Historia ya Benin

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Benin inahusu eneo la Afrika Magharibi ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Benin, lakini kabla ya mwaka 1975 lilijulikana kama Dahomey.

Historia ya awali[hariri | hariri chanzo]

Ufalme wa Dahomey[hariri | hariri chanzo]

Sherehe na ngoma kule Abomey, 1908.

Ufalme wa Dahomey ulianzishwa katika nchi ya kisasa ya Benin.

Katika karne ya 17, ufalme huo uliotawaliwa na oba (ni cheo cha mfalme wake) ulienea sehemu kubwa ya Afrika ya Magharibi.

Askari wa kike wa Mfalme wa Dahomey ("Waamazoni").

Dahomey ilianzishwa na Waaja baada ya uhamisho wao kutoka Togo kuja Benin ya leo. Jina la Dahomey linasemekana kuwa limetokana na neno la Kifon la "dan" lenye maana ya "nyoka" - dokezo la ibada ya nyoka kusini mwa nchi.

Jina la mfalme wa kwanza ni Do Aklin aliyekuwa mmoja wa wana watatu wa mfalme wa Ardra waliogawanya ufalme kati yao mnamo 1625 BK. Do Aklin aliunda mji wa Abomey ukawa mji mkuu wa Dahomey.

Waaja wa Abomey walichanganyikana na wenyeji wakawa kabila jipya la Wafon au Wadahomey. Waliratibu ufalme wao kwa kuupa serikali ya mfalme mwenye nguvu, wakaunda jeshi la kudumu.

Hasa mfalme Wegbadja aliweka utaratibu kwa vizazi vilivyofuata: mfalme alikuwa mtawala mkuu, mkoani au majimboni hapana watawala wa kieneo bali watumishi wake tu.

Ardhi yote ilitazamwa kuwa mali ya mfalme mwenyewe, mafundisho yaliyohakikisha malipo ya kodi kutoka kwa wakulima waliokubali ya kwamba nchi waliyoilima ni mali ya mfalme.

Mamlaka ya mfalme yalihakikisha nguvu ya Dahomey katika mazingira yake. Jeshi la kudumu lilimpatia chombo muhimu. Ndani ya jeshi hilo kulikuwa na kikosi kimoja cha pekee ambacho kilikuwa kikosi cha wanawake.

Wasafiri wa Ulaya walikiita kikosi hiki "Waamazoni" kutokana na askari wa kike katika masimulizi ya Wagiriki wa Kale.

Wegbadja na wafuasi wake walikaza pia umuhimu wa ibada za pamoja. Wafalme wenyewe na mizimu yao walipewa nafasi muhimu. Sadaka zilienda na kila nafasi, hasa sadaka kwa mizimu ya wafalme.

Dahomey na biashara ya watumwa[hariri | hariri chanzo]

Kulikuwa na utajiri mkubwa kwa sababu ya kufanya biashara na Wazungu, hasa Wareno na Waholanzi waliofika kuanzia mwisho wa karne ya 15.

Ufalme uliongezeka nguvu ya kiuchumi hasa kutokana na biashara ya watumwa. Kupaa kwa nguvu ya Dahomey kulikwenda sambamba na kuenea kwa wafanyabiashara Wazungu kwenye pwani za Afrika ya Magharibi walionunua watumwa kwa ajili ya safari ya Marekani, wakiuza silaha na bidhaa kutoka Ulaya.

Katika karne tatu za historia yake Dahomey ilikuwa kati ya wafanyabiashara wakuu wa watumwa. Pwani ya Benin ya leo ilijulikana kama Pwani ya Watumwa.

Jeshi la Dahomey lilikuwa na bunduki zilizonunuliwa kwa Wazungu wakiwauzia watumwa; silaha hizo zilitumika kwa ajili ya kupiga vita dhidi ya majirani na kujipatia wafungwa waliouzwa kama watumwa. Mapato kutoka biashara hiyo yaliwezesha wafalme wa Dahomey kununua silaha mpya.

Biashara ya watumwa iliendelea kwa karne tatu mpaka mwaka wa 1885.

Chini ya Wafaransa[hariri | hariri chanzo]

Kuanzia karne ya 18, ufalme wa Dahomey ulidhoofika mpaka Ufaransa uliweza kuuvamia mwaka wa 1892. Dahomey ikawa chini ya ukoloni wa Ufaransa kuanzia mwaka wa 1899 hadi ilipopata tena uhuru tarehe 1 Agosti 1960.

Baada ya uhuru[hariri | hariri chanzo]

Mpaka mwaka wa 1972 makundi mbalimbali walipigana vita, hatimaye Wakomunisti walianza kutawala chini ya kiongozi wao Mathieu Kérékou.

Hapo nchi ilipewa jina jipya, yaani Jamhuri ya Watu wa Benin, mwaka wa 1975 hadi 1991.

Tangu miaka ya 1980 nchi ilifuata mfumo wa soko huria. Kérékou alikuwa Rais hadi 1991, halafu tena miaka 1996-2006.

Katika uchaguzi wa Machi 2006, Yayi Boni alipata urais aliouanza tarehe 6 Aprili 2006.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Benin kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.