Bara Arabu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Bara Arabu

Bara Arabu ni ile sehemu ya dunia iliyoko baina ya Bara la Afrika na Bara la Asia ambayo sehemu kubwa yake imezungukwa na bahari, upande wa magharibi na Bahari ya Shamu, upande wa kusini na Bahari ya Hindi na mwengine wa Mashariki na Ghuba ya Uajemi. Sehemu za Kaskazini mwa Bara Arabu imepakana na nchi za ufalme wa Jordani na jamhuri ya Iraq.

Kwa sababu ya makame hakuna mito ya kudumu katika bara hili ijapokuwa kwenye sehemu mbali mbali kunapatikana chemchemu na vijito vya maji ambavyo huzidi wakati wa msimu wa mvua katika majira ya baridi. Sehemu kubwa ni jangwa tu. Bara Arabu ina milima upande wa Magharibi na Kusini mwake, lakini kila ukiteremkia Mashariki unakutana na ardhi tambarare mpaka kufikia kwenye Ghuba ya Uajemi.

Eneo la Bara Arabu[hariri | hariri chanzo]

Eneo la Bara Arabu kwa jumla ni 3,191,022 kilomita muraba, ikiwa Saudia inakalia sehemu nne katika tano ya jumla ya maeneo yake, na sehemu iliyobakia ambayo ni moja katika tano inakaliwa na nchi zilizobakia, zote zikiwepo pembezoni mwa Saudia kwenye bahari ya Ghuba ya Uajemi na bahari ya Waarabu na bahari ya Shamu.

Nchi za Bara Arabu[hariri | hariri chanzo]

Nchi zilizokuweko kwenye bara hili ni Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudia, Muungano wa Falme za Kiarabu, na Yemen. Sita za mwanzo zikiwemo kwenye Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba, zina mfumo wa kifalme katika utawala wake, na ya mwisho ni Jamhuri ya Yemen. Nchi hizi zina historia ndefu inayorudi nyuma kabla ya kuja Uislamu, na ustaarabu mbali mbali ulipatikana katika maeneo mbali mbali ya nchi hizi. Katika ustaarabu mashuhuri wa nchi hizi ni ule ustaarabu wa nchi ya Yemeni, ambao ulikuwa ukijulikana kuwa ni ustaarabu wa Sabaa zama za Balqis, malkia wa Yemen wa wakati huo.

Miji Mikuu[hariri | hariri chanzo]

Kuna miji mingi katika Bara Arabu, lakini miji mikuu ya madola mbali mbali ya Bara Arabu ni Riyadh, mji mkuu wa Saudia, ijapokuwa kuna miji mashuhuri na mitukufu katika Saudia kama Makka na Madina. Mji mkuu wa Yemeni ni Sanaa, lakini mengine muhimu ni Aden, Hudeidah, Taez, Mukalla, Shibam na Seyun. Ama mji mkuu wa Oman ni Maskat, lakini kuna miji mengine mashuhuri yenye tarehe kubwa kama Salala, Sohari, Nizwa na Rustaq. Mji mkuu wa Falme za Kiarabu ni Abu Dhabi, na mengine mashuhuri ni Dubai, Sharjah, Ajman, Ras-al-Khayma, Ummul-Quwain na Fujairah. Kuwait, mji mkuu wake ni Kuwait, na Qatar mji mkuu wake ni Doha, na Bahrain ni Manama.

Hali ya hewa[hariri | hariri chanzo]

Nusu Kisiwa cha Bara Arabu kina jangwa kubwa la Rub al Khalikusini mwake na An-Nafud kaskazini mwake. Ni sehemu ya ulimwengu ambayo haina mvua nyingi na ukame ndio tabia ya nchi zilizokuwemo katika bara hili, na kwa hivyo, hali ya hewa huwa ni joto sana katika majira ya joto kufikia hadi daraja 55 . katika baadhi ya sehemu zake, na kufikia daraja hadi 0 C° katika baadhi ya sehemu nyengine katika majira ya baridi.

Idadi ya Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Idadi ya wakaazi wa nchi hizi saba kwa ujumla inafikia 50,000,000, wakiwemo asilimia 85 wenyeji na asilimia 15 wageni. Wenyeji au wananchi wa nchi hizi aghlabu yake ni Waarabu, lakini pia kuna Wajemi, Mabulushi, Wahindi, Mabangladeshi, Wazungu, Mapakistani, Waafrika na kabila nyenginezo.

Dini[hariri | hariri chanzo]

Nchi zote saba zilizokuwepo kwenye Bara Arabu ni za kiislamu, na aghlabu ya Waislamu wake ni wa madhehebu ya Sunni, lakini pia kuna madhehebu ya Shia na Ibadhi kwenye baadhi ya nchi hizi. Asilimia 99% ya wananchi wa nchi hizi ni Waislamu, lakini vile vile kuna wafuasi wa dini nyenginezo katika wakazi wake, kama Mayahudi, Mabaniani, Wakristo na kadhalika.

Lugha[hariri | hariri chanzo]

Kiarabu ndio lugha inayotumika kwenye nchi hizi saba, na ndio lugha rasmi ya nchi hizi, lakini Kiingereza, karibuni, kimeanza kutumika sana kwa sababu ya kuwepo dharura ya kutumia lugha hii katika biashara, mawasiliano baina ya wananchi na wageni, na katika uhusiano wa kimataifa baina ya nchi mbali mbali ulimwenguni.

Mali Asili[hariri | hariri chanzo]

Bara Arabu ina aina nyingi ya madini na nishati. Kuna dhahabu, fedha, chumvi, na kadhalika. Inajulikana hasa kwa akiba zake kubwa za mafuta ya petroliamu na gesi, jambo lililofanya hizi nchi kutegemea zaidi mali asili hizi kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi zao na maendeleo mengine ya nchi.

Hapo zamani watu wa nchi hizi wakitegemea sana uvuvi, ufugaji wa wanyama kama mbuzi, kondoo, ng'ombe, ngamia na farasi. Aidha, walikuwa wakilima na kupanda mitende, matunda, ngano na shayiri, na kwa hivyo, bidhaa zao walizokuwa wakisafirisha nje zilikuwa zaidi ni tende, buni, samaki na papa wakavu, na ngozi za wanyama.