Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Mali

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Mali inahusu eneo la Afrika Magharibi ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Mali.

Historia ya kale

[hariri | hariri chanzo]

Mali ina historia ndefu ambayo ni historia ya pamoja ya nchi za kanda la Sahel na kanda la Sudan.

Zamani za Wafinisia na za Waroma palikuwa na mawasiliano ya biashara na nchi za Mediteranea kupitia wanafayabiashara Waberberi walioelewa njia za Sahara.

Uvamizi wa Wavandali katika Afrika ya Kaskazini ulivuruga mawasiliano hayo.

Dola la Ghana

Baada ya uvamizi wa Waarabu na uenezaji wa Uislamu biashara ilianza upya. Ndio Waberberi Waislamu walioingiza dini mpya hata kusini ya Sahara.

Katika eneo la Mali ya leo pamoja na nchi jirani ni hasa madola matatu makubwa yaliyotawala upande wa kusini wa njia za biashara iliyovuka Sahara.

Dola la Ghana

[hariri | hariri chanzo]

Dola la kwanza lilikuwa Dola la Ghana. Kuanzia karne ya 8 BK hadi mwaka 1076 lilitawala biashara ya dhahabu, pembe za ndovu na chumvi. Mji mkuu ulikuwa Kumbi Sale wenye wakazi 30,000 katika Mauretania ya leo.

Taarifa za wanahistoria Waarabu zimeonyesha ufalme tajiri. Utamaduni wake haukuwa wa Kiislamu bali wa Kiafrika asilia.

Mwisho wake ulianza wakati jeshi la Wamurabitun kutoka Moroko lilivuka jangwa na kuvamia Kumbi Sale.

Dola la Mali

[hariri | hariri chanzo]
Eneo la Dola la Mali

Mali ilianza kama ufalme mdogo wa Wamalinke kando ya Ghana. Wakati wa karne ya 13 ilianza kupanuka chini ya mfalme Sundiata Keita. Sundiata mwenyewe alipokea Uislamu mnamo 1240 BK na wafalme baada yake waliendela kuwa Waislamu.

Mfalme wa Mali aliyejulikana zaidi ndiye Mansa Kankan Musa I (13121337). Miaka 1324-1325 alihiji kwenda Makka. Alisafiri na dhahabu nyingi sana. Huku Misri alitoa zawadi kiasi cha kuharibu thamani ya dhahabu kwa miaka 12 iliyofuata.

Wakati ule mji wa Timbuktu ulikuwa kitovu cha biashara na elimu iliyojulikana kote katika umma wa Kiislamu hata Ulaya.

Katika karne ya 14 BK uwezo na utawala wa Mali ulipungua na Songhai ilichukua nafasi yake.

Dola la Songhai

[hariri | hariri chanzo]
Eneo la Dola la Songhai

Asili ya Wasonghai ilikuwa Nigeria ya Kaskazini ya leo. Walipanua utawala wao kuelekea magharibi wakapokea Uislamu wakati wa uvamizi wa Almurabitun.

Mnamo mwaka 1250 walikuwa chini ya Mali lakini katika karne ya 14 walijipatia uhuru tena, wakaanza kushika maeneo ya Mali yenyewe.

Kilele cha nguvu yake ilikuwa wakati wa mfalme Askia Mohammad I katika karne ya 16 walipotawala eneo kubwa kutoka Kano (Nigeria) hadi pwani ya Atlantiki. Wakati wake mji wa Timbuktu ilitembelewa na msafiri Leo Africanus aliyeleta baadaye habari za nchi hadi Ulaya.

Utawala wao uliporomoka baada ya mashumbulizi kutoka Moroko mwaka 1591. Wakati ule mataifa ya Ulaya yameshaanza kufika kwenye mwambao wa Afrika ya Magharibi wakifungua biashara ya moja kwa moja na Ulaya. Umuhimu wa biashara ya kuvuka Sahara ulipungua vikali pamoja na faida iliyopatikana kwa watawala katika maeneo ya Sahel.

Kipindi cha madola madogo na jihadi

[hariri | hariri chanzo]

Kilichofuata kilikuwa kipindi cha madola madogo. Viongozi Waislamu walijaribu mara kadhaa kujenga utawala juu ya eneo lote.

Anayejulikana zaidi alikuwa Alhaj Omar aliyepiga vita kwa jina la dini ya Kiislamu dhidi ya Wabambara waliofuata utamaduni na dini asilia za Kiafrika.

Mtoto wa Alhaj Omar aliyeitwa Ahmadu alijaribu kuendeleza jihadi yake. Lakini wakati ule Wafaransa walianza kuenea katika Afrika ya Magharibi wakamshinda.

Mali ikawa koloni la Ufaransa kuanzia mwaka 1895. Ilikuwa sehemu ya Afrika ya Magharibi ya Kifaransa, na kuanzia 1920 ya Sudan ya Kifaransa.

Mji wa Bamako

Mwaka 1960 Mali pamoja na Senegal zilipata uhuru kama "Shirikisho la Mali". Baada ya Senegal kuacha umoja huo, Jamhuri ya Mali chini ya rais wa kwanza Modibo Keïta ikawa nchi ya kujitegemea.

Keita alipinduliwa mwaka 1968 na wanajeshi akishtakiwa kuwa ameharibu uchumi na kujitajirisha. Kiongozi mpya Moussa Traoré alitawala kama dikteta wa kijeshi, baadaye kwa msaada wa katiba ya chama kimoja.

Mabadiliko yaliyotokea kote Afrika tangu mwisho wa Ukomunisti kuanzia miaka ya 1990 yalisababisha kupinduliwa kwa Traoré katika Machi 1991 na kamati ya kijeshi iliyoongozwa na Amadou Toumani Touré.

Katiba mpya ya mwaka 1992 iliunda kipindi cha kura huru alimoshinda Amadou.

Mnamo Septemba 2021, mkataba ulisainiwa kati ya serikali ya Mali na kampuni binafsi ya jeshi la Urusi iliyounganishwa na kikundi cha jeshi la Urusi Wagner. Hati hiyo inataka kupelekwa kwa mamluki nchini, kwa kushirikiana na jeshi la Mali, na ulinzi wa wahusika wakuu.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe katika kaskazini na maasi ya kijeshi

[hariri | hariri chanzo]

Kaskazini mwa Mali kunakaliwa hasa na Watuareg na sehemu yao hawakupenda kuwa chini ya Mali. Hivyo kulikuwa mara kadhaa na mapigano kati ya Watuareg na jeshi la Mali. Tangu mwaka 2012 mapigano yameanza upya[1]. Mwaka ule wanamgambo na wanajeshi walikimbia vita kwenda Libya na kujiunga na wapiganaji Watuareg waliotangaza mnamo Aprili 2012 uhuru wa eneo la "Azawad" katika mikoa ya Timbuktu, Gao na Kidal. Lakini wanamgambo wa makundi yenye mwelekeo mkali wa Kiislamu kama Al-Qaeda waliwashinda Watuareg wenyewe na kushika utawala wakianzisha mfumo wa sharia ya Kiislamu[2].

Serikali ya Mali iliomba usaidizi wa kijeshi wa Ufaransa uliokubaliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa azimio na. 2085 ya tarehe 20 Desemba 2012. Jeshi la Kifaransa lilifaulu kuwaondoa wanamgambo Waislamu katika miji yote[3] lakini hao waliendelea kujificha kwenye milima.

Baada ya mwisho wa kampeni ya Wafaransa nafasi yao ilichukuliwa na jeshi la Umoja wa Mataifa lililoingia kwa jina la "MINUSMA"[4] lililokuwa na wanajeshi kutoka nchi 60. 19 kati ya nchi hizo ni za Kiafrika ambazo walileta idadi kubwa ya askari.

Mapigano yameendelea. Wananchi wengi vijijini walichukua silaha na kuunda vikundi vya wanamgambo kwa kujihami lakini vikundi hivyo vinashambuliana pia.[5]

Miaka 2020 na 2021 jeshi la Mali liliasi mara mbili na kupindua serikali za kiraia[6][7]. Kanali Assimi Goïta alitangazwa kuwa rais mtendaji. ECOWAS na Umoja wa Afrika vilisimamisha uanachama wa Mali[8]. Ufaransa na nchi nyingine zilianza kuondoa wanajeshi katika ushirikiano na jeshi la kitaifa[9].

Mnamo Januari 2022 wanajeshi kutoka Urusi walianza kufika Mali kwa kibali cha serikali ya kijeshi[10].

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Mali kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Mali clashes force 120 000 from homes Archived 10 Oktoba 2017 at the Wayback Machine. News24 (22 February 2012). Retrieved 23 February 2012.
  2. Tiemoko Diallo. "Islamists declare full control of Mali's north", Reuters, 28 June 2012. 
  3. "French Troops Retake Kidal Airport, Move into City", USA Today, 30 January 2013.  French troops retake the last remaining Islamist urban stronghold in Mali.
  4. United Nations Multidimensional Integrated Stabilization Mission in Mali
  5. ""We Used to Be Brothers" | Self-Defense Group Abuses in Central Mali". Human Rights Watch (kwa Kiingereza). 7 Desemba 2018. Iliwekwa mnamo 30 Machi 2019.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  6. "Mali timeline: From military coup to interim leaders removed". www.aljazeera.com (kwa Kiingereza). 25 Mei 2021. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 25 Mei 2021. Iliwekwa mnamo 2021-05-28.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  7. "Mali President, PM Resign After Arrest, Confirming 2nd Coup in 9 Months". VOA News. 26 Mei 2021. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 29 Mei 2021. Iliwekwa mnamo 29 Mei 2021.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  8. "ECOWAS suspends Mali over second coup in nine months", May 31, 2021. Retrieved on June 2, 2021. 
  9. Ahmed, Baba; Larson, Krista (Juni 2, 2021). "French military suspends joint operation with Mali military". The Associated Press. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 4 Juni 2021. Iliwekwa mnamo 4 Juni 2021.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  10. "Russian military advisors arrive in Mali after French troop reduction". France 24 (kwa Kiingereza). 2022-01-07. Iliwekwa mnamo 2022-01-07.