Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Ghana

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sherehe ya Waashanti ya viazi vikuu, karne ya 19 kwa mujibu wa Thomas E. Bowdich
Ngome ya Cape Coast
Kasri la Elmina

Historia ya Ghana ilianzia mbali sana, hata kabla ya ukoloni tunaweza kuizunguzia Ghana katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, utawala au jamii.

Historia ya kale[hariri | hariri chanzo]

Kuna ushahidi kutoka kwa maarifa ya mambo ya kale ambao unaonyesha kwamba watu wameishi katika eneo linalojulikana siku hizi kama Ghana kutoka karibu miaka ya 1500 KK (Kabla ya Kristo).[1]

Licha ya hayo, hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa wakazi hao wana uhusiano na wale wa eneo hili kwa sasa. Kwa mujibu wa mapokeo simulizi, mengi kati ya makabila ya Ghana, leo kama vile watu wa chimbuko la makabila kadhaa kama Waakan, Waga na Waewe, walifika Ghana mnamo karne ya 13.

Mengi ya maeneo ya Ghana yanajumuisha eneo lililokuwa la Ufalme wa Ashanti, mojawapo ya falme zilizokuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara kabla ya enzi za ukoloni.

Wahamiaji Waakan walihama kuelekea kusini na kuanzisha mataifa kadhaa, likiwemo lile la kwanza la himaya kuu ya Akan ya Wabono, ambayo kwa sasa inajulikana kama eneo la Brong Ahafo nchini Ghana.

Sehemu kubwa ya eneo la sasa la kusini na kati mwa Ghana ilikuwa imeungana chini ya Himaya ya Ashanti ya Waashanti, tawi la Waakan wa karne ya 16.

Utawala wa Waashanti ilihudumu mwanzoni kama mtandao mlegevu kabla ya kuwa ufalme ulioungana huku ukiwa na urasimu ulioendelea na wenye uchanganuzi mkubwa uliokuwa na makao yake Kumasi. Inasemekana kuwa katika kilele chake, Waasantehene wangeweza kutuma askari 500,000 vitani na kuwa na ushawishi wa kijeshi wa kiwango fulani juu ya majirani wake wote.

Thuluthi moja ya Waashanti wote walikuwa watumwa.[2]

Waga walianzisha muungano wenye ufanisi mnamo 1500[3] na Wagonja, Wadagomba na Wamamprusi, pia walipigania uwezo wa kisiasa katika miaka ya 1620.[3]

Mwanzo wa ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Mawasiliano ya awali na Ulaya kutoka kwa Wareno, walioingia Ghana mnamo 1419, yalizingatia upatikanaji wa dhahabu. Wareno walitua kwanza katika jiji la pwani lililokuwa makazi ya ufalme wa Wafante na kuliita eneo hili Elmina, jina ambalo linamaanisha “mgodi” kwa Kireno.

Mwaka wa 1481, Mfalme John II wa Ureno aliagiza Diogo de Azambuja kujenga Kasri ya Elmina, ambayo ilikamilishwa mwaka uliofuata. Lengo lao lilikuwa kufanya ubadilishanaji wa dhahabu, pembe za ndovu na watumwa, ili kuimarisha mamlaka yao yaliyokuwa yanakua kwa kasi katika eneo hilo.

Kufikia mwaka wa 1598 Waholanzi walikuwa wameungana nao, na kujenga ngome katika maeneo ya Komenda na Kormantsi. Mwaka wa 1637, waliiteka Kasri ya Elmina kutoka kwa Wareno na vilevile Axim mwaka wa 1642 (Ngome ya Mtakatifu Antoni).

Wafanyabiashara wengine kutoka Ulaya walijiunga nao kufikia miaka ya kati ya karne ya 17, hasa Waingereza, Wadenmarki na Waswidi. Wafanyabiashara Waingereza, waliovutiwa na rasilimali katika eneo hilo, waliliita Gold Coast, (Pwani ya Dhahabu), huku nao wafanyabiashara Wafaransa, wakivutiwa na mapambo waliyokuwa wakivaa watu wa pwani, wakiliita eneo la sehemu ya magharibi “Côte d'Ivoire", au Ivory Coast (pwani ya pembe za ndovu).

Zaidi ya ngome na kasri thelathini zilijengwa na wafanyabiashara Wareno, Waholanzi, Waingereza na Wadenmarki.

Eneo la Gold Coast lilijulikana kwa karne nyingi kama ‘Kaburi la Mtu Mweupe’ kwa sababu wengi kati ya Wazungu walioenda huko kutoka Ulaya walikufa kutokana na malaria na magonjwa mengine ya eneo la hari.[4]

Baada ya Waholanzi kuondoka mwaka wa 1874, Uingereza iliiweka Gold Coast chini ya himaya yake. Kufuatia ushindi wa Uingereza mwaka wa 1896, hadi unyakuzi wa uhuru mnamo Machi 1957, eneo la Ghana ya sasa ghairi ya sehemu ya Volta Region (British Togoland), lilikuwa likijulikana kama Gold Coast.

Vita vingi vilitokea baina ya utawala wa kikoloni na baadhi ya mataifa ya eneo hilo vikiwemo Vita vya 1806 vya Ashanti-Fante na mapambano ya kudumu ya Waashanti dhidi ya Waingereza, ambayo yalikoma baada ya Vita vya Tatu baina ya Waashanti na Waingereza (the third Ashanti-British War) (1900-1901).[5]. ]

Hata chini ya utawala wa kikoloni machifu na watu wao walipinga mara kwa mara sera za Waingereza; hata hivyo, ushawishi wa kupinga ukoloni ulikolea baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Mwaka wa 1947 chama kipya cha United Gold Coast Convention (UGCC) kilitoa wito wa “utawala wa kujitegemea katika wakati mfupi iwezekanavyo.”[6]

Kuelekea uhuru[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuongezeka kwa maandamano mnamo 1948, wanachama wa chama cha United Gold Coast Convention walikamatwa, akiwemo Waziri Mkuu na Rais wa baadaye, Kwame Nkrumah. Baadaye, Nkrumah aliunda chama chake mwenyewe, the Convention People's Party (CPP) ambacho kiliongozwa na usemi ‘serikali ya kujitegemea sasa’ (self government now). Alianzisha kampeni ya ‘Vitendo Chanya’ na kupata ufuasi wa watu wa sehemu za mashambani na wa daraja la wafanyakazi.[5]

Kwa mara nyingine Nkrumah alishikwa na kuzuiliwa kwa kuwa msimamizi wa chama ambacho kilisababisha ususiaji, migomo na vitendo vingine vya uasi wa raia.

Hata hivyo, baada ya kushinda wingi wa viti katika Bunge ya Kuunda Sheria mnamo 1952, Kwame Nkrumah aliachiliwa na kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa Masuala ya Serikali.

Baada ya uhuru[hariri | hariri chanzo]

Tao la Uhuru, Accra

Baada ya mazungumzo na Uingereza, hatimaye tarehe 6 Machi 1957 saa sita usiku, Kwame Nkrumah alitangaza Ghana kuwa “huru milele”.[5]

Baada ya uhuru mnamo mwaka 1957 nchi ya Ghana ilikuwa chini ya Kwame Nkrumah ambaye alitoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa uhuru wa nchi nyingine.

Utawala wa Ghana ulikuwa wa kidemokrasia ambao ulipatikana kutoka kwa wakoloni bila kupigana vita bali kwa njia za mazungumzo na msaada wa Umoja wa Mataifa.

Bendera iliyokuwa na rangi nyekundu, dhahabu, kijani kibichi na nyota nyeusi ilikuwa bendera mpya mnamo 1957. Bendera hiyo iliundwa na Theodosia Salome Okoh, na rangi nyekundu inawakilisha damu iliyomwagwa ili kupata uhuru, rangi ya dhahabu inawakilisha ukwasi wa madini wa Ghana, ile ya kijani kibichi inaashiria utajiri wa kilimo na ile nyeusi ni ishara ya Uhuru wa Waafrika.[7]

Huku ikiundwa kutoka kwa muungano wa maeneo ya Gold Coast na British Togoland kufuatia matokeo ya kura ya maoni ya watu yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa mnamo 1956, Ghana ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika Kusini mwa Sahara kunyakua uhuru mnamo 1957.

Kwame Nkrumah, Waziri Mkuu wa kwanza na baadaye Rais wa nchi ya sasa ya Ghana, hakuwa tu kiongozi wa Kiafrika wa kupigana dhidi ya ukoloni ila alikuwa pia mtu aliyekuwa na ndoto ya muungano wa Afrika ambayo haingejipata katika ukoloni mamboleo. Alikuwa kiongozi wa serikali ya kwanza Afrika kukuza Muungano wa Waafrika (Pan-Africanism), wazo ambalo alilipata wakati wa masomo yake katika Chuo Kikuu Cha Lincoln lililoko Pennsylvania (Marekani), wakati ambapo Marcus Garvey alikuwa anapata umaarufu kwa harakati zake za “Back to Africa Movement." Aliunganisha ndoto za Macus Garvey na zile za mwanachuo mashuhuri Mmarekani Mweusi W.E.B. Du Bois ili kuandaa Ghana kisasa.

Kanuni za Ghana za uhuru na haki, usawa na elimu ya bure kwa wote, bila kujali kabila, dini au mila, zinatokana na utekelezaji wa wazo la Pan-Africanism.

Ingawa lengo lake la muungano wa Afrika halikuwahi kuafikiwa, Osagyefo Dr. Kwame Nkrumah, kama ajulikanavyo sasa, alishiriki kwa kiwango kikubwa katika kuzinduliwa kwa Shirika la Umoja wa Afrika, ambalo lilifuatwa mnamo 2002 na Umoja wa Afrika (African Union). Ingawa Nkrumah aliheshimika sana ng’ambo, hakuwa akipendwa katika masuala ya ndani ya nchi.[8]

Hakufeli tu kuanzisha uchumi wa viwanda, ila hata sera zake hukusu uchumi ziliishia kuifanya nchi ya Ghana kuwa maskini kuliko ilivyokuwa wakati wa kupata uhuru. Mafanikio yake yalikuwa kutambuliwa na raia wa Ghana wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa Centenary wake na siku aliliweka kama likizo umma nchini Ghana.

Hatimaye Nkrumah aliondolewa madarakani na jeshi alipokuwa ng’ambo mnamo Februari 1966, na mabadiliko hayo yalikaribishwa na wengi wa wakazi wa Ghana. Inaaminika na wengi wa wachanganuzi wa masuala ya kisiasa kwamba shirika la Marekani la Central Intelligence Agency (CIA) lilihusika na mapinduzi hayo, lakini wazo hilo halijawahi kuthibitishwa.

Mfululizo wa baadaye wa mapinduzi kati ya 1966 na 1981 uliishia kwa kuingia madarakani kwa Liuteni wa Jeshi la Wanahewa (Flight Lieutenant) Jerry Rawlings mwaka wa 1981.

Mabadiliko hayo yalisababisha kusimamishwa kwa katiba ya nchi mnamo 1981 na kupigwa marufuku kwa vyama vya kisiasa. Uchumi ulishuka sana punde baadaye, na Waghana wengi walihamia nchi zingine. Ingawa wengi wa Waghana waliohama walienda Nigeria, serikali ya Nigeria iliwarudisha Ghana karibu Waghana milioni moja mwaka wa 1983.[9]

Punde baadaye, Rawlings aliafikiana na shirika la International Monetary Fund juu ya mkataba wa mpango wa maendeleo (structural development plan) na kubadili sera nyingi za awali za uchumi na hivyo uchumi ukaanza kukua.

Maeneo ya Ghana

Katiba mpya iliyorudisha mfumo wa siasa za vyama vingi ilitangazwa mwaka wa 1992, na Rawlings alichaguliwa kuwa Rais na tena mwaka wa 1996. Katiba ya mwaka wa 1992 ilimzuia kuwania kiti hicho kwa muhula wa tatu, kwa hivyo chama chake, National Democratic Congress, kilimchagua Makamu wake wa Rais, John Atta Mills, kuwania urais dhidi ya vyama vya upinzani.

Huku akishinda uchaguzi wa mwaka 2000, John Kufuor wa chama pinzani cha New Patriotic aliapishwa kama Rais mnamo Januari 2001, na kumshinda tena Mills mwaka wa 2004; hivyo kuhudumia kama Rais kwa mihula miwili.

Mwaka wa 2009, John Atta Mills alichukua mamlaka huku kukiwa na tofauti ndogo sana ya kura 40,000 ambazo ni 0.46% [10] kati ya chama chake, National Democratic Congress, na kile cha New Patriotic Party, tukio hili likiwa la pili la ubadilishanaji wa mamlaka kutoka kwa kiongozi mmoja aliyechaguliwa kihalali kwa mwingine, na hivyo kuimarisha hadhi ya Ghana kama demokrasia iliyo imara.[11]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. "Ghana - MSN Encarta". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-11-01. Iliwekwa mnamo 2015-09-22. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help); Unknown parameter |deadurl= ignored (|url-status= suggested) (help); Unknown parameter |https://www.webcitation.org/5kwpviLJm?url= ignored (help)
 2. Utumwa. [16] ^ Karibu Kwenye Encyclopaedia Britannica's Guide to Black History
 3. 3.0 3.1 "Ghana - MSN Encarta". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-11-01. Iliwekwa mnamo 2015-09-22. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help); Unknown parameter |deadurl= ignored (|url-status= suggested) (help); Unknown parameter |https://www.webcitation.org/5kwpviLJm?url= ignored (help)
 4. Bush kumtakasa Strong Uongozi wa Rais wa Ghana Kufuor. America.gov. 15 Septemba 2008.
 5. 5.0 5.1 5.2 [1] MSN Encarta. Archived 2009/10/31.
 6. Historia ya Ghana - Google Books
 7. Ghana Bendera
 8. Kevin Shillington. Encyclopedia of African history. uk. 575.
 9. "Ghana - MSN Encarta". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-11-01. Iliwekwa mnamo 2015-09-22. {{cite web}}: Unknown parameter |= ignored (help); Unknown parameter |deadurl= ignored (|url-status= suggested) (help); Unknown parameter |https://www.webcitation.org/5kwpu3n3T?url= ignored (help)
 10. BBC: kiongozi wa upinzani wins Ghana uchaguzi - modernghana.com / ghana uchaguzi
 11. "Thousands celebrate as new president takes office", The Guardian, 8 Januari 2009. 
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Ghana kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.