Réunion

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kisiwa cha Réunion
Région Réunion
Nembo
Jina la Kifaransa Région Réunion
Jina la kawaida Reunion
Mji Mkuu Saint-Denis
Eneo 2,512 km²
Mkuu wa Mkoa Didier Robert
(UMP) (tangu 2016)
Idadi ya wakazi 706,300
Sensa ya mwaka 1999
Wakazi kwa km² 309
Wilaya (arrondissements) 4
Ramani Reunion na Ufaransa bara

Réunion (kwa Kifaransa: La Réunion) ni kisiwa cha Afrika na mkoa wa ng'ambo wa Ufaransa (kwa Kifaransa: département d'outre-mer, au DOM) katika Bahari Hindi. Kisheria hali yake ni sawa na mikoa mingine ya Ufaransa hivyo ni pia sehemu ya Umoja wa Ulaya.

Eneo lake[hariri | hariri chanzo]

Reunion iko km 800 upande wa mashariki wa Madagaska. Pamoja na visiwa vya Mauritius na Rodrigues inaunda funguvisiwa la Maskareni.

Kisiwa kina eneo la km² 2.512 kikiwa na kipenyo cha km 50 hadi 70.

Milima mikubwa ni ya kivolkeno. Upande wa mashariki wa kisiwa ndipo mlima wa "Piton de la Fournaise" wenye urefu wa mita 2611 uliolipuka zaidi ya mara 100 tangu kumbukumbu ya kimaandishi ilipoanzishwa mwaka 1640. Mlipuko wa mwisho hadi leo ulitokea tarehe 4 Oktoba 2005.

Mlima wa "Piton des Neiges" ndio mkubwa kisiwani ikiwa na 3070 m juu ya UB.

Hali ya hewa[hariri | hariri chanzo]

Hali ya hewa ni ya joto mwaka wote. Majira ya mvua ndiyo kati ya Desemba hadi Machi.

Historia na Utawala[hariri | hariri chanzo]

Taarifa za kwanza za kimaandishi hudokeza kwamba kisiwa kilikuwa bila ya wakazi.

Waarabu waliita "dina margabin" yaani kisiwa cha magharibi.

Baharia Mreno Diego Dias alifika tarehe 9 Februari 1513 ambayo ni sikukuu ya Mt. Apolonia katika mapokeo ya Kanisa Katoliki na kukiita kisiwa kwa jina la mtakatifu huyu "Santa Apolonia", jinsi inavyoonekana katika ramani za kwanza.

Baadaye Wareno walitumia jina la nahodha maarufu Pedro de Mascarenhas na kujumlisha visiwa vya Reunion, Mauritius na Rodrigues kwa jina la visiwa vya Maskareni. Visiwa hivyo vilikuwa na umuhimu fulani kama vituo vya kupumzika katika safari kati ya Ulaya na Bara Hindi, mabaharia wakitafuta maji ya kunywa, nafasi ya kutengeneza jahazi zao na kuongeza chakula. Lakini hapakuwa na makao ya kudumu kisiwani.

Utawala wa Kifaransa[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1640 Wafaransa walivamia kisiwa na kukitangaza kuwa mali ya Ufaransa. Walikiita "Île Bourbon" kutokana na jina la familia ya wafalme wa Ufaransa.

Mwaka 1665 walowezi wa kwanza Wafaransa walianza kujenga nyumba zao.

Ufalme ulipoondolewa wakati wa mapinduzi ya Ufaransa kisiwa kimepewa jina jipya la Reunion tarehe 17 Machi 1793.

Wakati wa vita vya Napoleoni, Waingereza walivamia kisiwa mwaka 1810 lakini wakakirudisha kwa Wafaransa baada ya vita (1815).

Visiwa vya Maskarena kati ya visiwa vya Kiafrika katika Bahari Hindi.

Uchumi wa mashamba na watumwa[hariri | hariri chanzo]

Walowezi Wazungu walianzisha mashamba kwa ajili ya mahitaji ya jahazi zilizopita.

Kuanzia mwaka 1718 mazao ya biashara yalilimwa, kwanza kahawa baadaye pia vanilla na hasa sukari. Kwa kusudi hilo watumwa walipelekwa Reunion kutoka Afrika bara, Bara Hindi na Madagaska.

Mwaka 1768 kisiwa kilikuwa na wakazi huru 26,284 (hasa Wafaransa) na watumwa 45,000.

Ufaransa ulitia sahihi maazimio ya Mkutano wa Vienna mwaka 1815 pamoja na kumaliza biashara ya watumwa lakini biashara hii iliendelea kwa siri na kupanuka hasa kwa wafungwa kutoka Afrika. Idadi ya watumwa iliendela kuongezeka hadi kuondolewa hali ya utumwa tarehe 20 Desemba 1848.

Baada ya mwisho wa utumwa walowezi walitafuta wafanyakazi huko Bara Hindi wakachukua Wahindi wasiofika kama watu huru kwa miaka na haki kidogo.

Baadaye hata wafanyakazi Wachina walichukuliwa.

Mkoa wa Ufaransa[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1946 Reunion ilipewa cheo cha Mkoa wa Ufaransa, na tangu 1997 imekuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya.

Mkoa wa Reunion ina wilaya (Kifaransa: arrondissements) nne.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Wakazi wanaonyesha historia hii katika mchanganyiko wao wa aina za watu na tamaduni kutoka pande mbalimbali wa dunia.

Sehemu kubwa ya wakazi ni wajukuu wa watumwa au wafanyakazi wasio huru wa zamani wakionyesha tabia za Wahindi, Waafrika na Wachina. Takriban robo ya wakazi ni wa asili ya Ulaya.

Kuna lugha tatu tu ambazo huzungumzwa na wakazi wa Réunion, yaani Kifaransa (lugha rasmi), Kitamil na krioli inayotokana na Kifaransa. Pia kuna wahamiaji kutoka visiwa vya jirani ambao huzungumza lugha za Kichina na za Komori, kama vile Kimaore, Kimwali, Kindzwani na Kingazidja.

Vikundi hivi havikai mbali: kuna mchanganyiko wa kila aina. Wakazi wengi hufuata Ukristo wa Kikatoliki, wengine Uislamu na Uhindu. Kuna pia Waprotestanti.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Réunion kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.