Spishi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Ngazi za uainishaji katika biolojia; ngazi ndogo za kati hazionyeshwi

Spishi (kutoka Kilatini "species" yaani aina, maumbile) katika biolojia ni jina la kutaja kundi la wanyama au mimea wa aina moja. Spishi ni Kitengo muhimu katika uainishaji wa kisayansi.

Kwa kuhesabiwa katika spishi ileile haitoshi kama viumbe vinafanana sana ni lazima ya kwamba vinaweza kuzaa pamoja na kuwa na watoto ambao wanaweza kuzaa tena.

Kwa mfano farasi na punda ni spishi mbili tofauti zinazoweza kuzaa lakini watoto wao wanaoitwa baghala hawazai tena. Mbwa wote ni spishi moja hata kama wanaonekana na maumbile tofauti kutokana na historia ya ufugaji wa kuteua sifa kadhaa tu kwa kuzaana. Lakini hata mbwa mkubwa kabisa anaweza kuzaa na mbwa mdogo na watoto wao wanazaa tena.

Spishi za karibu hupangwa pamoja katika jenasi.

Mfano: mbwa, mbweha, mbweha wa Ethiopia na koyote wa Marekani wote ni spishi mbalimbali wa jenasi inayoitwa "canis".

Nususpishi[hariri | hariri chanzo]

Nususpishi ni aina ndani ya spishi moja inayoonesha tofauti za wazi na spishi kwa jumla. Viumbe vya nususpishi moja wanaweza kuzaa na viumbe vya nususpishi nyingine lakini hii haitokei kwa kawaida; mfano moja ni ya kwamba eneo la nususpishi lipo mbali kwa hiyo hawakutani.

Nususpishi inapewa neno la tatu ndani ya jina lake.

Jina la kisayansi[hariri | hariri chanzo]

Kila spishi inaweza kupewa jina la kisayansi kufuatana na kanuni za uainishaji. Hali halisi wanyama wakubwa wameshaainishwa karibu wote lakini bado kuna wadudu, viumbehai wa baharini wengi na bakteria wengi ambao hawakuainishwa bado.

Jina la spishi huwa na maneno mawili: Kwanza jina la jenasi (linaloanza kwa herufi kubwa) halafu neno la pili la kutofautisha spishi (linaloanza kwa herufi ndogo).

Kwa mfano paka ni "Felis silvestris". Felis ni jenasi na paka yumo pamoja na wanyama wengine wanaofanana naye kama simba, tiger au chui. Ndani ya spishi la Felis silvestris kuna nususpishi kadhaa; kwa mfano paka wa porini wa Afrika Kaskazini (Felis silvestris lybica) anayeaminiwa kuwa asili cha paka wa nyumbani (Felis silvestris catus).