Historia ya Sudan
Historia ya Sudan inahusu eneo la Afrika Kaskazini ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Sudan.
Historia ya awali
[hariri | hariri chanzo]Nchi ilikuwa na makazi ya kudumu kuanzia milenia ya 8 KK.
Katika milenia ya 5 KK watu walizidi kuhama Sahara ikigeuka jangwa wakasogea katika eneo la Sudan ya sasa (bonde la mto Nile).
Mchanganyiko wa watu hao uliunda ufalme wa Kush kwenye 1700 KK. Makao makuu yalikuwa Kerma.
Katika karne ya 8 KK watu wa ufalme huo waliteka Misri na kuitawala kwa karne moja hadi waliposhindwa na Waashuru.
Baadaye makao makuu yalikuwa Meroe, ambapo ufalme uliendelea hadi karne ya 4 BK ukiwa maarufu kwa uhunzi kwa jina la Ethiopia.
Ufalme kusambaratika
[hariri | hariri chanzo]Ufalme huo uliposambaratika, zilitokea falme mbalimbali katika eneo lake, mmojawapo ukiwa ule wa Nubia.
Huko Ukristo ulienea katika madhehebu tofauti: yale ya Kikopti kutoka Misri na yale ya Kibizanti kutoka Roma ya mashariki.
Baadaye Uislamu pia ulijitokeza katika falme hizo ukazidi kuenea hadi kuanzisha usultani wa Sennar.
Mwaka 1821 mtawala wa Misri chini ya himaya ya Waturuki aliteka Sudan kaskazini.
Katika miaka ya 1870 juhudi za Wazungu za kukomesha biashara ya utumwa zilisababisha kutokea kwa Mahdi.
Dola la Mahdi
[hariri | hariri chanzo]Dola la Mahdi (kwa Kiarabu المهدية, "mahdiyya") lilianzishwa na Muhammad Ahmad Al-Mahdi mwaka 1881 alipojitangaza kuwa mahdi kufuatana na imani ya Kiislamu akaongoza uasi dhidi ya Misri iliyotawala Sudan ikisimamiwa yenyewe na Uingereza.
Muhammad Ahmad Al-Mahdi alifaulu kukusanya wafuasi wengi na kushinda Wamisri. Tarehe 26 Januari 1885 jeshi lake lilitwaa mji mkuu Khartum na kumwua gavana Gordon Pasha.
Al-Mahdi alianzisha mji mkuu mpya ng'ambo ya mto Nile kwa kuunda Omdurman. Wamisri na Waingereza wakatoka nje ya Sudan.
Baada ya ushindi wake Al-Mahdi alikufa na homa ya matumbo.
Ugomvi ulitokea kati ya makamu wake hadi 1891 wakati Abdallahi ibn Muhammad mwenye sifa ya kuwa aliongoza jeshi la mahdi wakati wa mashambulio dhidi ya Khartum alikubaliwa wa viongozi wa mahdiyya akajiita "khalifa".
Khalifa Abdullahi aliimarisha utawala wake wa kuwaua wapinzani bila neema, kati yao wanafunzi na ndugu za mahdi mwenyewe. Akajenga jumba mjini Omdurman linalosimama hadi leo.
Khalifa Abdullahi alijaribu kutumia teknolojia mbalimbali. Akanunua meli za mvuke za mtoni alizoziona Waingereza walizitumia pia akajenga kiwanda cha kutengenezea bunduki. Akaanzisha nyaya za mawasilaino kwa simu. Lakini kwa ujumla vita na utawala wa mahdiyya zilikuwa ziliharubu uchumi iliyoendelea kuzorota.
Khalifa alifaulu kupanua utawala wake juu ya maeneo karibu yote ya Sudan ya leo lakini alishindwa kufikia jimbo la Ikweta ambako Emin Pasha aliendelea kutetea mabaki ya Sudani ya Kimisri.
Itikadi ya kupanua utawala wa mahdiyya kwa njia ya jihad ilimsababisha khalifa kushambulia nchi jirani ya Ethiopia iliyotawaliwa na kaisari wa Kikristo. Mwaka 1887 akaongoza jeshi la askari 60,000 hadi Gondar. Waethiopia wakajibu kwa kushambulia Sudan mwaka 1889. Kifo cha Kaisari Yohane IV katika mapigano ya Metemma tarehe 9 Machi 1889 ililazimisha Waethiopia kurudi kwao. Lakini jeshi la mahdiyya lilipoteza wanajeshi wengi pia likadhoofika.
Wakati huohuo jemadari wa khalifa Abd ar-Raħmān an-Nujumī alishambulia Misri lakini alishindwa kwenye mapigano ya Tushkah. Hii ilikuwa mara ya kwanza ya jeshi la mahdiyya kushindwa.
Majaribio ya vita za jihadi dhidi ya Wabelgiji katika jimbo la Ikweta na dhidi ya Waitalia katika Eritrea yalishindikana pia.
Mwaka 1895 mkuu wa jeshi la pamoja la Misri na Uingereza, jenerali Horatio Kitchener aliamua kulipiza kisasi kwa vita ya 1885 akaongoza jeshi kubwa dhidi ya Sudan. Kwa kutumia meli za mvuke kwenye mto Nile na kujenga reli akasongea mbele hadi Omdurman.
Tarehe 2 Septemba 1898 jeshi la mahdiyya lilishindwa kabisa katika mapigano ya masaa matano. Safari hiyo Waingereza waliandaliwa vizuri zaidi, pia silaha mpya kama bunduki ya mtombo ziliwapa ushindi. Upande wa khalifa walikufa askari 11,000, upande wa Waingereza na Wamisri watu 400 pekee.
Khalifa mwenyewe alitoroka akajenga jeshi upya na kutawala kusini mwa Sudan, lakini akauawa mwaka 1899 katika mapigano ya Umm Diwaykarat.
Hivyo Waingereza walitawala Sudan pamoja na Misri hadi 1956, na Kitchener akawa gavana mkuu wa kwanza.
Baada ya Uhuru
[hariri | hariri chanzo]Baada ya uhuru wa nchi (1956), makabila ya kusini, ambayo hayakukubali kusilimishwa, yalipigania vita ndefu hadi kupata uhuru wao.
Darfur ni eneo lenye majimbo matatu ambayo imeathiriwa na vita vya kisiasa, vita vya Darfur.
Kutokana na vita vingi serikali hazikuwa imara na kulikuwa na mabadiliko ya mara kwa mara baada ya uhuru. Mapinduzi ya kijeshi ya kwanza yalitokea mwaka 1958, kisha jenerali Ibrahim Abboud alitawala hadi 1964 wakati alipopaswa kujiuzulu kutokana na upanuzi wa vita katika Sudan Kusini na upinzani wa wananchi kwenye mji mkuu.
Kilifuata kipindi cha serikali tatu za kiraia hadi mwaka 1969.
Utawala wa Nimeiry
[hariri | hariri chanzo]Tarehe 25 Mai 1969 jeshi, chini ya kanali Gaafar Nimeiry, lilipindua tena serikali. Nimeiry alikuwa waziri mkuu, wakati bunge na vyama vyote vilipigwa marufuku. Nimeiry alitawala hadi 1985, na tangu 1971 alikuwa rais. Mwaka 1972 alifaulu kumaliza awamu ya kwanza ya vita ya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya Sudan Kusini kwa mapatano ya Addis Ababa. Sudan Kusini ilipewa mamlaka ya kujitawala katika mambo ya ndani chini ya serikali ya kieneo.
Mwanzoni Nimeiry alijaribu kuiga siasa ya Gamal Abd el Nasser nchini Misri na kutekeleza sera kadhaa za ujamaa. Utawala wake uliona upinzani kutoka kwa Wakomunisti na pia kutoka Waislamu wenye itikadi kali. Baada ya kupinduliwa kwa siku kadhaa na Wakomunisti alivunja ushirikiano na Urusi na kuanza kupokea wanasiasa wenye mwelekeo wa Uislamu mkali katika serikali yake.
Tangu miaka ya 1980 alisogea zaidi upande wa Uislamu wa kisiasa. Mwaka 1983 alitangaza sharia kuwa msingi wa sheria zote na kubadilisha sheria za jinai ipasavyo. Hatua hii ilisababisha upinzani katika sehemu za nchi zisizokaliwa na Waislamu. Alivunja pia serikali ya kieneo kwa Sudan Kusini na hivyo vita ya wenyewe kwa wenywewe ilianza upya.
Nimeiry alitangaza hali ya dharura iliyompa tena mamlaka za kidikteta. Mwaka 1985 aliruhusu kunyongwa kwa mwanafalsa Mwislamu Mahmoud Mohammed Taha kwa kosa la "uasi dhidi ya Uislamu". Miezi minne baadaye Nimeiry alipinduliwa kwenye mwaka huohuo.
Utawala wa Bashir
[hariri | hariri chanzo]Sudan ilirudi kwa miaka michache chini ya serikali ya kiraia. Mapinduzi yaliyofuata mwaka 1989 yalileta utawala wa jenerali Omar al-Bashir. Vita ya wenyewe kwa wenye iliendelea hadi mwaka 2005 ikamalizika kwa Mapatano ya Naivasha baina ya Sudan na SPLA. Sudan Kusini ilipewa miaka hadi 2011 kujitawala halafu kuwa na kura ya wananchi wa kusini kuhusu uhuru uliotangazwa mwaka uleule.
Tangu mwaka 2003 Bashir alisimamia pia vita ya jeshi lake na wanamgambo dhidi ya wakazi wasio Waarabu wa Darfur waliopinga utawala wake.
Mwaka 2019 Bashir alipinduliwa na jeshi lake baada ya wiki kadhaa za maandamano ya wananchi wa Khartum na miji mingine dhidi yake.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Sudan kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |