Nenda kwa yaliyomo

Mapenzi ya jinsia moja

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ushoga)
Bendera ya fahari, bendera inayowakilisha watu wa LGBT, wakiwemo wapenzi wa jinsia moja.
Utafiti wa mwaka 2019 (Pew Global Research Poll): Asilimia ya wakazi wanaokubali mapenzi wa jinsia moja yawe halali katika jamii:      0-10%      11-20%      21-30%      31-40%      51-60%      61-70%      71-80%      81-90%      91-100%      Hakuna taarifa

Mapenzi ya jinsia moja (kwa Kiingereza: homosexuality) ni mwelekeo wa kijinsia ambapo mtu anahisi kuvutiwa kimapenzi na kihisia na mtu wa jinsia yake mwenyewe.[1]Hii ni hali inayojitokeza katika jamii nyingi, na inaeleweka tofauti kulingana na utamaduni na muktadha wa kila sehemu. Kwa kuwa mtazamo wa jamii kuhusu hili hutofautiana sana, mwaka kwa mwaka nchi nyingine zinazidi kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja na nyingine zinazidi kutunga sheria dhidi yake.

Hata hivyo kuna wanawake wanaovutiwa na wanawake wenzao na wanamume wanaovutiwa na wanaume wenzao, mbali ya watu wanaovutiwa na jinsia zote mbili (kwa Kiingereza: “bisexual”), mbali na wale wasio na mwelekeo wowote wala kusikia mvuto wowote wa namna hiyo (kwa Kiingereza: “asexual”).

Watu wana mang'amuzi tofauti juu ya mwelekeo wao wa kimapenzi. Baadhi wanajitambua kwa muda mrefu kabla hawajaanza uhusiano na wengine.Vivutio vya msingi ambavyo mwelekeo wa kimapenzi huanza kuonekana katika hatua ya ubalehe kwa baadhi ya watu.[2] Wakati huo wengine wanayumba kwa muda fulani katika kujitambua, lakini baadaye baadhi yao hubadilika au kuendelea na mwelekeo waliokuwa nao awali.[3]

Istilahi

Aina kuu za wapenzi wa jinsia moja ni wasagaji, mashoga, na mabasha.

Neno 'basha' hutumika katika baadhi ya tamaduni kumrejelea mwanaume katika mahusiano ya jinsia moja, lakini maana yake hutofautiana.[4][5]

Kwa Kiingereza, shoga anaitwa gay. Hapo awali, gay ilimaanisha "furaha", lakini imekuwa na maana ya mwanamume anayeelekea watu wa jinsia yake, huku wanawake wa namna hiyo wakitajwa kuwa lesbians.

Historia

Historia ya mapenzi ya jinsia moja inarudi nyuma hadi katika ustaarabu wa zamani, ambako mahusiano ya watu wa jinsia moja yaliandikwa katika muktadha mbalimbali wa kitamaduni. Katika Mesopotamia ya zamani, Misri, Ugiriki, na Roma, tabia za ushoga ziliwahi kuonyeshwa waziwazi na, katika baadhi ya jamii, hata kupewa nafasi rasmi[6]. Kwa mfano, mahusiano kati ya wanaume wakubwa kwa umri na wavulana wadogo, yaliyofahamika kama "pederasty," yalikuwa sehemu ya kawaida ya jamii katika Ugiriki ya Kale. Vilevile, ushahidi wa kihistoria unaonyesha kwamba mapenzi ya jinsia moja yalitambuliwa kati ya baadhi ya Kaizari wa Roma, akiwemo Hadrian, ambaye uhusiano wake na Antinous ulikumbukwa sana na kuenziwa.[7]

Kwa kuenea kwa Ukristo kote Ulaya wakati wa mwisho wa Dola ya Roma na katika Enzi za Kati, vitendo vya ushoga vilianza kuangaliwa zaidi kupitia mtazamo wa maadili ya kidini. Kwa kuathiriwa na tafsiri za Biblia, viongozi wa Kikristo wa enzi za kati walilaani mahusiano ya watu wa jinsia moja kama dhambi na uhalifu. Katika jamii nyingi za Ulaya, sheria dhidi ya sodomia ziliwekwa, na kusababisha mateso na mauaji ya watu waliotuhumiwa kwa tabia za ushoga. Licha ya hili, maandiko yanaonyesha kuendelea kuwepo kwa tamaduni za siri za mashoga katika Ulaya ya enzi za kati na mapema ya kisasa, hasa ndani ya miji mikubwa.[8]

Historia ya kisasa ya ushoga ilishuhudia mabadiliko ya taratibu kuanzia karne ya 19, kwa kuibuka kwa harakati za awali za kutetea haki za mashoga, hasa nchini Ujerumani. Karne ya 20 ilishuhudia mabadiliko makubwa ya kisheria, kisiasa, na kijamii, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa makosa ya kisheria kwa ushoga katika nchi nyingi, kuibuka kwa harakati za haki za LGBTQ+, na kukubalika zaidi kwa jamii katika maeneo kadhaa ya dunia. Hata hivyo, ubaguzi na uhalalishaji wa adhabu dhidi ya ushoga bado vinaendelea katika maeneo mbalimbali, kuonyesha tofauti zinazoendelea duniani kuhusu mtazamo wa ushoga.[9]

Sayansi

Hakuna makubaliano kati ya wanasayansi juu ya sababu hasa ambazo humfanya mtu kuwa na mwelekeo wa kupenda jinsia moja ya kwake au kupenda jinsia zote mbili badala ya jinsia tofauti. Hata hivyo, wanasayansi wanakubaliana kwamba chanzo cha mwelekeo wa kimapenzi wa mtu ni muungano changamani wa vipengele vya kibiolojia na kimazingira.[10]

Wanasayansi wengi wanafikiri mwelekeo wa kimapenzi hauwezi kubadilika kwa hiari, utashi, nguvu, au malezi tofauti.[11][12][13] Hadi leo, hakuna utafiti wa kutosha wa kisayansi kuonyesha kwamba tiba inayolenga kubadili mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja ni salama au inafaa. Kwa kuongezea, uhamasishaji wa matibabu ya mabadiliko unaonekana kuchangia mazingira mabaya kwa wapenzi wa jinsia moja.

Misimamo ya sheria

Mashoga wa Marekani.
Wasagaji wa Marekani.
Sheria za nchi kuhusu ushoga      Ndoa za jinsia moja      Mahusiano mengine      Laws against expression      Faini au kifungo (haitekelezwi)      Faini au kifungo      Adhabu ya kifo (haitekelezwi)      Adhabu ya kifo

Pengine mashoga, wasagaji na wapenda jinsia zote mbili hukumbana na unyanyapaa, na hata ukatili kwa sababu ya mwelekeo wao wa kimapenzi tofauti na kawaida. Wengine hubaguliwa mashuleni, vyuoni na sehemu zao za kazi, hata wananyimwa huduma za afya na haki, na hupata msaada mdogo kutoka kwa wanafamilia na marafiki.[14] Hali hiyo huwafanya baadhi ya watu kusita kueleza hadharani mwelekeo wao wa kimapenzi.

Tatizo hilo la kimataifa ni kubwa zaidi katika nchi nyingi za Afrika.[15] Chuki dhidi ya mashoga (kwa Kiingereza: “homophobia”) ina madhara makubwa kwa afya ya akili na ustawi wa wasagaji, mashoga na wapenda jinsia mbili, hasa wakijaribu kuficha mwelekeo wao wa kimapenzi. Unyanyapaa na ukatili vinazidisha mafadhaiko waliyonayo tayari kutokana na kutambua tofauti iliyopo kati ya mwili wao na mwelekeo wao. Mara nyingi wanashindwa kukabili hali hiyo na kujikubali walivyo. Hivyo wako katika hatari ya kuingia ulevi wa aina mbalimbali na kujiua kuliko wenzao wanaovutiwa na jinsia tofauti.[16] Watu wanaotamani kuwasaidia wanaweza kufanya kazi na mashirika husika kuwapatia ushauri nasaha[17] pamoja na kupambana na unyanyapaa.

Mashoga, wasagaji na wapenda jinsia mbili wanaotaka kupunguza unyanyapaa wanaweza kuamua kueleza mwelekeo wao wa kimapenzi, wakiwa waangalifu kulingana na mazingira yao ya kijamii ili kuwa salama kadiri iwezekanavyo. Kuwaambia watu wengine kuwa wewe ni mshiriki wa mapenzi ya jinsia moja au tofauti hujulikana kama “kujitokeza” au “coming out”. Mara nyingi hiyo ni hatua muhimu ya kisaikolojia kwa sababu wanaohisi lazima wafiche mielekeo yao ya kimapenzi huripoti wasiwasi wa mara kwa mara kuliko mashoga na wasagaji ambao wako wazi.[18]

Msimamo wa dini

Mitazamo kuhusu mapenzi ya jinsia moja ndani ya dini hutofautiana. Ingawa mitazamo mingi huchukulia tabia ya mapenzi ya jinsia moja kuwa dhambi[19][19][20][21] , baadhi ya madhehebu, wasomi, na waumini wanathibitisha kwamba mwelekeo wa kimapenzi unaweza kuendana na imani ya kidini. Asilimia fulani ya watu wa LGBTQ+ huripoti kuwa hawaoni mgongano kati ya mwelekeo wao wa kimapenzi na utambulisho wao wa kidini.

Katika Biblia

Kadiri ya Biblia, Mungu baada ya kumuumba Adamu alisema, “Si vema mtu awe peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mwa 2:18). Maana yake, umbile la mwanamume linaelekea kukamilishana na lile la mwanamke kiroho na kimwili. Kwa kuwa roho haionekani, ni rahisi zaidi kuona jinsi miili yao inavyofaa kuungana iwe mwili mmoja. Hata hivyo mkamilishano huo unafanyika katika nafsi pia, ambazo zina vipawa tofauti vinavyowezesha kwa pamoja kukabili vizuri maisha ya nyumbani, ya uchumi, ya siasa, ya dini n.k. Kufikiria uumbaji wa mtu katika jinsia mbili ndiyo njia ya kuelewa Muumba alitaka nini, kwamba jinsia hizo zinalenga kukamilishana katika ndoa kwa kupendana na kuzaliana (Mwa 1:26-28): "Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi".

Baadhi ya maandiko ya Mtume Paulo pia yametumiwa na baadhi ya wakristo kueleza mtazamo wao kuhusu jinsia na ndoa, ingawa tafsiri hizo zinatofautiana.[22]

Katika Kanisa Katoliki

Papa Fransisko, mkuu wa Kanisa Katoliki, ameongea mara kwa mara juu ya hitaji la kukaribisha na kupenda watu wote, bila kujali mwelekeo wao wa kimapenzi, kwa kuwa wote ni sura na mfano wa Mungu. Hata hivyo mafundisho ya Kikatoliki kuhusu mvuto wa jinsia moja yamefupishwa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki. [23]

Tazama pia

Marejeo

  1. "What Does Homosexuality Mean?". Iliwekwa mnamo 2025-02-06.
  2. Long, Monique. "Adolescent Sexuality" (kwa Kiingereza). Umoja wa Mataifa. Iliwekwa mnamo 2024-04-07.
  3. mygenes.co.nz - summary
  4. Amory, Deborah P. (1998). Murray, Stephen O.; Roscoe, Will (whr.). Mashoga, Mabasha, and Magai: 'Homosexuality' on the East African Coast. Boy-Wives and Female Husbands (Ripoti) (kwa Kiingereza). uk. 77.
  5. Böhme, Claudia (2015). "Showing the Unshowable: The Negotiation of Homosexuality through Video Films in Tanzania". Africa Today (kwa Kiingereza). 61: 63–82 – kutoka JSTOR.
  6. Joshua Mark. "Homosexuality in the Ancient world" (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2025-04-27.
  7. Williams, Craig (2010). Roman Homosexuality. Oxford University Press. ISBN 978-0-19-538874-9.
  8. Boswell, John (1980). Christianity, Social Tolerance, and Homosexuality. University of Chicago Press. ISBN 978-0-226-34522-2.
  9. Fone, Byrne (2001). Homophobia: A History. Holt Paperbacks. ISBN 978-0-312-42030-7.
  10. "Sexual orientation, homosexuality and bisexuality" (kwa Kiingereza). American Psychological Association. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-08-08.
  11. "Submission to the Church of England's Listening Exercise on Human Sexuality". The Royal College of Psychiatrists. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-10-16.
  12. Frankowski BL; American Academy of Pediatrics Committee on Adolescence (2004). "Sexual orientation and adolescents". Pediatrics (kwa Kiingereza). 113 (6): 1827–32. doi:10.1542/peds.113.6.1827. PMID 15173519. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-03-20.
  13. Gloria Kersey-Matusiak (2012). Delivering Culturally Competent Nursing Care (kwa Kiingereza). Springer Publishing Company. uk. 169. ISBN 978-0826193810. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2016-11-30. Most health and mental health organizations do not view sexual orientation as a 'choice.'
  14. Tusipopata Huduma, Tutakufa: Kuandamwa kwa LGBT na Kunyimwa Haki ya Afya Tanzania (Ripoti). Human Rights Watch.
  15. The Global Divide on Homosexuality Persists (Ripoti) (kwa Kiingereza). 2020-06-25. Iliwekwa mnamo 2024-04-10.
  16. mygenes.co.nz - suicide
  17. www.lifesitenews.com
  18. "An Open Statement from the Psychological Society of South Africa to the People and Leaders of Uganda Concerning The Anti-Homosexuality Bill 2009" (PDF) (kwa Kiingereza). Psychological Society of South Africa.
  19. 19.0 19.1 Biblia Takatifu Walawi 20:13
  20. "Katekisimu ya Kanisa Katoliki". Iliwekwa mnamo 2024-04-07.
  21. "Do you approach males among the worlds and leave what your Lord has created for you as mates? But you are a people transgressing". — Quran , Surah 26 (165-166)
  22. Waraka kwa Waroma 1:19–27: "19. Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia. 20 Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru; 21 kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. 22 Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; 23 wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. 24 Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. 25 Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. 26 Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; 27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao."
  23. The teachings of the Catholic Church on same-sex attraction are summarized in the Catechism of the Catholic Church: 2357 Homosexuality refers to relations between men or between women who experience an exclusive or predominant sexual attraction toward persons of the same sex. It has taken a great variety of forms through the centuries and in different cultures. Its psychological genesis remains largely unexplained. Basing itself on Sacred Scripture, which presents homosexual acts as acts of grave depravity, tradition has always declared that 'homosexual acts are intrinsically disordered.' They are contrary to the natural law. They close the sexual act to the gift of life. They do not proceed from a genuine affective and sexual complementarity. Under no circumstances can they be approved. 2358 The number of men and women who have deep-seated homosexual tendencies is not negligible. This inclination, which is objectively disordered, constitutes for most of them a trial. They must be accepted with respect, compassion, and sensitivity. Every sign of unjust discrimination in their regard should be avoided. These persons are called to fulfill God's will in their lives and, if they are Christians, to unite to the sacrifice of the Lord's Cross the difficulties they may encounter from their condition. 2359 Homosexual persons are called to chastity. By the virtues of self-mastery that teach them inner freedom, at times by the support of disinterested friendship, by prayer and sacramental grace, they can and should gradually and resolutely approach Christian perfection.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mapenzi ya jinsia moja kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.