Mali

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kwa maana nyingine ya neno hili angalia Mali (maana)
Mali
Bendera
Nembo
Mji mkuu (na mkubwa zaidi){{{mji_mkuu}}}
12°39′ N 8°0′ W
Lugha rasmi{{{lugha_rasmi}}}
Serikali{{{serikali}}}
{{{vyeo_viongozi}}}{{{majina_viongozi}}}
{{{muundo_uhuru}}}{{{tarehe_uhuru}}}
Eneo
 • Eneo la jumla{{{eneo_jumla}}}
 • Maji (%){{{maji}}}
Idadi ya watu
 • Kadirio la 2023{{{watu_kadirio}}}
Pato la TaifaKadirio la 2023
 • Jumla{{{pato}}}
 • Kwa kila mtu{{{pato_kwa_mtu}}}
Pato Halisi la TaifaKadirio la 2023
 • Jumla{{{pato_halisi}}}
 • Kwa kila mtu{{{pato_halisi_kwa_mtu}}}
Maendeleo ({{{mwaka_maendeleo}}}){{{maendeleo}}}
Fedha{{{fedha}}}
Majira ya saa{{{majira_saa}}}
Muundo wa tareheDD/MM/YYYY
Ramani ya Mali

Mali (kwa Kifaransa: République du Mali = Jamhuri ya Mali) ni nchi ya Afrika ya Magharibi.

Imepakana na Algeria, Mauritania, Niger, Burkina Faso, Cote d'Ivoire na Senegal. Mali haina pwani kwenye bahari yoyote.

Sehemu ya juu ni mlima Hombori Tondo (mita 1155 juu ya UB) ulioko katikati ya nchi.

Upande wa Kaskazini sehemu kubwa ya eneo la Mali ni jangwa la Sahara.

Wakazi walio wengi huishi kusini, karibu na mito Senegal na Niger.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Theluthi mbili za eneo la Niger ni jangwa. Maeneo mengine ni ya Sahel na kanda la Sudan. Sehemu za kusini ni hasa tambarare za bonde la mto Niger.

Hali ya hewa ni tofautitofauti, kulingana na eneo. Kuna kanda tatu:

  • Kanda la jangwani kaskazini - usimbishaji chini ya mm 100 kwa mwaka, yabisi na yabisi sana. Hapa wanaishi wafugaji pekee.
  • Kanda la Sahel: mbuga nusu yabisi inayobadilika kuwa savana kusini kwenye mvua zaidi. Kuna kilimo kando ya mto Niger.
  • Kanda la Sudan lina usimbishaji wa mm 1400 . Lina savana ilhali miti inaongezeka hadi kufika hali ya misitu kabisa kusini.

Kuna malighafi kama vile dhahabu, urani, fosfati, kaolini, chumvi na chokaa.

Ugatuzi wa nchi[hariri | hariri chanzo]

Makala kuu: Mikoa ya Mali Baada ya uhuru Mali ilikuwa na mikoa 8. Tangu mwaka 2016 Mali imegawanywa katika mikoa kumi na eneo la pekee la mji mkuu.

Sheria ya mwaka 2012 ililenga kuwa na mikoa 19[1], lakini hadi mwaka 2023 kuna mikoa miwili mipya pekee iliyoanzishwa.

Kila mkoa unaitwa jina la mji mkuu wake. Mikoa imegawanywa katika wilaya (cercles) 56. Wilaya zote zimegawanywa katika manispaa (communes) 703 . [2]

Historia[hariri | hariri chanzo]

Mali ina historia ndefu ambayo ni historia ya pamoja ya nchi za kanda la Sahel na kanda la Sudan.

Zamani za Wafinisia na za Waroma palikuwa na mawasiliano ya biashara na nchi za Mediteranea kupitia wanafayabiashara Waberberi walioelewa njia za Sahara.

Uvamizi wa Wavandali katika Afrika ya Kaskazini ulivuruga mawasiliano hayo.

Dola la Ghana

Baada ya uvamizi wa Waarabu na uenezaji wa Uislamu biashara ilianza upya. Ndio Waberberi Waislamu walioingiza dini mpya hata kusini ya Sahara.

Katika eneo la Mali ya leo pamoja na nchi jirani ni hasa madola matatu makubwa yaliyotawala upande wa kusini wa njia za biashara iliyovuka Sahara.

Dola la Ghana[hariri | hariri chanzo]

Dola la kwanza lilikuwa Dola la Ghana. Kuanzia karne ya 8 BK hadi mwaka 1076 lilitawala biashara ya dhahabu, pembe za ndovu na chumvi. Mji mkuu ulikuwa Kumbi Sale wenye wakazi 30,000 katika Mauretania ya leo.

Taarifa za wanahistoria Waarabu zimeonyesha ufalme tajiri. Utamaduni wake haukuwa wa Kiislamu bali wa Kiafrika asilia.

Mwisho wake ulianza wakati jeshi la Wamurabitun kutoka Moroko lilivuka jangwa na kuvamia Kumbi Sale.

Milki ya Mali[hariri | hariri chanzo]

Eneo la Dola la Mali

Milki ya Mali ilianza kama ufalme mdogo wa Wamalinke kando ya Ghana. Wakati wa karne ya 13 ilianza kupanuka chini ya mfalme Sundiata Keita. Sundiata mwenyewe alipokea Uislamu mnamo 1240 BK na wafalme baada yake waliendela kuwa Waislamu.

Mfalme wa Mali aliyejulikana zaidi ndiye Mansa Kankan Musa I (13121337). Miaka 1324-1325 alihiji kwenda Makka. Alisafiri na dhahabu nyingi sana. Huku Misri alitoa zawadi kiasi cha kuharibu thamani ya dhahabu kwa miaka 12 iliyofuata.

Wakati ule mji wa Timbuktu ulikuwa kitovu cha biashara na elimu iliyojulikana kote katika umma wa Kiislamu hata Ulaya.

Katika karne ya 14 BK uwezo na utawala wa Mali ulipungua na Songhai ilichukua nafasi yake.

Dola la Songhai[hariri | hariri chanzo]

Eneo la Dola la Songhai

Asili ya Wasonghai ilikuwa Nigeria ya Kaskazini ya leo. Walipanua utawala wao kuelekea magharibi wakapokea Uislamu wakati wa uvamizi wa Almurabitun.

Mnamo mwaka 1250 walikuwa chini ya Mali lakini katika karne ya 14 walijipatia uhuru tena, wakaanza kushika maeneo ya Mali yenyewe.

Kilele cha nguvu yake ilikuwa wakati wa mfalme Askia Mohammad I katika karne ya 16 walipotawala eneo kubwa kutoka Kano (Nigeria) hadi pwani ya Atlantiki. Wakati wake mji wa Timbuktu ilitembelewa na msafiri Leo Africanus aliyeleta baadaye habari za nchi hadi Ulaya.

Utawala wao uliporomoka baada ya mashumbulizi kutoka Moroko mwaka 1591. Wakati ule mataifa ya Ulaya yameshaanza kufika kwenye mwambao wa Afrika ya Magharibi wakifungua biashara ya moja kwa moja na Ulaya. Umuhimu wa biashara ya kuvuka Sahara ulipungua vikali pamoja na faida iliyopatikana kwa watawala katika maeneo ya Sahel.

Kipindi cha madola madogo na jihadi[hariri | hariri chanzo]

Kilichofuata kilikuwa kipindi cha madola madogo. Viongozi Waislamu walijaribu mara kadhaa kujenga utawala juu ya eneo lote.

Anayejulikana zaidi alikuwa Alhaj Omar aliyepiga vita kwa jina la dini ya Kiislamu dhidi ya Wabambara waliofuata utamaduni na dini asilia za Kiafrika.

Mtoto wa Alhaj Omar aliyeitwa Ahmadu alijaribu kuendeleza jihadi yake. Lakini wakati ule Wafaransa walianza kuenea katika Afrika ya Magharibi wakamshinda.

Mali ikawa koloni la Ufaransa kuanzia mwaka 1895. Ilikuwa sehemu ya Afrika ya Magharibi ya Kifaransa, na kuanzia 1920 ya Sudan ya Kifaransa.

Mji wa Bamako

Uhuru[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1960 Mali pamoja na Senegal zilipata uhuru kama "Shirikisho la Mali". Baada ya Senegal kuacha umoja huo, Jamhuri ya Mali chini ya rais wa kwanza Modibo Keïta ikawa nchi ya kujitegemea.

Keita alipinduliwa mwaka 1968 na wanajeshi akishtakiwa kuwa ameharibu uchumi na kujitajirisha. Kiongozi mpya Moussa Traoré alitawala kama dikteta wa kijeshi, baadaye kwa msaada wa katiba ya chama kimoja.

Mabadiliko yaliyotokea kote Afrika tangu mwisho wa Ukomunisti kuanzia miaka ya 1990 yalisababisha kupinduliwa kwa Traoré katika Machi 1991 na kamati ya kijeshi iliyoongozwa na Amadou Toumani Touré.

Katiba mpya ya mwaka 1992 iliunda kipindi cha kura huru alimoshinda Amadou.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe kaskazini na maasi ya kijeshi[hariri | hariri chanzo]

Kaskazini mwa Mali kunakaliwa hasa na Watuareg na baadhi yao hawakupenda kuwa chini ya Mali. Hivyo mara kadhaa kulikuwa na mapigano kati yao na jeshi la nchi. Tangu mwaka 2012 mapigano yameanza upya[3]. Mwaka huo wanamgambo na wanajeshi walikimbia vita kwenda Libya na kujiunga na wapiganaji Watuareg waliotangaza mnamo Aprili 2012 uhuru wa eneo la "Azawad" katika mikoa ya Timbuktu, Gao na Kidal. Lakini wanamgambo wa makundi yenye mwelekeo mkali wa Kiislamu kama Al-Qaeda waliwashinda Watuareg na kushika utawala wakianzisha mfumo wa sharia ya Kiislamu[4].

Serikali ya Mali iliomba usaidizi wa kijeshi wa Ufaransa uliokubaliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa azimio na. 2085 ya tarehe 20 Desemba 2012. Jeshi la Kifaransa lilifaulu kuwaondoa wanamgambo Waislamu katika miji yote[5] lakini hao waliendelea kujificha kwenye milima.

Baada ya mwisho wa kampeni ya Wafaransa nafasi yao ilichukuliwa na jeshi la Umoja wa Mataifa lililoingia kwa jina la "MINUSMA"[6] lililokuwa na wanajeshi kutoka nchi 60. Kati ya nchi hizo, 19 ni za Kiafrika ambazo walileta idadi kubwa ya askari.

Mapigano yameendelea. Wananchi wengi vijijini walichukua silaha na kuunda vikundi vya wanamgambo kwa kujihami lakini vikundi hivyo vinashambuliana pia.[7]

Miaka 2020 na 2021 jeshi la Mali liliasi mara mbili na kupindua serikali za kiraia[8][9]. Kanali Assimi Goïta alitangazwa kuwa rais mtendaji. ECOWAS na Umoja wa Afrika vilisimamisha uanachama wa Mali[10]. Ufaransa na nchi nyingine zilianza kuondoa wanajeshi katika ushirikiano na jeshi la kitaifa[11].

Mnamo Januari 2022 wanajeshi kutoka Urusi walianza kufika Mali kwa kibali cha serikali ya kijeshi[12].

Watu[hariri | hariri chanzo]

Katika maeneo makubwa ya kaskazini wanaishi makabila ya Waberberi, hasa Mauri na Watuareg ambao ni wahamaji. Ndio 10% ya wakazi wa nchi wakikalia asilimia kubwa za eneo.

Kikundi kikubwa ndio Wabambara (33.3%) katika eneo la mji mkuu Bamako, halafu wako Wafula, Wasoninke, Wasenufo/Wabwa, Wamandinka, Wadogon, Wasonghai, Watuareg na wengineo.

Lugha[hariri | hariri chanzo]

Kutokana na ukoloni, Kifaransa kilikuwa lugha rasmi, lakini sasa kimeshushwa cheo na kuwa lugha ya mawasiliano tu. Kibambara ndiyo lugha inayoeleweka na takriban 80% za wakazi, nacho kimefanywa lugha rasmi pamoja na nyingine 12 kati ya lugha asilia 56 zinazotumika nchini.

Dini[hariri | hariri chanzo]

Uislamu ni dini kubwa nchini (95 % za wakazi). Wakristo wanafikia 2.3% (Wakatoliki 1.9% na Waprotestanti 0.4%). Wachache wanafuata bado dini asilia za Kiafrika (2.5%).

Ibada na desturi asilia zinapatikana pia katika mazingira ya Waislamu.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. LOI No 2012-017 DU 02 MARS 2012 PORTANT CREATION DE CIRCONSCRIPTIONS ADMINISTRATIVES EN REPUBLIQUE DU MALI. Journal officiel de la République du Mali (2 March 2012). Jalada kutoka ya awali juu ya 2018-11-23. Iliwekwa mnamo 21 February 2017.
  2. Loi N°99-035/ Du 10 Aout 1999 Portant Creation des Collectivites Territoriales de Cercles et de Regions (in French), Ministère de l'Administration Territoriales et des Collectivités Locales, République du Mali, 1999, archived from the original on 2012-03-09 .
  3. Mali clashes force 120 000 from homes Archived 10 Oktoba 2017 at the Wayback Machine. News24 (22 February 2012). Retrieved 23 February 2012.
  4. Tiemoko Diallo. "Islamists declare full control of Mali's north", Reuters, 28 June 2012. 
  5. "French Troops Retake Kidal Airport, Move into City", USA Today, 30 January 2013.  French troops retake the last remaining Islamist urban stronghold in Mali.
  6. United Nations Multidimensional Integrated Stabilization Mission in Mali
  7. ""We Used to Be Brothers" | Self-Defense Group Abuses in Central Mali". Human Rights Watch (in English). 7 December 2018. Retrieved 30 March 2019. 
  8. Mali timeline: From military coup to interim leaders removed (en) (25 May 2021).
  9. Mali President, PM Resign After Arrest, Confirming 2nd Coup in 9 Months. VOA News (26 May 2021).
  10. "ECOWAS suspends Mali over second coup in nine months", May 31, 2021. Retrieved on June 2, 2021. 
  11. French military suspends joint operation with Mali military. The Associated Press (June 2, 2021).
  12. Russian military advisors arrive in Mali after French troop reduction (en) (2022-01-07).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira