na tano akapata kazi ya kumfanyia biashara Khadija, bibi mtukufu wa Kikureshi ambaye baadaye alikuja kuwa mkewe, na kuzaa naye aghlabu ya watoto wake.

Miaka 13 ya utume Makka

Katika miaka 13 aliyoyaishi hapo Makka baada ya kupewa utume, Muhammad alipata kila aina ya mateso na masumbuko, juu ya nafsi yake na juu ya wafuasi wake, naye alisubiri na kustahimili kila aina ya taabu na shida kwa ajili ya Mola wake, mpaka Mwenyezi Mungu alipompa amri ya kuhama mji huo na kuelekea Madina.

Katika muda huu alipokuwa Makka, wengi katika jamaa zake na watu wa makabila mengine wa matabaka mbalimbali za jamii waliingia dini yake.

Mwaka 622 Wakureshi, wakiona hasara katika mafungamano yao na Waarabu wengine wenye kuabudu miungu mingi, kwa dukuduku zao zilimfanya Muhammad ahame pamoja na sahibu wake Abubakar Assiddiq na wafuasi wake 70 hivi akaishi Yathrib, mji ambao ulikaliwa na Waarabu na Wayahudi pamoja na ambao baadaya ukaitwa Madinat al-Nabi (yaani Mji wa Nabii, kifupi Madina).

Mwaka huo ukawa wa kwanza katika Kalenda ya Kiislamu inayotumika tangu wakati wa halifa 'Omar ibn al-Khattàb hadi leo.

Kuhamia Madina na mwanzo wa Umma

Mtume Muhammad, baada ya kupewa amri ya kuguria Madina, aliondoka na kuhamia mji huo ambao ulimpokea na kumkubali na kumsaidia na kumtukuza na kumlinda na maadui.

Ingawa Wayahudi wa Madina walikataa kumsadiki kuwa nabii kama wale wa Biblia, aliendelea kuhubiri huko na tangu mwaka wa kwanza alitunga Hati ya Agano iliyokubaliwa na Wamadina wote: ndiyo asili ya Umma, jamii ya waumini.

Mtume Muhammad aliishi Madina kwa muda wa miaka 10 mingine akitangaza dini ya Mwenyezi Mungu na huko watu wengi na makabila mbali mbali ya Kiarabu yaliingia dini ya Uislamu kwa makundi makundi.

Wakati huohuo alianza kushambulia misafara ya Wamakka wapagani na kuwashinda kwanza huko Badr (624), akashindwa huko Uhud (625), hatimaye akapata ushindi mkuu huko Madina katika vita vya handaki (627): hapo alifukuza na hatimaye akaangamiza kama wasaliti Wayahudi wote wa Madina na wanaume wote wa Waqurayza, wakati wanawake wao pamoja na watoto wakauzwa kama watumwa huko Syria.

Mwaka 630 Muhammad akiwa na nguvu za kutosha aliweza kurudi Makka na kuiteka, akairudisha Kaaba ambayo ndiyo kibla cha Waislamu wote ulimwenguni katika mambo ya Sala na Hija.

Hata hivyo akarudi kuishi Madina na kutoka huko akaeneza kazi yake ya kisiasa na ya kidini katika Hijaz yote. Baada ya ushindi wake huko Hunayn dhidi ya Waawazin na wenzao, aliteka au kusilimisha vijiji mbalimbali vya maana upande wa uchumi au wa vita kwa mfululizo wa mapigano kwenye Wadi al-qura.

Kwa jumla alihudhuria vita 27, akiua kwa mkono wake mtu mmoja tu.

Akiendelea kuishi Madina, alinadhimu kwa Sharia na hukumu nyingi maisha ya jamii ya Waislamu huko, na kuweka chanzo cha dola ya kiislamu ulimwenguni.

Sharia na hukumu hizo zinapatikana katika kitabu kitakatifu cha (Qurani), ambacho leo Waislamu wote ulimwenguni wananadhimu maisha yao kulingana nacho.

Wake zake

Ingawa Kurani inaruhusu wake 4 tu, Muhammad alisema ana idhini ya kuvuka kiwango hicho. Jumla alioa wake 11, ambao majina yao yamepangwa hapa chini kufuatana na tarehe ya ndoa.

1. Khadija binti Khuwaylid (tangu 595 hadi kifo chake Januari 620) ambaye aliwahi kuolewa na waume wawili na kuwazalia watoto 5. Katika maisha mazuri ya ndoa alimzalia Muhamad mabinti 4 (Ruqayya, Umm Khulthūm, Zaynab na Fatima), mbali na watoto 2 wa kiume (Qàsim na ‘Abd Allah) ambao lakini walikufa wakiwa bado wadogo.

2. Sawda binti Zam’a (tangu Machi 620) aliyewahi kuolewa na mume mmoja.

3. Aysha binti Abu Bakr (tangu Januari 623) aliyeolewa na Mohamed akiwa na umri wa miaka 9.

4. Hafsa binti Umar (tangu Novemba 624), aliyewahi kuolewa na mume mmoja.

5. Zaynab binti Khuzayma (tangu Juni 625 hadi kifo chake Agosti 625).

6. Hindi Umm Salama binti Abi Umayya (tangu Februari 626), aliyewahi kuolewa na mume mmoja na kuachiwa watoto wengi. Alikuwa mtoto wa kambo wa shangazi ya Mohamed.

7. Zaynab binti Jahsh (tangu Juni 626) aliyeachwa na mume wake. Alikuwa binamu wa Mohamed.

8. Juwayriya binti Al Harith (tangu Desemba 626).

9. Ramla Umm Habība binti Abi Sufyan (tangu Agosti 628) alipoachana na mumewe aliyeingia Ukristo.

10. Safiyya binti Huyay (tangu Septemba 628) ambaye alikuwa Myahudi akatekwa nyara katika vita vya Khybar.

11. Maymuna binti Harith (tangu Februari 629) aliyekuwa na umri wa miaka 51.

Kati yao, wa kwanza tu alimzalia Muhammad watoto, lakini wana wote walifariki kabla ya baba yao, isipokuwa Fatma aliyekufa miezi sita baada yake.

Aliwaoa pia, lakini bila ya kulala nao, Asma’ binti Al Nu‘man (mkoma) na ‘Amra binti Yazid (aliyekataa katakata ndoa hiyo akapewa mara talaka).

Mbali na wake rasmi, Kurani inaruhusu kuwa na masuria wasio na idadi (dhāt al-yamīn, "waliomilikiwa na mkono wa kuume", yaani watumwa, hasa waliotekwa vitani). Muhammad alikuwa nao 16: kati yao Marya (Mkristo) alimzalia mtoto wa kiume: Ibrahim, aliyefariki mdogo sana, kwa huzuni kubwa ya baba yake aliyemfuata kaburini muda mfupi baadaye.

Marejeo

  • KADHI SHEIKH ABDULLA SALEH FARSY, Maisha ya Nabii Muhammad - Mulla Karimjee Mulla Mohamedbhai & Son, Zanzibar 1942

Viungo vya nje

Visivyotolewa na Waislamu
Vilivyoandikwa na Waislamu

Kujisomea

Kamusi elezo

  • William H. McNeill, Jerry H. Bentley, David Christian, ed. (2005). Berkshire Encyclopedia of World History. Berkshire Publishing Group. ISBN 978-0-9743091-0-1
      .
  • Richard C. Martin, Said Amir Arjomand, Marcia Hermansen, Abdulkader Tayob, Rochelle Davis, John Obert Voll, ed. (2003). Encyclopedia of Islam & the Muslim World. MacMillan Reference Books. ISBN 978-0-02-865603-8
      .
      .
  • Lindsay Jones, ed. (2005). Encyclopedia of Religion (2nd ed.). MacMillan Reference Books. ISBN 978-0-02-865733-2
      .
      .
      .
  • The New Encyclopædia Britannica (Rev ed.). Encyclopædia Britannica, Incorporated. 2005. ISBN 978-1-59339-236-9
      .