Historia ya Sudan Kusini
Historia ya Sudan Kusini inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Sudan Kusini.
Historia ya kale
[hariri | hariri chanzo]Kuna nyaraka chache sana za historia ya mikoa ya kusini mpaka mwanzo wa utawala wa Misri upande wa kaskazini mapema 1820 na baadaye kuendelezwa kwa biashara ya utumwa kuingia kusini.
Kabla ya wakati huo, habari zote zinapatikana kwa misingi ya historia simulizi. Kulingana na mila hizo, watu wa Niloti (Wadinka, Nuer, Shilluk) na wengine waliingia kusini mwa Sudan kwa mara ya kwanza wakati fulani kabla ya karne ya 10.
Katika kipindi cha kati ya karne ya 15 na karne ya 19, uhamiaji wa makabila, hasa kutoka eneo la Bahr al Ghazal, ulileta watu hawa katika maeneo yao ya sasa. Makabila yasiyo Niloti yaani Waazande, ambao waliingia Sudan Kusini katika karne ya 16, waliunda jimbo kubwa zaidi katika kanda hii.
Katika karne ya 18, watu wa Avungara waliingia na kwa haraka wakaweka mamlaka yao juu ya Waazande. Utawala wa Avungara ulikaa kwa muda bila kupingwa mpaka kuwasili kwa Waingereza mwishoni mwa karne ya 19. Vizuizi vya kijiografia viliwalinda watu wa kusini kutokana na kuenea kwa Uislamu, na kuwawezesha kurejesha turathi zao za kijamii na kitamaduni na urithi wao wa kisiasa na taasisi za kidini.
Misri, chini ya utawala wa Khedive Ismail Pasha, ilijaribu kwa mara ya kwanza kuikoloni kanda hiyo katika miaka ya 1870, na kuanzisha jimbo la Equatoria katika sehemu ya kusini. Gavana wa kwanza wa Misri alikuwa Samwel Baker, aliyeanza kuhudumu mwaka 1869, akifuatiwa na Charles George Gordon mwaka 1874 na Emin Pasha mnamo 1878.
Maasi ya Mahdist ya miaka ya 1880 yaliuyumbisha mkoa huu mchanga, na Equatoria ilikoma kuwepo kama milki ya Misri mwaka 1889. Makazi muhimu katika Equatoria yalikuwa pamoja na Lado, Gondokoro, Dufile na Wadelai.
Sudan Kusini ilitawaliwa kama eneo la pekee wakati wa ukoloni wa Kiingereza hadi 1947 ilipounganishwa na kaskazini kama nchi moja bila kuwauliza wenyeji.
Ndani ya Sudan huru
[hariri | hariri chanzo]Wakati wa uhuru wa Sudan mwaka 1956 viongozi wa kusini walidai haki ya kujitawala ndani ya taifa jipya, lakini mapatano yalishindikana na hali hiyo ilisababishwa kutokea kwa vita ya Anyanya kati ya 1956 na 1972.
Baada ya kipindi cha amani, vita vilianza upya mwaka 1983 wakati kanali John Garang alipounda SPLA dhidi ya badiliko la Sudan kutangazwa nchi ya Kiislamu.
Vita hivyo vya pili vilikwisha mwaka 2005 kwa mkataba wa amani ulioacha kusini kama sehemu ya kujitawala ndani ya Sudan hadi ipigwe kura juu ya swali la kujitenga iliyopangwa kwa mwaka 2011.
Nchi imeathiriwa vibaya na vita vya kwanza vya Anya-nya na vya pili Anya na pia Vita vya Pili vya Wenyewe kwa Wenyewe vya Sudan vya SPLA / M kwa karibu miaka 21 tangu historia ya mwanzo wa SPLA / M mwaka wa 1983 - na kupelekea kutelekezwa vibaya, ukosefu wa miundomsingi ya maendeleo, na uharibifu mkubwa na kuhama kutoka makazi yao.
Zaidi ya watu milioni 2.5 wameuawa, zaidi ya milioni 5 kuachwa bila makao na wengine kuwa wahamiaji wa ndani, na kuwa wakimbizi kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na sababu zingine zinazohusiana na vita.
Baada ya kifo cha John Garang, majeshi ya Southern Sudan Army na South Sudan Defense Force (SSDF) yalisitisha uhasama wao na kuungana mnamo Januari 2006, chini ya Azimio la Juba. SSDF ilianzishwa na Makamu wa Rais wa sasa wa Sudan Kusini, Dkt. Riek Machar.
Chini ya Azimio la Juba, Jenerali Matip akawa Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Sudan Kusini, na vikosi vyake vya SSDF kuingizwa katika Jeshi la Sudan Kusini, na kuongezea safu yake kutoka 50,000 hadi 309,000. Jumla ikawa askari 359,000. Wote sasa ni jeshi moja linalojulikana kama Jeshi la Sudan Kusini.
Jenerali Oyay Deng Ajak aliteuliwa kuwa Ofisa-mkuu-wa-Watumishi wa Jeshi la Sudan Kusini, hadi Mei 2009 wakati alipompisha Meja Jenerali James Hoth Mai[1].
Mbali na Katiba ya Mpito ya Jamhuri ya Sudan [2], Katiba ya Mpito ya Sudan Kusini ya 2005 iliwekwa kuwa sheria kuu [3] ya Sudan Kusini.
Katiba imeweka Tawi Kuu linaloongozwa na Rais ambaye ni Mkuu wa Nchi, Mkuu wa Serikali, na Kamanda Mkuu wa Sudan People's Liberation Army. John Garang, mwanzilishi wa SPLA / M alikuwa Rais wa kwanza hadi kifo chake tarehe 30 Julai 2005.
Salva Kiir Mayardit, naibu wake, aliapishwa kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan na Rais wa Serikali ya Sudan Kusini tarehe 11 Agosti 2005. Riek Machar aliingia mahala pake kama Makamu wa Rais.
Nguvu za kuunda sheria ziko mikononi mwa serikali na Bunge la pamoja la Sudan Kusini.
Katiba pia imeweka mahakama huru, chombo cha juu kabisa kikiwa Mahakama Kuu.
Uhuru
[hariri | hariri chanzo]Mnamo Januari 2011 wakazi wa Sudan Kusini walipiga kura juu ya swali la kujitenga na Sudan wakaamua karibu kwa kauli moja (98.83%) kuwa nchi huru.
Tofauti kubwa kati ya pande hizo ilikuwa kwamba katika Sudan yenyewe idadi kubwa ya watu wamekuwa Waislamu na utamaduni wao una mchaganyiko wa tabia za Kiarabu na Kiafrika pamoja na usambazaji mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Kumbe kusini kuna Waislamu wachache, wengi ni wafuasi wa dini za jadi au ni Wakristo. Kiuchumi na kielimu kusini wako nyuma sana kulingana na kaskazini.
Nchi ina muundo wa shirikisho.
Tangu upatikane uhuru, nchi imeendelea kuvurugwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na kwa sasa inashika nafasi ya kwanza katika orodha ya nchi dhaifu.
Hata hivyo mnamo Machi 2016 nchi imekubalika kama mwanachama wa sita wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Sudan Kusini kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |