Historia ya Tanzania
Historia ya Tanzania inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Historia ya awali
Nchi ina mabaki ya kale sana ya zamadamu (kiumbe aliyekaribiana na binadamu kwa umbile). Sehemu ya Bonde la Ufa, kama Bonde la Oltupai (zamani Olduvai Gorge) lililoko ndani ya hifadhi ya Serengeti, ndiko kulikogunduliwa masalia ya viumbe wa jamii ya watu wa kale yenye umri mkubwa kuliko yote yanayojulikana duniani hadi hivi sasa.
Kutokana na ugunduzi huo, baadhi ya wanasayansi duniani wanaamini kuwa Tanzania bara ni chimbuko la binadamu. Ushahidi wa kisayansi unatokana na nyayo za zamadamu zilizogunduliwa katika eneo la Laetoli lililoko kusini kidogo mwa Oltupai, umeongeza uzito wa hoja ya Tanzania kuwa chimbuko la binadamu.
Binadamu wa kwanza kuishi huko huaminiwa kuwa wawindaji-wakusanyaji wa jamii ya Wasani, halafu Wabilikimo. Wa kwanza wanaendelezwa na wajukuu wao Wasandawe, kabila la pili limemezwa na makabila mengine
Milenia za mwisho Kabla ya Kristo walihamia huko Wakushi kutoka kaskazini, nao wakameza kwa kiasi kikubwa wakazi asili, wakaingiza kilimo, ufugaji na uzalishaji kwa jumla. Wairaqw wa leo ni wajukuu wa wahamiaji hao.
Inajulikana kwamba pwani za Tanzania pamoja na pwani za Afrika ya Mashariki kwa jumla zilitembelewa na mabaharia kutoka nchi za mbali; taarifa ya kwanza ya kimaandishi inapatikana katika kitabu cha "Periplus ya Bahari ya Eritrea" kilichotungwa mnamo mwaka 200 BK. Pwani hizo zilikuwa mapema sehemu ya biashara ya kimataifa katika Bahari Hindi. Asili ya miji ya Waswahili inapatikana katika biashara hiyo.
Katika karne za kwanza BK walifika kwa awamu kutoka magharibi wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi. Nao wakameza kwa kiasi kikubwa wakazi waliotangulia. Makabila mengi sana ya leo katika Tanzania ni wajukuu wa wahamiaji hao.
Hatimaye Waniloti kutoka kaskazini walizidi kuingia hadi karne ya 18. Mababu wa Wajaluo na Wamasai walifika katika mwendo huu.
Miji ya Waswahili ilikua kufuatana na mabadiliko ya biashara ya kimataifa; kufika kwa Wareno baada ya mwaka 1500 ilileta vurugu kwa muda, ilhali miji kadhaa ya Waswahili walishikamana nao na miji mingine iliwapinga. Hatimaye watawala wa Omani waliingilia kati na kuwafukuza mabaki ya Wareno na kwa njia hiyo kuunda kipindi cha ukuu wa Sultani wa Oman juu ya miji ya pwani.
Kabla ya kufika kwa ukoloni kulikuwa na madola madogo mbalimbali na maeneo madogo ya kikabila.
Kanda la pwani pamoja na njia za misafara kuelekea Ziwa Tanganyika vilikuwa chini ya athira ya Usultani wa Zanzibar ulioanzishwa baada ya Sultani wa Omani kuhamia Unguja.
Usultani wa Zanzibar
Usultani huo ulikuwa nchi kwenye pwani ya Afrika mashariki kati ya 1856 na 1964.
Tangu 1890 ilikuwa nchi lindwa chini ya Uingereza.
Ilianzishwa wakati wa kugawa Usultani wa Omani mwaka 1856 ikaishia mwaka 1964 baada ya mapinduzi ya Zanzibar na muungano na Tanganyika uliozaa Tanzania.
Sayyi Said kuhamia Unguja
Usultani ulianzishwa wakati Sultani Sayyid Said alipoamua kuhamisha makao makuu yake kutoka Maskat (Omani) kwenda Unguja.
Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki.
Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini.
Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini.
Biashara ya karafuu na watumwa
Sayyid Said aliona nafasi kubwa ya biashara ya karafuu kwa ajili ya soko la Uhindi na kwingineko. Mwaka 1829 akaanzisha mashamba ya mikarafuu kwa kutumia kazi ya watumwa kutoka bara.
Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno.
Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka.
Nchi za nje zikatambua mji mkuu mpya na kujenga uhusiano. Ubalozi wa Marekani ulijengwa mwaka 1837, Uingereza ukafuata mwaka 1841 na Ufaransa mwaka 1844.
Sultani mwenyewe aliondoka kabisa Maskat mwaka 1840. Kukua kwa Zanzibar kulisababisha kukonda kwa mji wa Maskat
Kugawiwa kwa Omani kulikuwa mwanzo wa Zanzibar
Baada ya kifo cha Sayyid Sultan mwaka 1856, usultani wa Oman uligawiwa kati ya wanawe. Sayyid Majid bin Said Al-Busaid (1834/1835–1870) akawa Sultani wa kwanza wa Zanzibar na kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said akawa Sultani wa Oman akitawala nchi hiyo bila maeneo ya Afrika ya Mashariki.
Usultani mpya ulikuwa nchi yenye nguvu kati ya Rasi Delgado (mpakani na koloni la Kireno ya Msumbiji) hadi Mogadishu (Somalia). Athira yake ilienea kupitia njia za misafara ya pembe za ndovu na watumwa hadi mto Kongo.
Wafanyabiashara kama Tippu Tip waliokuwa raia wa Usultani wakapita Tabora na Ujiji kwenda ziwa Tanganyika na kuingia ndani ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo. Wapagazi wao walibeba bidhaa kutoka Zanzibar zilizobadilishwa kwa pembe za ndovu hasa. Watumwa walikamatwa au kununuliwa wakabeba pembe hadi pwani.
Sayyid Bargash
Sultani wa pili wa Zanzibar yenyewe, Sayyid Bargash, alijitahidi kujenga uhusiano na nchi za nje. Alifunga soko la watumwa Zanzibar mjini kulingana na mapatano ya kimataifa, lakini akavumilia biashara ya watumwa kuendelea chinichini. Wakati wa Bargash majengo mengi ya Mji Mkongwe yakajengwa.
Mwishowe mwa utawala wake aliona kupungukiwa kwa eneo lake kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ya kuenea katika Afrika baada ya mkutano wa Berlin.
Mwaka 1885 Karl Peters alifanya mikataba ya ulinzi na watawala wadogo waliokuwa chini ya Sultani barani Tanganyika. Upingamizi wa Sultani ulishindikana kwa sababu Wajerumani walituma manowari Unguja akapaswa kukubali maeneo mapya ya Wajerumani.
Kuenea kwa ukoloni
Mwaka 1886 mkataba kati ya Uingereza na Ujerumani ulibana eneo la sultani barani katika kanda yenye upana wa maili kumi tu kati ya Rasi Delgado na Mogadishu. Bargash na mfuasi wake Khalifa bin Said waliamua kuuza maeneo hayo au kuyakodisha.
- 1887/1888 pwani ya Kenya ilikodishwa kwa Waingereza. Wakati wa uhuru wa Kenya sehemu hii ikaingizwa katika Jamhuri ya Kenya.
- Pwani ya Tanganyika ikakodishwa kwa Wajerumani mwaka 1888 na hatimaye kuuzwa mwaka 1890.
- Miji kwenye pwani ya Somalia ikakodishwa kwa Italia mwaka 1892 ikauzwa mwaka 1906, ila Mogadishu mwaka 1924.
Hali halisi usultani ukabaki na visiwa viwili vya Unguja na Pemba tu.
Waingereza walikuwa walisita kuhusu Zanzibar lakini baada ya jaribio la Karl Peters la kufanya mkataba na Sultani ili kuingiza visiwa hivyo katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, Uingereza uliamua kutafuta utawala wa visiwa.
Mkataba wa Zanzibar-Heligoland na mwisho wa uhuru
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland kati ya Ujerumani na Uingereza ulileta patano la kuwa Zanzibar itakuwa chini ya Uingereza.
Tangu mwaka 1890 waziri mkuu wa Sultani alikuwa Mwingereza aliyepokea amri kutoka London.
Tangu mwaka 1913 nafasi ilichukuliwa na afisa mkazi mkuu.
Kwa muda wa miaka 26 usultani ulikuwa na fedha yake ya pekee iliyoitwa Riali ya Zanzibar.
Koloni la Kijerumani
Tazama makala kuu: Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na Vita Kuu ya Kwanza katika Afrika ya Mashariki
Maeneo yaliyoitwa baadaye (1920) "Tanganyika" na baadaye tena Tanzania Bara yaliunganishwa mara ya kwanza tangu mwaka 1886 kama koloni la Ujerumani lililoitwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Tangu mwaka 1885 Karl Peters, kwa niaba ya Shirika la Ukoloni wa Kijerumani (Gesellschaft für Deutsche Kolonisation) alianza kufanya mikataba na watawala wenyeji katika maeneo ya Usagara, Nguru, "Useguha" (yaani Uzigua) na Ukami iliyoweka msingi wa madai yake ya kuchukua utawala mkuu wa maeneo hayo.
Uenezeaji wa Wajerumani uliendelea hasa baada ya kushinda upinzani katika vita ya Abushiri na vita dhidi ya Wahehe.
Koloni lile la Kijerumani lilikuwa kubwa kuliko Tanganyika ya baadaye, maana ilijumlisha pia maeneo ya Rwanda na Burundi pamoja na sehemu ndogo ya Msumbiji.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 - 1918) koloni hilo la Kijerumani lilitekwa na majeshi ya Uingereza na Ubelgiji.
Mkataba wa Versailles wa mwaka 1919 ulikuwa na kanuni za kuchukua makoloni yote ya Ujerumani na kuzikabidhi kwa mataifa washindi wa vita. Sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani iliwekwa chini ya utawala wa Uingereza, kasoro maeneo ya Rwanda na Burundi yaliyokabidhiwa mikononi mwa Ubelgiji.
Tanganyika Territory ya Kiingereza baada ya kuondoka kwa Wajerumani
Utawala wa Wajerumani ulikoma katika eneo la Tanzania Bara baada ya Ujerumani kushindwa katika vita vikuu vya kwanza vya dunia vilivyodumu kutoka mwaka 1914 hadi mwaka 1918.
Mwaka 1919 sehemu kubwa ya koloni la Kijerumani, ikiwa na wakazi 3,500,000 hivi, ilikabidhiwa rasmi mikononi mwa Uingereza kama eneo lindwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa kulingana na kifungo 22 cha mkataba wa Versailles.
Mwaka 1922 Shirikisho la Mataifa lilithibitisha hatua hiyo na kuamua masharti ya kukabidhi.
Waingereza walihitaji jina jipya kwa ajili ya koloni hilo na tangu Januari 1920 wakaamua kuliita "Tanganyika Territory" kwa kutumia jina la ziwa kubwa upande wa mashariki ya eneo. [1]
Uhuru na Muungano
Tanganyika ilipata uhuru wake tarehe 9 Desemba 1961.
Zanzibar ilipata uhuru wake tarehe 10 Desemba 1963. Uhuru wa usultani ukadumu muda mdogo tu. Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 yakamuondoa Sultani. Mauaji ya familia nyingi zenye asili ya Kiarabu yakafuata.
Tarehe 26 Aprili 1964 Tanganyika na Zanzibar ziliungana kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hapo kiongozi wa Tanganyika Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kuwa Rais wa kwanza (1964-1985) na kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar Abedi Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Tanzania, chini ya Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania na kuanza mpango wa kurekebisha uchumi kuendana na masharti ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa (1995-2005) aliendeleza mfumo wa uchumi wa soko huria ambapo mashirika ya umma yanabinafsishwa.
Tarehe 21 Desemba 2005 Jakaya Kikwete aliapishwa kuwa Rais wa nne wa taifa (2005-2015), naye aliendeleza sera za watangulizi wake akitokea chama hichohicho cha CCM.
Aliyemfuata mwaka 2015 ni rais wa tano John Pombe Magufuli (CCM) kuanzia 2015-2020 halafu 2020-2021 kilipotokea kifo chake 17 Machi kwa tatizo la moyo. Nafasi yake akaendelea nayo makamu wa rais Samia Suluhu Hassan tangu Machi, 2021 hadi sasa.
Tanbihi
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Tanzania kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |