Historia ya Burundi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Burundi inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Burundi.

Historia ya awali[hariri | hariri chanzo]

Wakazi wa kwanza huaminiwa kuwa wawindaji wa jamii ya Wasani na ya Wabilikimo.

Katika karne za BK walifika wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi.

Ufalme wa Burundi[hariri | hariri chanzo]

Dola la kwanza katika eneo hili lilikuwa Ufalme wa Burundi. Katika mapokeo ya wenyeji ulianzishwa katika karne ya 17 na mtu kwa jina la Cambarantama aliyefika ama kutoka Rwanda ama kutoka Buha katika Mkoa wa Kigoma, Tanzania ya leo.

Ufalme huo ulitawaliwa na kundi la Watutsi waliokuwa wafugaji wa ng'ombe na kutawala wenyeji waliokuwa wakulima Wabantu. Watutsi walikuwa tabaka la kikabaila. Mfalme au mwami alikuwa mkuu wa makabaila hao ambao walitazamiwa kama mabwana wa ardhi iliyolimwa na watu wa kawaida. Hao wakulima waliruhusiwa kulima nchi wakipaswa kutoa huduma na sehemu ya mavuno kwa mabwana waliopaswa kuwatetea dhidi ya maadui.

Ufalme huo ulienea katika karne zilizofuata. Mwami Ntare IV Rutaganzwa Rugamba aliyetawala tangu mwaka 1796 hadi 1850 aliweza kupanua mipaka ya ufalme wake hadi kushika sehemu kubwa ya eneo la leo.

Ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Wazungu wa kwanza waliofika walikuwa wapelelezi Waingereza Richard Burton na John Hanning Speke mnamo mwaka 1854. Lakini habari za falme kwenye eneo kati ya maziwa makubwa hazikuenea sana. Wakati wa Mkutano wa Berlin 1885 Wajerumani hawakujua ya kwamba falme za Burundi na Rwanda zilikuwepo ndni ya eneo waliotegemea kutwaa. Waliitambua baadaye tu.

Mwaka 1894 Mjerumani wa kwanza alipita Burundi aliyekuwa Oskar Baumann. Wakati ule Ujerumani uliwahi tayari kuanzisha koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani lakini Wajerumani walichelewa kufika kaskazini-magharibi mwa maeneo waliyotazama kuwa sehemu yao.

Katika Burundi kikosi cha kwanza cha Kijerumani kilifika mnamo 1896 wakakuta ufalme wa mwami wakaridhika kumwacha mwakilishi mkazi (resident) katika mji mkuu Gitega ambaye hakuhusika na mambo ya utawala wa ndani. Wakati ule eneo lilijulikana kwa jina "Urundi". Hapa sawa na Rwanda na Bukoba Wajerumani walitumia mbinu ya eneo lindwa ingawa walikuwa pia na majadiliano kuingiza falme hizi za kienyeji moja kwa moja ndani ya koloni lao.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Burundi pamoja na Rwanda ilikabidhiwa kwa Ubelgiji kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa kama [[eneo la kudhaminiwa] lililoitwa Ruanda-Urundi. Kimsingi Wabelgiji waliendelea na mfumo wa Wajerumani uliomwachia mtemi mamlaka kubwa. Waliweka Ruanda-Urundi chini ya serikali ya Kongo ya Kibelgiji.

Lakini baadaye walianza kuingilia zaidi na ilhali wakati ule walipendelea Watutsi karibu na machifu wote walikuwa Watutsi na Wahutu walipotea katika nafasi za uongozi kimahali.

Tangu 1946 Shirikisho la Mataifa lilikwisha na Ubelgiji ilipokea wito wa kutawala Ruanda-Urundi na Umoja wa Mataifa.

Hali ya nchi kijamii na kisiasa[hariri | hariri chanzo]

Burundi ilundwa kama ufalme ulioongozwa na Watutsi waliotawala Wahutu. Lakini kabla ya ukoloni mipaka kati ya makundi hayo haikuwa imara mno; Wahutu matajiri katika utumishi wa mwami waliweza kupanda ngazi na kuwa Watutsi na pia Watutsi maskini waliweza kushuka ngazi na kuhesabiwa kati ya Wahutu, hasa baada ya kuoa au kuolewa na mtu wa upande mwingine. Uhusiano wa makundi hayo ulifanana zaidi na ule wa matabaka si wa makabila tofauti, pia kwa sababu lugha ilikuwa moja kwa wote.

Utawala wa kikoloni uliimarisha mipaka kati ya makundi hayo mawili maana kila mtu aliandikishwa na kupangwa katika moja kati ya makundi hayo. Pia Wabelgiji walipendelea Watutsi na kuangalia wapate nafasi zote za uchifu ambako walipaswa kutoa kibali. Kuhamia katika kundi lingine kulikwisha. Uhusiano kati ya makundi ulianza kufanana zaidi na ukabila.

Mwishoni mwa ukoloni Wabelgiji walibadilisha msimamo na kupendelea Wahutu.

Katika hali hiyo Burundi ilikaribia uhuru. Vyama vya siasa viliundwa vilivyofuata ugawaji wa kimbari kati ya Watutsi na Wahutu. Mapigano ya kwanza kati ya Wahutu na Watutsi yalitokea mwaka 1959 kabla ya uhuru yakakomeshwa na Wabelgiji.

Uhuru[hariri | hariri chanzo]

Mwaka moja kabla ya uhuru kulikuwa na uchaguzi wa kwanza chini ya usimamizi ya UM na chama mshindi kilikuwa UPRONA kilichoongozwa na mwanamfalme Mtutsi Louis Rwagasore aliyemwoa mwanamke wa Kihutu na chama kiliunganisha pande zote mbili. Lakini miezi michache baadaye Rwagasore aliuawa na chama chake kilitengana kufuatana na ukabila.

Mwaka 1962 Umoja wa Mataifa uliamua kuipa Ruanda-Urundi uhuru kamili, lakini kila nchi pekee.

Baada ya uhuru katika Burundi, kinyume na Rwanda, utawala ulibaki upande wa Watutsi kwa sababu jeshi lilikuwa mikononi mwao. Vipindi vya mashambulio kati ya vikundi vilifuata.

Baada ya uchaguzi wa 1965 mapigano yalitokea kwa silaha, na kikundi cha Watutsi wakali kilichukua serikali.

Mwaka 1966 mwami alipinduliwa na mwanasiasa Michel Micombero aliyejitangaza kuwa rais na nchi kuwa jamhuri. Kuanzia hapo wanasiasa na watumishi wakubwa walio Wahutu walifukuzwa, kukamatwa au kuuawa.

Mwaka 1972 malaki ya Wahutu waliuawa na jeshi la Kitutsi waliolenga hasa Wahutu wenye elimu.

Mwaka 1993 uongozi wa Kitutsi ulikubali tena uchaguzi huru ambako Mhutu Melchior Ndadaye alichaguliwa kuwa rais. Alipouawa na wanajeshi Watutsi malaki ya Watutsi waliuawa na Wahutu wakali.

Kipindi kilichofuata kilikuwa cha Vita ya wenyewe kwa wenyewe katika sehemu mbalimbali za nchi.

Uwanja wa Ndege, Bujumbura

Tangu mwaka 1995 Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa zilijitahidi kujenga mapatano kati ya vikundi. Marais na wanasiasa walioshiriki katika jitihada hizo walikuwa pamoja na Julius Nyerere, Boutros Boutros-Ghali, Nelson Mandela, Thabo Mbeki na rais wa Marekani Bill Clinton.

Mapatano yalifikiwa na kusainiwa mwaka 2000 na washiriki karibu wote huko Arusha. Majadiliano yaliendelea hadi mwaka 2003 hatimaye vita ilisimamishwa. Mapatano yaliyofikiwa yanasema ya kwamba Watutsi pamoja na Watwa, ambao ni asilimia 15 za wananchi, watakuwa na asilimia 40 ya nafasi kwenye bunge na ya kwamba jeshini kila upande utashika asilimia 50 za nafasi. Pia kwenye senati ya bunge kila upande utakuwa na asilimia 50. [1]

Rais atachaguliwa na wananchi wote lakini mapatano yalisema rais wa kwanza atachaguliwa na bunge.

Hali ya siasa[hariri | hariri chanzo]

Rais Nkurunziza mwaka 2006

Mwaka 2005 uchaguzi wa kwanza wa bunge baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ulifanyika. Chama cha CNDD-FDD kilipata kura nyingi na kiongozi chake Pierre Nkurunziza alichaguliwa na bunge kuwa rais wa taifa. Vyama vya UPRONA na FRODEBU vilivyotangulia kuongoza serikali ya mpito vilipata kura chache kwa sababu vilishtakiwa kuwa na rushwa na upendeleo wa kindugu.

Chama tawala kinajaribu kufuata siasa ya mapatano ya ndani, lakini ina uvumilivu mdogo tu kwa upinzani na mawazo yanayopinga siasa yake.

Mwezi wa Aprili 2009 chama cha Palipehutu FNL hatimaye kilisimamisha upinzani kwa silaha kikakubaliwa kama chama cha kisiasa cha FNL.

Nkurunziza alichaguliwa tena kwa kura ya wananchi wote mwaka 2010. Chama cha upinzani FNL kilikataa kukubali ushindi wa CNDD-FDD.

Mwaka 2015 rais Nkurunziza alipendekezwa kugombea tena urais katika uchaguzi akakubali. Hatua hiyo ilisababisha upinzani mkali wa wananchi walioandamana wakiona hii inavunja mapatano ya amani ya Arusha.

Tarehe 13 Mei jenerali Godefroid Niyombare alitangaza kufukuzwa kwa Nkurunziza kutoka urais wakati huyo alikuwa safarini Tanzania, lakini hakufaulu. Uasi huu wa kijeshi ulikandamizwa. Nkurunziza alirudi na kutangaza ya kwamba kura inatakiwa kufanyika jinsi ilivyopangwa tarehe 26 Mei 2015 kwa bunge na 26 Juni kwa uraisi.

Taasisi ya kimataifa na nchi jirani walitamka wasiwasi kuhusu mwelekeo wa hali ya kisiasa katika Burundi. Nkosazana Dlamini-Zuma, mwenyekiti wa kamati tendaji ya Umoja wa Afrika, aliomba kuahirishwa kwa kura nchini Burundi hadi hali iwe imetulia.

Tarehe 24 Julai 2015 Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Nkurunziza mshindi wa uchaguzi kwa 69.41% za kura. Agathon Rwasa alishika nafasi ya pili kwa 18.99% ingawa alikuwa amehimiza wananchi wasipige kura.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Burundi kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Mapatano ya Arusha ya 2000 kuhusua mani na upatanisho kwa ajili ya Burundi, uk. Protocoll II, I, 11, 4a, Appendix I,I B 2-4. Jalada kutoka ya awali juu ya 2008-02-25. Iliwekwa mnamo 2015-09-26.