Salva Kiir Mayardit

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Salva Kiir Mayardit, Rais ya Kwanza ya Sudan Kusini

Salva Kiir Mayardit (amezaliwa 13 Septemba 1951) ni Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini. Amekuwa Rais wa nchi hiyo tangu mwaka 2011, wakati Sudan Kusini ilipopata uhuru kutoka Sudan. Kwa hiyo, yeye ni rais ya kwanza wa nchi. Kabla ya uhuru, Kiir alikuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa nchi ya Sudan na Rais wa eneo la Kusini la Sudan.

Maisha ya zamani[hariri | hariri chanzo]

Maisha binafsi[hariri | hariri chanzo]

Kiir alizaliwa siku ya 13, mwezi wa 9, mwaka 1951 katika mji wa Gogrial, nchi ya Sudan. Kiir ni mwanachama wa kabila la Wadinka.[1]

Baba yake Kiir alikuwa mchungaji wa ng’ombe na mama alikuwa mkulima.[1] Kiir alikuwa mmoja wa watoto tisa. Sasa, ana wake wawili na watoto wawili, wote wasichana. Majina ya wake hao ni Mary Ayen Mayardit na Aluel William Nyuon Bany.[1]

Kazi kabla ya urais[hariri | hariri chanzo]

Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, Kiir ametegemeza harakati ya uhuru kwa Sudan Kusini. Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kwanza, Kiir alipigana na kikundi cha Anyanya[1], ambacho kilitaka uhuru kwa Sudan Kusini. Halafu, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya pili, Kiir alipigana na Sudan People's Liberation Army (SPLA), na hatimaye, alikuwa kiongozi wa jeshi hilo.[1]

Rais Kiir amevaa nguo za kijeshi kama mwanachama wa SPLA

Baada ya kifo cha Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang, mwaka 2005, Kiir alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Sudan na Rais ya Sudan Kusini.[2]

Katika uchaguzi wa 2010 wa Sudan, Kiir alishinda tena. Alipata asilimia 93 ya kura, na nchi nyingi za kidemokrasia zilishutumu uchaguzi huu.[3] Hata hivyo, ushindi mkubwa wa Kiir ulikuwa muhimu sana kwa uhuru wa Sudan Kusini mwaka 2011.

Uchaguzi[hariri | hariri chanzo]

Katika mwezi wa kwanza, mwaka 2011, watu wa Sudan Kusini walipiga kura kujitenga kutoka Sudan kwa sababu ya migogoro kati ya kaskazini na kusini ya Sudan. Watu wengi wa Sudan Kusini ni Wakristo, na watu katika kaskazini na serikali ya Sudan ni Waislamu, kwa hiyo watu wa kusini walihisi wanakandamizwa.[4] Mwaka 2011, asilimia 99 ya watu wa Sudan Kusini walitaka kuondoka.[5] Wakati Sudan Kusini ilipata uhuru kutoka kaskazini, Kiir alikuwa Rais ya Kwanza ya Jamhuri ya Sudan Kusini, kwani alishinda uchaguzi mwaka uliopita.

Urais[hariri | hariri chanzo]

Sera ya Ndani[hariri | hariri chanzo]

Chama cha Kiir ni Sudan People's Liberation Movement (SPLM). Kiir alianza urais wake kwa kusamehe watu ambao walipinga SPLM.[1] Hata hivyo, Rais Kiir aliwafukuza baraza lake la mawaziri, ikiwamo Makamu wa Rais wake, Riek Machar. Pia, alifukuza majenerali wa jeshi 117. Watu wengi, ikiwamo Machar, wanasema kwamba hii ni jaribio la Kiir kuwa na nguvu zaidi.[1]

Kiir amekataliwa kwa kuwatishia waandishi wa habari ambao waliandika vitu vibaya kuhusu yeye. Mwaka 2015, Kiir alisema kwamba waandishi wa habari hawapaswi kufanya kazi dhidi ya nchi wake, na kwamba ataonyesha kwamba nchi yake inaweza kuua watu.[6] Mwaka huo, waandishi wa habari sita waliuawa.[6]

Pia, Kiir ana msimamo dhidi ya ushoga. Alisema kwamba ushoga ni “ugonjwa wa ubongo” na kama nchi za Magharibi zikijaribu kuleta ushoga mpaka Sudan Kusini, watu hawatakubali.[1]

Mapigano na Riek Machar[hariri | hariri chanzo]

Riek Machar, Makamu wa zamani wa Rais wa Sudan Kusini

Tangu mwaka 2013, kumekuwa na migogoro ya kisiasa katika Sudan Kusini kati ya Kiir na upinzani wake. Baada ya Kiir kumfukuza Makamu wa Rais wake, Riek Machar, Machar alianza kusema dhidi ya serikali ya Kiir. Mwezi wa 12, mwaka 2013, baada ya mkutano kati ya Kiir na Machar, kulikuwa na risasi nyumbani kwa Rais Kiir. Kiir alisema kwamba hii ilikuwa jaribio la Machar kupindua serikali ya Kiir.[7] Ingawa Machar alikanusha hili, tukio hili limeanza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini.[1] Machar alisema kwamba alipanga kushinda uchaguzi wa 2015.[7] Leo, Kiir na Machar bado wanapigana kwa nguvu. Pia, mapigano kati ya Kiir na Machar ni matokeo ya tofauti ya makabila.[8]

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Kiir kusema kwamba Machar alijaribu kumpindua, mapigano kati ya chama cha Kiir, SPLM, na upinzani wake, SPLM-IO, yalianza.[9] Upinzani wa Kiir unaongozwa na Machar. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan Kusini ni migogoro ya kikabila na kisiasa. Imekadiriwa kwamba zaidi ya watu 300,000 wamekufa kutokana na vita hivyo.[10] Pia, vita vimesababisha wakimbizi milioni nne.[10] Rais Kiir amepata upinzani kutoka jumuiya ya kimataifa kwa sababu ya vita.[11]

Sera ya nje[hariri | hariri chanzo]

Uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 2011, Rais Kiir alijaribu kufanya Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa sababu nchi za EAC zilitegemeza Sudan Kusini katika harakati yake ya uhuru.[1] Sudan Kusini ilikubaliwa ndani ya EAC mwaka 2016.[12]

Mgogoro wa Heglig wa 2012[hariri | hariri chanzo]

Ingawa Sudan Kusini alipata uhuru kwa Sudan, bado kuna mgogoro kati ya nchi hizo mbili. Mwaka 2012, jeshi la Sudan Kusini lilishambulia shamba la mafuta la Heglig, kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.[13] Mafuta yamekuwa tatizo linaloendelea kabla na baada ya uhuru wa Sudan Kusini, kwa sababu ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi zote mbili. Mwezi wa tisa, mwaka 2012, Rais Kiir alikutana na Rais al-Bashir wa Sudan huko Addis Ababa kwa ajili ya kushara makubaliano kuhusu shamba la mafuta hili.[1] Hata hivyo, bado kumekuwa na mgogoro na Kiir alilalamika kwa Umoja wa Mataifa mwaka 2012.[1]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. 1.00 1.01 1.02 1.03 1.04 1.05 1.06 1.07 1.08 1.09 1.10 1.11 "Salva Kiir Mayardit", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2019-04-12, iliwekwa mnamo 2019-04-15 
 2. "Salva Kiir Mayardit | president of South Sudan". Encyclopedia Britannica (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2019-04-15. 
 3. "Salva Kiir Mayardit | president of South Sudan". Encyclopedia Britannica (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2019-04-15. 
 4. "Second Sudanese Civil War", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2019-04-14, iliwekwa mnamo 2019-04-15 
 5. Gettleman, Jeffrey (2011-07-09), "After Years of Struggle, South Sudan Becomes a New Nation", The New York Times (kwa en-US), ISSN 0362-4331, iliwekwa mnamo 2019-04-15 
 6. 6.0 6.1 Committee to Protect Journalists 330 7th Avenue, 11th Floor New York, Ny 10001. "South Sudanese President Salva Kiir threatens to kill journalists". cpj.org (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2019-04-15. 
 7. 7.0 7.1 Kushkush, Isma’il (2013-12-16), "President Says a Coup Failed in South Sudan", The New York Times (kwa en-US), ISSN 0362-4331, iliwekwa mnamo 2019-04-15 
 8. "What Triggered the Kiir-Machar Rift in South Sudan?". VOA (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2019-04-15. 
 9. "South Sudanese Civil War", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2019-04-10, iliwekwa mnamo 2019-04-15 
 10. 10.0 10.1 [1]A new report estimates that more than 380,000 people have died in South Sudan’s civil war. Washington Post. 26 September 2018.
 11. [2]South Sudan is a disaster. Its president says: Not my fault. Washington Post. 15 October 2017.
 12. AfricaNews (2016-04-15CEST13:15:31+02:00). "South Sudan officially joins East African Community". Africanews (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2019-04-15.  Check date values in: |date= (help)
 13. "Heglig Crisis", Wikipedia (kwa Kiingereza), 2019-04-11, iliwekwa mnamo 2019-04-15 
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Salva Kiir Mayardit kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.