Uainishaji wa kisayansi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Ngazi za uainishaji katika biolojia; ngazi ndogo za kati hazionyeshwi

Uainishaji wa kisayansi ni namna jinsi wataalamu wa biolojia hupanga viumbehai kama mimea na wanayama kwa vikundi kwenye ngazi mbalimbali. Inaweza kuitwa pia taksonomia.

Tangu muda mrefu watu walitambua ya kwamba wanyama au mimea mbalimbali wanafanana kati yao kwa namna moja au nyingine. Wataalamu walijaribu kupanga aina hizi kwa vikundi vyenye tabia za pamoja. Carolus Linnaeus alianza kuzipanga kwa muundo ulioeleweka kulingana na tabia za maubile yao.

Mfumo wa Linnaeus uliendelezwa baadaye kulingana na nadharia ya Charles Darwin inayoona ya kwamba spishi mbalimbali huwa na chanzo cha pamoja kwa hiyo inawezakana kupanga uhai wote kama matawi ya mti yenye matawi makubwa na tena madogo yanayotoka kwenye makubwa.

Ujuzi wa kisasa kutokana na utafiti wa DNA ndani ya seli za viumbehai unaendelea kuongeza ujuzi wetu kwa hiyo katika mengi uainishaji ni utaalamu unaozidi kubadilika.

Majina ya Kisayansi[hariri | hariri chanzo]

Kila spishi ya viumbehai inapewa jina la kisayansi lenye maneno mawili kufuatana na muundo wa uainishaji. Jina la Kisayansi linaanza kwa kutaja jenasi inayoandikwa kwa herufi kubwa halafu neno la pili kama sehemu maalum ya jina ya spishi ile. Maneno haya huandikwa kwa herufi za italiki. Kwa mabano hufuata jina la mtaalamu wa spishi pamoja na mwaka alikoandika maelezo yake.

Kwa mfano paka anaitwa Felis silvestris (Linnaeus, 1758) na spishi hii inajumlisha paka wa porini na paka wa nyumbani.

  • Felis ni jina la jenasi. Jenasi huandikwa kwa herufi kubwa.
  • "silvestris" ni sehemu ya pili la neno; linasema "wa msituni" kwa sababu inaaminiwa ya kwamba asili ya paka hizi zote ni aina ya paka wa porini wa Asia, Ulaya na Afrika Kaskazini.

Paka wa nyumbani anayefugwa na watu anatazamiwa kama nususpishi na nususpishi hii inaweza kutofautishwa kwa kuongeza neno la tatu "catus" kuwa "Felis silvestris catus". Hili ni jina la nususpishi ya paka wanaofugwa na watu. Nususpishi hii ina aina nyingi ndani yake kutokana na ufugaji na uteuzi lakini zote zimo ndani ya nususpishi ileile.

Katika mabano lipo jina la mtaalamu aliyeeleza spishi hii mara ya kwanza kwa namna ya kisayansi pamoja na mwaka alipoandika. Katika mfano wa paka ni Carolus Linnaeus anayefupishwa mara nyingi kama "L.". Aliandika kitabu chake mwaka 1728.

Umbo la majina katika uinishaji[hariri | hariri chanzo]

Katika ainishaji wataalamu wamepatana jinsi ya kutumia majina kwa ngazi mablimbali. Umbo la majina haya hufuata sarufi ya Kilatini.

Ngazi Mimea
(planta)
Mwani
(algae)
Nyoga
(fungi)
Wanyama
(animalia)
Faila -phyta -mycota
Nusufaila -phytina -mycotina
Ngeli -opsida -phyceae -mycetes
Nusungeli -idae -phycidae -mycetidae
Oda ya juu -anae
Oda -ales
Nusuoda -ineae
Familia ya juu -acea -oidea
Familia -aceae -idae
Nusufamilia -oideae -inae
Kabila -eae -ini
Nusukabila -inae -ina