Nenda kwa yaliyomo

Historia ya Ethiopia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya Ethiopia inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Shirikisho ya Ethiopia.

Ni nchi ambayo ina historia ya pekee Afrika na hata duniani kwa ujumla.

Ethiopia ni nchi pekee ya Afrika ambayo haikutawaliwa na wakoloni wakati walipong’ang’ania Afrika. Kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Ethiopia ilivamiwa na Waitalia (1936) lakini ilipata uhuru wake tena baada ya miaka michache.

Historia ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Historia ya binadamu katika Ethiopia ilianza mapema kabisa. Mifupa ya kale kabisa ya viumbe jamii ya watu imepatikana katika nchi hii kwa sababu zilihifadhiwa katika mazingira yabisi ya nchi.

Wataalamu wengi huamini ya kwamba Ethiopia (pamoja na Kenya na Tanzania) inaweza kuwa mahali ambako watu wa aina ya Homo Sapiens walianza kupatikana duniani.

Kuna mabaki mbalimbali ya kiutamaduni yanayochunguzwa na akiolojia, lakini sehemu kubwa ya nchi haijaangaliwa bado kitaalamu. Inaonekana kwamba katika karne za K.K. kulikuwa na uhusiano wa karibu na Uarabuni kwa sababu lugha za Kiethiopia ni karibu na lugha za upande mwingine wa Bahari ya Shamu. Inaaminiwa kwamba watu kutoka Uarabuni Kusini walihamia Ethiopia na kuleta lugha yao huko.

Biblia ina taarifa juu ya ziara ya malkia wa Sheba aliyemtembelea mfalme Suleimani wa Yerusalemu. Milki ya Sheba imedaiwa kuwepo ama Ethiopia ama Yemen na wengine huamini ya kwamba ilikuwa dola la pande zote mbili za mlangobahari wa Bab el Mandeb unaotenganisha Eritrea ya leo na Uarabuni Kusini.

Historia ya kale

[hariri | hariri chanzo]

Milki ya kwanza ya Ethiopia inayoweza kutajwa kutokana na mabaki ya majengo na maandishi ilikuwa milki ya D'mt (pia: Da'amot) katika Ethiopia ya kaskazini pamoja na Eritrea ya leo. Kuna mabaki ya hekalu la Yeha pamoja na makaburi ambako majina ya wafalme kadhaa yamehifadhiwa kwa maandishi kwenye mawe. Lugha ilikuwa karibu sana na lugha za kale za Uarabuni. Ilikuwa na athira juu ya sehemu za kaskazini ya Ethiopia kwa kipindi kikubwa cha milenia ya 1 KK.

Ilifuata milki kubwa ya Aksum, iliyoanzishwa wakati wa kuzaliwa Yesu. Ufalme wa Aksum ulikuwa milki ya kwanza kutawala maeneo makubwa ya Ethiopia. Nabii Mwajemi Mani aliuweka Ufalme wa Aksum kwa utukufu sawa na Roma, Uajemi na Uchina kama nchi zilizokuwa na nguvu duniani karne ya 3 BK, wakati yeye alipoishi.

Ilikuwa karne ya 4 BK ambapo Frumentius, mtu Msiro-Mgiriki aliyekuwa amepotelea baharini kutokana na kuzama kwa jahazi, alishikwa na Wahabeshi na kupelekwa kortini na baadaye kumuongoa mfalme Ezana kuingia Ukristo. Kwa hiyo Wahabeshi wakampa jina Abba Selama. Kwa muda mfupi dini hiyo mpya ilienea kote[1].

Mara nyingi karne ya 6 Aksum ilitawala eneo la Yemeni ng'ambo ya Bahari ya Shamu.

Aksum ilistawi hasa kutokana na biashara kati ya Mediteranea na Bara Hindi iliyopita kwenye mlangobahari wa Bab el Mandeb ikatumia bandari ya Adulis (karibu na Massawa ya leo nchini Eritrea).

Uenezi wa Uislamu ulivuruga biashara hiyo na Aksum ilipoteza utawala juu ya pwani. Kuporomoka kwa uwezo wa kibiashara kunaonekana katika kusimamishwa kwa uchapaji pesa ya wafalme wa Aksum katika karne ya 7. Nchi ilishambuliwa pia kutoka milki za barani.

Mabaki ya ufalme wa Aksum yaliharibiwa mnamo mwaka 900 wakati na malkia Gudit (au Judith) aliyekuwa ama Myahudi ama kiongozi wa makabila ya Kipagani kutoka nyanda za juu.

Milki ya Ethiopia

[hariri | hariri chanzo]

Kiongozi wa kabila la Agaw alimwoa binti wa mfalme wa mwisho wa Aksum akaanzisha nasaba ya Zagwe na kuunda upya ufalme wa Kikristo katika nyanda za juu. Kitovu cha ufalme huu kilipelekwa zaidi mbali na pwani.

Nasaba hii ilipinduliwa mnamo 1270 na Yekuno Amlak aliyetumia jina la kifalme Tasfa Iyasus. Alianzisha nasaba iliyojiita "Wa Suleimani" kwa kudai ilikuwa ukoo wa mwana wa mfalme Suleimani na malkia wa Sheba. Tasfa Iyasus alitumia cheo cha Negus Negesti ("Mfalme wa Wafalme").

Enzi ya Mfalme Lebna Dengel, Ethiopia iliweza kuwasiliana na nchi za Ulaya na kudumisha ubalozi na nchi kama Ureno. Lakini, Mfalme Susenyos alipojiunga na Kanisa Katoliki mwaka 1622, chakari na misukosuko ilifuata. Wamisionari Wajesuiti walichukiwa na waamini wa Kanisa la Ethiopia, na katika hiyo karne ya 17 Susenyos mwana wa Mfalme Basil aliwafukuza wanamisheni hao.

Baadaye Waoromo wakaanza kuasi amri ya Kanisa la Ethiopia na kutafuta njia za dini yao, eneo hili la Uhebeshi.

Mambo hayo yote yalifanya Ethiopia itengwe miaka ya 1700. Wafalme wakawa kama wakurugenzi, ambao waliamriwa na masharifu kama Ras Mikael Sehul wa Tigrinya. Ethiopia ilitoka kutoka utengo kwa kufuatia misheni ya Uingereza kufika Ethiopia na kukamilisha muungano kati ya nchi hizi mbili; lakini, hadi milki ya Tewodros II ndipo Ethiopia ilipoanza tena shauri za Duni.

Mashujaa Ethiopia miaka ya 1800.

Miaka ya 1880 ilikuwa miaka ya Ulaya kung’ang’ania ukoloni Afrika ambapo Waitalia na Waingereza walitafuta kutawala eneo la Assab, bandari iliyoko karibu na mdomo wa bahari ya Shamu. Bedari ya Kusini, karibu na kiingilio cha bahari ya Shamu, ilinunuliwa na Waitalia kutoka sultani mwenyeji Machi 1870 ambayo mwaka 1882 ilizaa koloni la Eritrea.

Haya yalizua magombano kati ya Waethiopia na Waitalia na Vita vya Adowa mwaka 1896, ambapo Waethiopia walishtua dunia kwa kupiga nguvu za wakoloni na kulinda madaraka yao kwa uongozi wa Menelik II. Italia na Ethiopia zilisaini mkataba wa amani tarehe 26 Oktoba 1896.

Karne ya 20 hadi leo

[hariri | hariri chanzo]

Karne ya 20 miaka ya kwanzakwanza ilimilikiwa na Mfalme Haile Selassie I, aliyechukua nafasi ya kuendeleza Ethiopia mpaka uongozi wake ulipokatizwa kwa Vita vya pili vya Uhabeshi na Waitalia (1936). Waingereza na wazalendo wa Jeshi la Ethiopia wakakomboa nchi mwaka 1941, na Waingereza kukiri madaraka ya Ethiopia kwa mkataba wa Uingereza na Ethiopia mnamo Desemba 1944.

Milki ya Haile Selassie ilikoma mwaka 1974, ambapo wazalendo Wakomunisti ("Derg") walimpindua na kuanzisha serikali ya kikomunisti. Hii ilifuatwa na msukosuko wa kupindua serikali, vita na migogoro pamoja na ukame na shida za wakimbizi.

Mwaka 1977 Somalia ilivamia eneo la Ogaden (Vita vya Ogaden), lakini Ethiopia iliweza kuwafukuza Wasomali kwa msaada wa vifaa vya kijeshi vya Urusi, na majeshi ya Kuba, Ujerumani wa mashariki na Yemeni. Usaidizi mwingi kutoka Nchi za Kikomunisti uliwezesha Ethiopia kudumisha mojawapo ya majeshi kubwa Afrika.

Lakini hii haikuzuia ukereketwa wa jimbo la Eritrea na Tigray, ambapo ukame wa mwaka 1985 na mapinduzi ya siasa hasa kwa Kambi za Ujamaa, zilileta uongozi wa Derg 1991 kukoma. Chama cha kukomboa Eritrea (EPLF) na Chama cha Mapinduzi cha Kidemokrasi Ethiopia (EPRDF), ziliungana kukomboa Ethiopia, wengi wa wanamgambo wakiwa wakombozi wa Eritrea.

Mwaka 1993, jimbo la Eritrea ukawa huru kutoka Ethiopia, kufuatia kura ya maoni iliyofanywa ili kumaliza vita hii iliyodumu miaka 20, mojawapo kati ya migogoro ya muda mrefu zaidi Afrika.

Mwaka 1994, Ethiopia kaiweka Katiba mpya ambayo ilileta uchaguzi wa kidemokrasia.

Mwaka 1998 magombano ya mipaka na Eritrea yalileta Vita vya Eritrea na Ethiopia ambayo ilidumu hadi Juni 2000. Vita hivi vilileta uvivu wa uchumi na nguvu ya muungano unaongoza nchi.

Uchaguzi wa Ethiopia uliendekeza wanabaraza kwa viti 547 Bungeni. Baraza hilo la bunge lilijumuika Juni 1994 na kupitisha katiba mpya ya Jimbo la Demokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia mnamo Desemba 1994. Uchaguzi huu ulikuwa wa kwanza kuchagua wanabaraza wa kitaifa kwa sifa bungeni na wanabaraza wa majimbo mnamo Mei na Juni 1995. Vyama vingi vya upinzani viligoma kushiriki uchaguzi. Ushindi ulichukuliwa na Chama cha Mapinduzi cha Kidemokrasi cha Watu wa Ethiopia (EPRDF). Umoja wa Mataifa ukasema vyama vya upinzani vingeweza kushiriki uchaguzi kama zingetaka.

Serikali ya Majimbo ya Demokrasia ya Jamhuri ya Ethiopia ilichukua mamlaka mnamo Agosti 1995. Rais wa kwanza Negasso Gidada. EPRDF ikaongoza serikali na Waziri Mkuu Meles Zenawi ambaye ameunga mkono majimbo ya kikabila, na kuwapa madaraka viongozi wa kikabila. Ethiopia sasa ina maeneo 9 ambayo yana serikali ya madaraka ya shirika, na hata majimbo haya yanakubaliwa kutoza ushuru na kutumia akiba ya ushuru. Hii aina ya serikali imefanya Waethiopia kupata uhuru wa siasa lakini Uhuru wa idhaa na gazeti bado umefinyiliwa.

Serikali ya Zenawi ilichaguliwa tena mwaka 2000 kwa uchaguzi wa kwanza wa Kidemokrasia, Rais akiwa Girma Wolde-Giorgis.

Kutoka 1991, Ethiopia imetafuta urafiki zaidi na Marekani na Umoja wa Ulaya, ili kuweza kukopa pesa za kusaidia uchumi wake na pia kutoka Benki ya Dunia.

Mwaka 2004, serikali ilianza kuhamisha watu kutoka maeneo ya ukame wakisema hii itazuia njaa. [2].

Uchaguzi mwingine wa Ethiopia ulikuwa tarehe 15 Mei 2005, ambao ulivutia wapigakura kiasi cha juu zaidi, asilimia 90% ya wananchi waliojiandikisha. Watazamaji wa Umoja wa Ulaya walidai uchaguzi haujafikia kiwango cha kimataifa, lakini Umoja wa Afrika ulitoa ripoti tarehe 14 Septemba kwamba Waethiopia walionyesha kujitokeza na adabu ya kidemokrasia, halafu tarehe 15 Septemba, US Carter Center, ikasema matokeo ya uchaguzi yaaminika na kuonyesha ushindani wa kisiasa. Uangalizi na ushuhuda wote ulimalizia kuranki Uchaguzi wa Ethiopia na kesi nyingine waipa, asilimia 64% ya matokeo mazuri, na vizuri zaidi kulingana na kesi nyingine 24%.

Katika Uchaguzi wa Ethiopia, 2005 EPRDF ilitokea iking’ang’ania uongozi. Tarehe za kwanza za Juni na tena Novemba, polisi kwa amri ya EPRDF wakafyatua risasi na kuua watu kwa maandamano yaliyokuwa yakipinga matokeo ya kura.

Ni kwamba vyama vya upinzani vililalamika kwamba EPRDF iliiba kura na kuwazisha wananchi na kusema baraza 299, wapata hitilafu ya wizi wa kura. Hayo yote yalichunguzwa na Watazamaji wa Uchaguzi wa kimataifa na pia Kamisheni ya Uchaguzi Ethiopia.

Matokeo ya uchunguzi huo kama haijatokea mnamo Juni 2005, wanafunzi wa chuo kikuu walianza maandamano wakisaidiwa na wanamgambo wa Muungano wa Vyama vya Upinzani. Lakini serikali kwa kutoa amri ya kukomesha maaandamano, mnamo 8 Juni, watu 26 waliuliwa mjini Addis Ababa kwa msukosuko wa maandamano na wengine wengi kushikwa.

Mnamo 5 Septemba 2005, Kamisheni ya Uchaguzi Ethiopia, ilitoa matokeo na kusema kwamba (EPRDF) kashinda uchaguzi na kwa hiyo iongoze serikali. Lakini vyama vya upinzani viliongezea viti bungeni kutoka 12 mpaka 176. Muungano wa umoja na demokrasia ulishinda viti vyote vya Addis Ababa, kwa Bunge la Taifa na Baraza la mtaala.

Maandamano yalizuka tena mitaani 1 Novemba, ambapo vyama vya upinzani viliitisha mgomo kwa jumla na pia kwa Bunge mpya, wakatae matokeo ya uchaguzi. Polisi tena walijaribu kuzuia maandamano hayo na watu 42 wakafa kwa misukosuko mjini Addis Ababa. Polisi saba pia wakafa na mwingine pia kafa kutokana na majeruhi ya mlipuko wa bomu. Tope la watu walishikwa na kufungwa jela. Februari 2006 watu elfu sita bado walikuwa jela wakingoja hukumu Machi.

Mnamo 14 Novemba, Bunge la Ethiopia lilipitisha mkataba kuimarisha Kamisheni huru na kuchunguza visa vya 8 Juni na tarehe 1 na 2 Novemba. Februari 2006 Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair, alitamka kwamba, EPRDF kashinda kura, lakini angetaka kuona Ethipia ikitatua shida zake yenyewe na iendelee katika njia ya demokrasia [2].

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Ethiopia kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.