John Magufuli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
John Magufuli.

John Pombe Joseph Magufuli (amezaliwa 29 Oktoba, 1959) ni mwanasiasa nchini Tanzania. Anatokea katika chama cha CCM.

Alikuwa mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki katika bunge la kitaifa huko nchini Tanzania na tangu mwaka 2010 waziri wa ujenzi.[1]

Tarehe 12 Julai 2015 alichaguliwa kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi na mgombea mwenza ni Samia Suluhu Hassani.

Tarehe 29 Oktoba 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ulimtangaza kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wa kura 8,882,935 sawa na 58.46% pamoja na makamu wa rais Samia Suluhu Hassani.

Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa kama rais wa tano wa Tanzania, ingawa upinzani haujakubali matokeo hayo.

Tarehe 10 Desemba 2015 alitangaza baraza la mawaziri likiwa na watu 34 tu katika nafasi ya waziri au naibu waziri.

Elimu[hariri | hariri chanzo]

Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (20062009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia miaka 19911994 alisomea Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza na miaka 19851988, alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati. Kabla ya hapo Magufuli alisoma diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati, hiyo ilikuwa miaka 19811982.

Upande wa sekondari, Magufuli alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa huko Iringa kipindi cha miaka 1979 – 1981. Kabla ya hapo miaka 19771978, alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza na miaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera. Hapo kati alikwenda Jeshi la Kujenga Taifa huko Arusha kwa mujibu wa sheria.

Ameandika vitabu na majarida mbalimbali..

Uzoefu wa kazi[hariri | hariri chanzo]

Magufuli alipomaliza elimu yake pande za Mkwawa mwaka 1982 akaanza kutumia taaluma yake ya Kemia na Hisabati kwa kufundisha shule ya Sekondari Sengerema hadi mwaka 1983.

Baada ya hapo akafanya kazi kama Mkemia katika Chama cha Ushirika cha Nyanza huko Mwanza hadi mwaka 1995 kisha akaanza safari yake ya siasa kwa kugombea ubunge mwaka 1995 huko Biharamulo Mashariki, kazi ambayo anaifanya hadi tarehe 1 Agosti 2015.

Akiwa Mbunge wa Biharamulo Masahriki huko Chato amekuwa Naibu Waziri na Waziri katika Wizara mbalimbali. Tangu mwaka 2000 hadi 2005 alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki. Mwisho 2010 – 2015: Waziri wa Ujenzi.

Urais[hariri | hariri chanzo]

Ndani ya mwezi mmoja tangu alipoingia madarakani ameanza kudhibiti matumizi mabaya ya fedha ndani ya serikali kwa kufuta baadhi ya sherehe zizizo na ulazima pamoja na kupambana kwa dhati na wakwepakodi.

Hivyo amefanikiwa kujenga imani kwa wananchi wengi wa Tanzania ambao kwa kiasi kikubwa walionyesha kuchoshwa na uongozi wa chama chake.

Wananchi wa Tanzania, nchi jirani na baadhi ya mataifa makubwa wamepongeza utendaji wake, ingawa wengine wanajiuliza kama kasi hiyo itaendelea.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Mengi kuhusu John Pombe Joseph Magufuli (18 Februari 2008). Iliwekwa mnamo 11 Novemba 2011.