Sahara

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Sahara jinsi inavyoonekana kutoka angani
Oasisi katika Sahara (Libya)
Matuta ya mchanga katika Sahara
Kumwagilia mashamba katikati ya Sahara

Sahara ni jangwa kubwa kabisa barani Afrika, ni la kwanza duniani kati ya majangwa joto na jangwa la tatu kwa ukubwa ulimwenguni baada Bara la Antaktiki na Aktiki.

Ina eneo la kilometa za mraba 9,065,000, sawa na eneo la Marekani au karibu sawa na eneo lote ya Ulaya.

Jina lake ni neno la Kiarabu (صحراء, sahra') linalomaananisha "jangwa".

Wataalamu wa jiografia huamini ya kwamba Sahara haikuwepo wakati wote. Kutokana na utafiti wa dalili katika udongo na mawe yake eneo la Sahara katika milenia zilizopita lilikuwa na vipindi vya ukame vikifuatana na vipindi vya mvua.

Eneo[hariri | hariri chanzo]

Sahara iko kaskazini mwa Afrika. Ina nchi za Moroko, Algeria, Tunisia na Libya upande wa kaskazini. Upande wa kusini kuna nchi za kanda la Sahel.

Upande wa magharibi Sahara inaanza kwenye pwani ya Atlantiki ikielekea hadi pwani ya Bahari ya Shamu kwa km. 5000

Oasisi ya mto wa Nile inakata eneo lake.

Nchi zenye sehemu kubwa ya maeneo yao katika Sahara ni hizi: Misri, Libya, Mali, Niger, Chad, Sudan, Mauretania, Sahara ya Magharibi, Moroko, Algeria na Tunisia.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Hali ya hewa ni ya joto na yabisi. Halijoto ni kati ya +58 °C wakati wa mchana ikishuka usiku hadi +13 °C (mlimani hadi -10 °C). Wastani wa mvua katika Sahara ni mm 45.5 kwa mwaka lakini kuna miaka bila mvua yoyote.

Kuna milima mikubwa kama milima ya Ahaggar, Tibesti na Aïr. Mlima mrefu ni Emi Koussi (m 3415) kwenye milima ya Tibesti katika Chad.

Jiolojia[hariri | hariri chanzo]

Sahara haikuwa jangwa wakati wote. Michoro ya watu wa zamani inaonekana katika milima ya Tibesti na Air inayoonesha watu wawindaji na wanyama kama viboko na mamba wanaohitaji maji mengi. Wataalamu wamegundua kutokana na utafiti wa mawe na udongo ya kwamba eneo la Sahara lilikuwa na vipindi vikavu na vipindi vya mvua nyingi.

Mnamo miaka 7000 iliyopita Sahara ilikuwa eneo nusu yabisi penye maji katika mito mirefu. Labda inawezekana kuilinganisha na Kenya ya Kaskazini ya leo. Watu waliwinda na kufuga wanyama.

Mnamo miaka 5000 iliyopita Sahara ilikauka kufikia hali yabisi kama leo. Lakini maji ya mvua ya nyakati zile bado yapo chini ya ardhi. Misri na Libya ina miradi mikubwa kutumia maji yale kwa pampu na kuanza kilimo jangwani kabisa.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Chris Scott. Sahara Overland. Trailblazer Guides, 2005.
  • Michael Brett and Elizabeth Frentess. The Berbers. Blackwell Publishers, 1996.
  • Charles-Andre Julien. History of North Africa: From the Arab Conquest to 1830. Praeger, 1970.
  • Abdallah Laroui. The History of the Maghrib: An Interpretive Essay. Princeton, 1977.
  • Hugh Kennedy. Muslim Spain and Portugal: A Political History of al-Andalus. Longman, 1996.
  • Richard W. Bulliet. The Camel and the Wheel. Harvard University Press, 1975. Republished with a new preface Columbia University Press, 1990.
  • Eamonn Gearon. The Sahara: A Cultural History. Signal Books, UK, 2011. Oxford University Press, USA, 2011.
  • János Besenyő. Western Sahara (2009), free online PDF book, Publikon Publishers, Pécs, ISBN 978-963-88332-0-4, 2009
  • Lizzie Wade. Drones and satellites spot lost civilizations in unlikely places, Science (American Association for the Advancement of Science), DOI: 10.1126/science.aaa7864, 2015

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Sciences de la terre.svg Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Sahara kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Anwani ya kijiografia: 23°N 13°E / 23°N 13°E / 23; 13