Nenda kwa yaliyomo

Kalasinga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Guru Nanaki muanzilishi wa ukalasinga

Kalasinga (Kipunjabi ਸਿੱਖੀ sikhi; pia: Usikhi) ni dini yenye asili ya Uhindi inayomwabudu Mungu mmoja tu. Wafuasi wake huitwa Kalasinga au Sikh na kitabu kitakatifu chao ni Guru Granth Sahib.

Idadi ya wafuasi ni takriban milioni 20 na wengi wao wanaishi Uhindi katika jimbo la Punjab. Kutokana na uhamiaji kuna pia jumuiya za Kalasinga huko Uingereza, Marekani, Kanada, Malaysia, Singapore na sehemu mbalimbali za dunia, zikiwa na pamoja na nchi za Afrika ya Mashariki.

Historia

[hariri | hariri chanzo]
Faili:GuruNanakwalking.jpg
Picha ya Guru Nanak.

Kalasinga ilianzishwa katika karne ya 15 na Guru Nanak aliyezaliwa katika familia ya Kihindu wakati wa utawala wa Waislamu juu ya Uhindi ya kaskazini.

Nanak alijishughulisha na dini tangu utotoni na kwenye umri wa miaka 30 aliondoka katika familia akianza kipindi kirefu cha matembezi. Anasemekana alizunguka kote Uhindi akafika pia Makka (Uarabuni), Uajemi na Afghanistan.

Hakukubali ibada nyingi za Uhindu, mafundisho na maandiko ya kidini, matabaka katika jamii. Alisikitika kuona jinsi dini ilivyogawa watu.

Hapo alianza kufundisha dini ya umoja. Wataalamu wengine wameeleza mafundisho yake kama jaribio la kuondoa matatizo kati ya Waislamu na Wahindu kwa kutafuta imani ya pamoja iliyojengwa kwenye misingi ya Uhindu lakini kupokea mengi kutoka Uislamu.

Guru Nanak alifuatwa na maguru tisa wengine. Katikia kipindi hicho polepole Kalasinga waliendelea kuwa jumuiya ya pekee, wakiteswa na watawala wa Kihindu lakini zaidi na watawala Waislamu. Walianza kubeba silaha ili kujihami na kuwa kundi muhimu katika Punjab.

Tangu guru ya kumi Gobind Singh walionekana kabisa kama dini ya pekee. Gobind Singh alikuwa guru wa mwisho wa kibinadamu alitangaza kitabu kitakatifu kuwa "Guru Granth Sahib" au kiongozi.

Kaakar tano

[hariri | hariri chanzo]
Kanga, Kara and Kirpan.

Wanaume hufuata kanuni za "Kaakar tano":

  • kes: nywele ndefu; hawakati nywele wala ndevu wakionyesha ya kwamba kila kitu kilichoumbwa na Mungu ni kizuri
  • kangha: chanuo dogo - nywele zinatakiwa kutunzwa vizuri
  • kara: bangili ya chuma - alama ya kuwa mali ya guru
  • kirpan: upanga mdogo - wawe tayari kutetea imani na haki
  • kaccha: chupi - inamkumbusha sikhi ya kwamba anahitaji kutawala tamaa za mwili wake

Sharti la kukokata nywele limesababisha alama ya nje ya Kalasinga yaani kilemba kwa sababu nywele za kichwa pamoja na ndevu hufungwa katika kilemba na Kalasinga huonekana kirahisi kutokana na vilemba vyao.

Imani kadhaa

[hariri | hariri chanzo]

Kati ya mafundisho ya msingi ni imani katika Mungu mmoja anayeitwa Waheguru. Waheguru au Mungu hana umbo na hawezi kuelezwa na akili ya kibinadamu.

Kama Wahindu wanaamini ya kwamba nafsi ya binadamu huzaliwa tena na tena na shabaha ya dini ni ukombozi katika mzunguko wa kuzaliwa upya. Ukombozi wanauona katika jina la Mungu na jitihada za kujisafisha kiroho.

  • Mungu ni mmoja tu. Aliumba ulimwengu, anautunza na kuwa na uwezo wa kuumaliza.
  • Mungu haingii katika umbile la kibinadamu.
  • Shabaha ya maisha ni kujiondoa katika giza la kiroho na mapenzi ya vitu vya kidunia. Njia yake ni kutakarai na kutamka jina la Mungu.
  • Guru wa pekee ni kitabu kitakatifu cha Guru Granth Sahib.
  • Wanawake ni sawa na wanaume.
  • Kila kalasinga anatakiwa kuchapa kazi na kuwa mwaminifu.
  • Wote wanatakiwa kushirikiana kwa mafanikio ya kazi yao.
  • Kila mmoja anatakiwa kumsaidia mwenzake na hasa mwenye matatizo.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: