Nenda kwa yaliyomo

Majina ya kisayansi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Jina la kisayansi)

Majina ya kisayansi ni majina rasmi katika matawi mbalimbali ya sayansi yanayotumia mara nyingi lugha ya Kilatini, lakini pia maneno kutoka Kiyunani.

Historia ya majina ya kisayansi

[hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha majina ya kisayansi ya kisasa kinapatikana katika Ulaya ya zama za mwamko (kwa Kiing. renaissance). Katika kipindi hicho pamoja na karne zilizofuata misingi ya mfumo wa sayansi ya kisasa ulitokea. Wakati ule lugha ya elimu kote Ulaya ilikuwa Kilatini ambacho kilikuwa lugha ya Roma ya Kale iliyoendelea kutumiwa kama lugha ya dini, sayansi na elimu kwa jumla. Pamoja na Kilatini wataalamu wengi wa Ulaya walijifunza pia Kigiriki cha Kale ambacho ilikuwa lugha siyo tu ya Agano Jipya lakini pia lugha ya vitabu vya kale vilivyosomwa upya ambamo watu walijifunza upya elimu ya zamani iliyosahauliwa kiasi katika karne zilizofuata.

Kutokana na misingi hiyo vyanzo vya mapatano kuhusu istilahi na majina ya kisayansi vilitumia lugha ya Kilatini pamoja na maneno mengi ya Kigiriki. Ushuhuda wake ni majina ya sayansi kwa lugha nyingi:

  • Biolojia ni neno lililotungwa kwa kuunganisha maneno mawili ya Kigiriki βίος bios (uhai) na λόγος logos (neno, elimu)
  • Jiometri ni neno lililotungwa kwa kuunganisha maneno mawili ya Kigiriki γεω geo (Dunia, ardhi) na μετρία metria (upimaji)

Mifano mashuhuri ni kitabu cha "Species Plantorum" (Aina za mimea) cha Carl Linne kilichoandikwa kwenye mwaka 1753 kwa Kilatini na kuwa msingi wa uainishaji wa kisayansi katika biolojia hadi leo.

Majina ya biolojia

[hariri | hariri chanzo]

Utaratibu wa uainishaji wa wanyama na mimea ulioanzishwa na Carl Linnaeus unaendelea kufuatwa hadi leo, hivyo kila mmea au mnyama anapewa jina la kisayansi yenye sehemu mbili: sehemu ya kwanza inataja jenasi na sehemu ya pili spishi. Kwa kawaida jina la mnyama linafuatwa na jina la ukoo (au kifupi chake cha herufi kadhaa) la mtaalamu aliyewahi kueleza spishi hiyo katika maandiko ya kisayansi, pamoja na mwaka ambapo makala yake imetolewa. Jina la mmea linafuatwa na kifupi cha herufi moja au kadhaa cha jina la mtaalamu bila mwaka. Majina ya jenasi na spishi huandikwa kwa mlazo na lile la jenasi linaanzia na herufi kubwa.

Hadi leo spishi za mimea zilizoainishwa na Linnaeus zinatajwa kwa herufi "L." baada ya jina la kisayansi. Kwa mfano, mpunga ni mmea wa jenasi inayotajwa kwa jina la kisayansi kama Oryza (L.) na "L." katika mabano inaonyesha kwamba jenasi hiyo ilielezwa mara ya kwanza na Linnaeus. Lakini jina la kisayansi la simba ni Panthera leo Linnaeus, 1758, kwa sababu pia mnyama huyu aliwekwa na Linnaeus katika utaratibu wa uainishaji wa kisayansi.

Majina ya astronomia

[hariri | hariri chanzo]

Katika masomo mengine yaliyoanza kupanuka katika karne ya 18 na 19 kuna pia istilahi nyingi zenye asili ya Kilatini. Kwenye astronomia wataalamu wa Ulaya walipokea sehemu kubwa ya elimu yao ya awali kutoka kwa Waislamu waliowahi kutunza maarifa ya Wagiriki wa Kale kwa lugha ya Kiarabu. Hivyo nyota nyingi zilizojulikana tangu zamani zinatajwa katika lugha ya kitaalamu ya kimataifa kwa majina yenye asili ya Kiarabu. Mifano ni en:Betelgeuse (), en:Rigel () na en:Altair (). Zilizotambuliwa baadaye zilipewa majina hasa kutoka mitholojia ya Kigiriki na Kilatini.

Pamoja na majina ya Kiarabu au Kilatini, nyota hutajwa pia kwa kundinyota zilimoonekana pamoja na herufi ya Kigiriki inayohesabu kiasi cha uangavu wa nyota katika kundi lake. Mfano: Alfa Centauri [1], yaani nyota angavu zaidi katika kundinyota la en:Centaurus (Kantarusi) na Beta Centauri ambayo ni nyota angavu ya pili katika Kantarusi.

Tangu matumizi ya mitambo ya kisasa yalipoanza idadi ya nyota zilizotambuliwa iliongezeka mara nyingi na hapo kuna orodha mbalimbali zinazotumia namba kwa nyota zote. Orodha ya kisasa zaidi ni "Guide Star Catalog II" iliyopatikana kwa kutumia matokeo ya ugunduzi wa darubini ya anga-nje ya Hubble na kutaja nyota na magimba mengine 945,592,683.[2]

  1. Jina la Kiswahili ni Rijili Kantori
  2. Lasker; Lattanzi, Mario G.; McLean, Brian J.; Bucciarelli, Beatrice; Drimmel, Ronald; Garcia, Jorge; Greene, Gretchen; Guglielmetti, Fabrizia; Hanley, Christopher; Hawkins, George; Laidler, Victoria G.; Loomis, Charles; Meakes, Michael; Mignani, Roberto; Morbidelli, Roberto; Morrison, Jane; Pannunzio, Renato; Rosenberg, Amy; Sarasso, Maria; Smart, Richard L.; Spagna, Alessandro; Sturch, Conrad R.; Volpicelli, Antonio; White, Richard L.; Wolfe, David; Zacchei, Andrea (Agosti 2008). "The Second-Generation Guide Star Catalog: Description and Properties". Astronomical Journal. 136 (2): 735–766. arXiv:0807.2522. Bibcode:2008AJ....136..735L. doi:10.1088/0004-6256/136/2/735. {{cite journal}}: Unknown parameter |displayauthors= ignored (|display-authors= suggested) (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Majina ya kisayansi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.