Samia Suluhu Hassan

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Samia Suluhu Hassan


Rais
Aliingia ofisini 
17 Machi 2021

tarehe ya kuzaliwa 27 Januari 1960 (1960-01-27) (umri 64)
Usultani wa Zanzibar
utaifa Mtanzania
chama Chama Cha Mapinduzi
ndoa Hafidh Ameir
watoto Mwanu Hafidh Ameir,Wanu Hafidh Ameir
mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe
Chuo Kikuu cha Manchester
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
SNHU
dini Uislamu

Samia Suluhu Hassan (alizaliwa 27 Januari 1960) ni Rais wa 6 wa Tanzania na mwanachama wa chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi.[1]

Kabla ya kuwa rais kutokana na kifo cha John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, Suluhu alikuwa makamu wa rais kwa sababu ya kuwa mgombea mwenza katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.[2]

Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa kama makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa mwanamke wa kwanza kufikia cheo hicho, akarudia baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2020.

Sasa amekuwa rais wa kwanza mwanamke na rais wa Pili kutoka Zanzibar Wa kwanza Akiwa ni Ally Hassan Mwinyi Rais wa awamu ya Pili.

Maisha ya awali

Suluhu alizaliwa katika Usultani wa Zanzibar.

Alisoma shule za msingi za Chwaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) katika miaka ya 1966 hadi 1972.

Aliendelea na masomo ya sekondari shule za Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976)[3].

Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari mnamo 1977, aliajiriwa na Wizara ya Mipango na Maendeleo kama karani. Alifuata kozi fupi kadhaa. Mnamo 1986, alihitimu kutoka Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo (Chuo Kikuu cha Mzumbe cha leo) na diploma ya hali ya juu katika utawala wa umma. [4]

Baada ya kuhitimu, aliajiriwa kwenye mradi uliofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme). Kati ya miaka 1992 na 1994, alisoma kwenye Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza na kuhitimu stashahada ya uzamili katika uchumi. [5]

Mnamo mwaka 2015, alipata MSc yake katika Maendeleo ya Uchumi wa Jamii kupitia mpango wa pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Kusini mwa New Hampshire. [6]

Kazi ya siasa

Mnamo mwaka 2000 aliamua kujiunga na siasa. Aliteuliwa na CCM kama mbunge wa viti maalum katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar akateuliwa na rais Amani Karume kuwa waziri wa utalii na bishara. Alikuwa mwanamke pekee kwenye ngazi ya mawaziri akaona alidharauliwa na wenzake wa kiume kwa sababu ya jinsia yake. [7] Alichaguliwa tena mnamo 2005 kwenye viti maalum na aliteuliwa tena kama waziri katika wizara ya kazi, jinsia na watoto. [8]

Mwaka 2010 aligombea kwenye uchaguzi kwa Bunge la Kitaifa, akisimama katika jimbo la Makunduchi na kushinda kwa zaidi ya % 80. [9] Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Nchi wa Mambo ya Muungano. [10] Mnamo 2014, alichaguliwa kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba iliyokuwa na jukumu la kuandaa katiba mpya ya nchi. [11] Mnamo tarehe 30 Aprili 2021 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM [12] akiwa mwenyekiti wa kwanza mwanamke.

Makamu wa Rais

Mnamo Julai 2015, mteule wa urais wa CCM, John Magufuli alimchagua kuwa mgombea mwenza wa uchaguzi wa 2015 na kumfanya kuwa mgombea mwenza wa kwanza mwanamke katika historia ya chama hicho. [13] Baadaye alikuwa makamu wa rais wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi kutokana na ushindi wa Magufuli katika uchaguzi. [14]

Maisha ya binafsi

Mnamo 1978 aliolewa na Hafidh Ameir aliye kwa sasa afisa kilimo mstaafu. Wana watoto wanne: binti mmoja na wavulana watatu. [15] Binti yake Wanu Hafidh Ameir (aliyezaliwa 9 Februari 1982), mtoto wa pili, ni mbunge wa viti maalum katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar. [16]

Tanbihi

  1. Member of Parliament CV. Bunge la Tazania. Jalada kutoka ya awali juu ya 2015-07-13. Iliwekwa mnamo 19 February 2013.
  2. Mgombea mwenza Urais 2015 wa Mhe. John Pombe Magufuli ni..
  3. [https://www.bbc.com/swahili/habari/2015/07/150712_profile_ccm_amina_salum_ali Wasifu wa makamu wa rais wa Tanzania Samia Hassan], tovuti ya BBC 13.07 / 05.11. 2015
  4. Member of Parliament CV. Parliament of Tanzania. Jalada kutoka ya awali juu ya 13 July 2015. Iliwekwa mnamo 19 February 2013.
  5. https://www.tanzania.go.tz/profiles/profiles/details/138 Archived 22 Septemba 2020 at the Wayback Machine. Profile Details : Former VP of Tanzania, Tovuti ya serikali ya Tanzania, iliangaliwa Machi 2021
  6. Member of Parliament CV. Parliament of Tanzania. Jalada kutoka ya awali juu ya 13 July 2015. Iliwekwa mnamo 19 February 2013.
  7. Samia Suluhu Hassan, a tough journey, gazeti la Daily News, tarehe 18 Septemba 2014
  8. Tovuti ya Bunge 2010-2015
  9. Samia Suluhu Hassan, a tough journey, gazeti la Daily News, tarehe 18 Septemba 2014
  10. "Tanzania: History Made as Samia Picked Running Mate", AllAfrica, 13 July 2015. 
  11. "Tanzania: Union 'Stalwart' Samia Is CA Vice-Chairperson", AllAfrica, 14 March 2014. 
  12. https://www.bbc.com/swahili/live/habari-56939323
  13. Mohammed (12 July 2015). Tanzania's ruling party nominates John Magufuli as presidential candidate. Quartz. Jalada kutoka ya awali juu ya 11 August 2015. Iliwekwa mnamo 12 August 2015.
  14. "CCM's John Magufuli declared Tanzania fifth president". Retrieved on 2021-03-18. Archived from the original on 2015-10-31. 
  15. Samia Suluhu Hassan, a tough journey, gazeti la Daily News, tarehe 18 Septemba 2014
  16. Hon. Wanu Hafidh Ameir. www.zanzibarassembly.go.tz. Jalada kutoka ya awali juu ya 2021-03-18. Iliwekwa mnamo 2021-03-18.
Alitanguliwa na
John Magufuli
Rais wa Tanzania
2021-
Akafuatiwa na
[[]]