Nenda kwa yaliyomo

Uchapaji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Matbaa ya karne ya 15: Fundi anakaza karatasi, wengi hutazama kurasa zilizochapwa tayari

Uchapaji ni njia ya kunakili maandishi na picha kwa karatasi au loho bapa nyingine, hata kitambaa.

Vitabu na magazeti vinatengenezwa kwa njia ya uchapaji. Hivyo vinaweza kutolewa kirahisi kwa nakala nyingi.

Kabla ya kupatikana kwa uchapaji vitabu, hati na maandiko yote yalinakiliwa kwa mkono pekee. Katika tamaduni mbalimbali waandishi na wanakili walikuwa mabingwa muhimu. Lakini kunakili matini ndefu kama kitabu kulichukua muda mrefu, hata miaka, hivyo vitabu havikupatikana kwa nakala nyingi, pia vilikuwa ghali mno.

Tangu kubuniwa kwa uchapaji maandishi yamepatikana kwa wingi tena kwa bei nafuu. Hii ilisaidia uenezaji wa habari na elimu na kusababisha mapinduzi makuu katika historia ya binadamu.[1][2][3][4]

Mhuri wa mcheduara kutoka Mesopotamia pamoja na nakala yake

Kitangulizi cha uchapaji kilikuwa matumizi ya mihuri. Mifano ya kwanza inajulikana kutoka Mesopotamia ambako mihuri yenye umbo la mcheduara yalikuwa kawaida. Majina, nembo au alama nyingine yichimbwa kwenye uso wa mhuri uliozungushwa baadaye katika kipande cha udongo wa mfinyanzi ulio mbichi. Kipande hiki kiliweza kukaushwa na hata kuchomwa baadaye kama kisahani kidogo ama kwa kitambulisho au uthibitisho wa maandishi juu ya mhuri huu ulioandikwa pia kwa udongo mbichi.

Mihuri mingine ilitokea kwa umbo la nembo au uchoraji mdogo uliowekwa kwenye pete.

Kitabu hiki cha Sutra ya almasi kutoka China ni kati ya kwanza cha kuchapishwa kwa kutumia mhuri wa ubao kwa ukurasa wote

Mhuri wa mbao barani Asia

[hariri | hariri chanzo]
Teknolojia ya Kichina katika Ulaya karne ya 15: Hadithi za Biblia ya picha na matini kidogo ilichongwa katika mihuri ya ubao

Mnamo mwaka 200 KK Wachina walianza kunakili maandishi kwa kutumia mbao. Kila ukurasa, ukiwa pamoja na maandishi yote na picha, uliandaliwa kwa muhuri mmoja. Kwa kazi hii walihitaji sehemu tatu

  • bamba la mbao lenye upande mmoja tambarare kabisa na hapa alama ya mwandishi au picha zilikatwa kwa kuondoa yote ambayo hayakutaka kuonekana, hivyo alama itokeze katika msingi wake.
  • wino yaani kiowevu kama lahamu chenye rangi kinachoweza kupakwa juu ya mhuri na kitakachoonekana vizuri kwenye karatasi/kitambaa tena kwa muda mrefu bila kupotea
  • kitambaa chembamba au karatasi iliyoanza kupatikana katika China kuanzia karne 3 au 2 KK.

Ubao uliwekwa chini, uso juu na wino kupakwa juu ya sehemu zilizotokea juu. Karatasi ikatandikwa juu ya ubao na kupurwa kutoka juu ili wino ifungamiwe kwa karatasi. Baada ya kutoa karatasi maandishi na picha zilionekana kwenye karatasi kama taswira geu ya muhuri. Hii inamaanisha ya kwamba ilikuwa lazima kuchonga maandishi na picha kama taswira geu ili zionekane sawa baada ya kuchapa.

Katika maandishi ya Kichina hakuna herufi za alfabeti, bali kila neno ni alama ya pekee. Matini ndefu kwa Kichina ina maneno na hivyo alama tofauti maelfu hata makumi elfu.

Michapo ya kwanza iliyotengenezwa kwa teknolojia hii ni picha za maua juu ya kitambaa cha hariri zilizochapwa takriban mwaka 200 BK.

Michapo ya kwanza kwenye karatasi zimehifadhiwa kutoka karne ya 7.

Mnamo karne ya 9 teknolojia ilikomaa na kitabu cha kwanza kilichochapishwa kwa njia hii kinachojulikana ni Sutra ya almasi ya mwaka 868, mkusanyo wa maneno na mafundisho ya Buddha. Uzuri wa alama na picha ni dokezo la kwamba watungaji walikuwa na maarifa ya muda mrefu, kwa hiyo si kitabu cha kale zaidi kuchapishwa bali kitabu cha kale kilichohifadhiwa kamili hadi leo.

Tunajua ya kwamba sutra za Buddha mamia elfu zilichapishwa kwa njia hii hadi mwaka 1000 hivi pamoja na mafundisho ya Konfusio. Fundi bora aliweza kuchapisha hadi nakala 2000 ya ukurasa mmoja kila siku.

Mchapaji huu ulienea hadi China, Korea na Vietnam. Baadaye ulipokewa na Waarabu Waislamu na kutoka kwao hadi Ulaya.

Katika nchi ya Korea mafundi walijaribu kufupisha kazi kubwa ya kuchonga ukurasa mzima kwa kuandaa alama mojamoja zilizoweza kuunganishwa baadaye. Walifanya majaribio kwa kutengeneza alama kwa kauri sini, udongo wa kuchomwa (uliovunjika kirahisi), ubao na baadaye pia metali ya shaba. Kuna vitabu kadhaa vilivyochapwa kwa njia hii lakini kwa jumla kazi ilikuwa kubwa mno kutokana na idadi kubwa ya alama katika maandishi ya Kichina. [5] Njia ya kuchonga kurasa zote kwa mbao iliendelea kutumiwa hadi karne ya 19 wakati mfumo wa Kiulaya ulifika Asia ya Mashariki.

Gutenberg na uchapaji kwa herufi za kusogezeka

[hariri | hariri chanzo]
Mkusanyo wa herufi metalia za kusogezeka alizobuni Gutenberg mnamo 1450
Ukurasa wa Biblia ya kwanza iliyochapishwa na Gutenberg uonyeshao utangulizi; rangi nyekundu na mapambo yaliongezwa kwa mkono baada ya uchapaji
Chapa au herufi ya kusogezeka "T" kwa uchapaji

Katika Ulaya teknolojia ya Kichina iliwahi kufika kupitia nchi za Waislamu kuanzia mwaka 1400 hivi. Mwanzoni wasanii walichonga picha za kidini zenye maandishi kidogo. Baadaye waliendelea kuchonga vitabu kamili vyenye picha nyingi na matini kidogo. Vitabu hivi vilishindana na michapo ya kwanza iliyotengenezwa kwa teknolijia ya herufi za kusogezeka iliyoanza mwaka 1450 hivi.

Mwanzilishi wa teknolojia hii mpya alikuwa fundi dhahabu na mfanyabiashara Johannes Gutenberg kutoka mji wa Mainz katika Ujerumani. Alibuni njia sawa jinsi walivyowahi Wachina zamani lakini mwandiko wa Kilatini ulimpa mafanikio makubwa zaidi. Kinyume na mwandiko wa Kichina mwenye alama maelfu mwandiko wa Kilatini una alama chache kwa herufi zake, kama 26 pekee.

Gutenberg alipambana na matatizo mengi akafanya majaribio mengi hadi kufaulu. Metali inadumu kuliko ubao ikamwezesha Gutenberg kuandaa ukurasa na kuuchapisha mara maelfu. Aliweka maandishi kwa kuandaa herufi metalia nyingi alizounganisha kuwa maneno, mistari hadi ukurasa wote.

Kwa kuandaa kalibu kwa kila herufi aliweza kutengeneza herufi nyingi kwa kurudia kumwaga metali ya kuyeyushwa mle na kurudia hatua hii baada ya kutoa herufi zilizipoa kwa kalibu ileile. Alibuni aloi ya plumbi (metali ya risasi), stani na antimoni ambayo yote ni metali zinazoyeyuka kwa joto dogo.

Baada ya kupanga herufi na kuzibana kwa ukurasa mzima aliweza kuchapisha ukurasa mara nyingi jinsi ilivyohitajika. Aliweza pia kufungua mbano wa ukurasa na kutumia herufi kwa kazi nyingine au kutunza ukurasa kwa marudio yaliyotarajiwa.

Kazi ya kwanza ya Gutenberg ilikuwa Biblia (1455 hivi). Imesifiwa kama kazi bora kifundi na kisanii.

Gutenberg alibuni pia wino wenye mafuta uliofaa kwa kazi yake kwa sababu ilidumu kuliko wino wa majimaji wa awali.

Halafu alibuni mashine ya matbaa iliyorahisisha kazi; badala ya kusukuma karatasi juu ya mfano wa ukurasa kwa mkono, mashine ilifanya kazi hii haraka zaidi. Ukurasa uliowahi kuandaliwa kwa herufi katika mistari (Biblia ya Gutenberg ilikuwa na mistari 42 kila ukurasa) ulifungwa katika matbaa upande mmoja, na karatasi ilikweka upande mwingine, halafu pande zote mbili zilikazwa pamoja kwa mwendo wa mashine. Karatasi ilitolewa, mashine ikafunguliwa, wino kupakwa juu ya herufi na karatasi mpya kuwekwa ndani ya mashine. Mashine iliwezesha uchapaji pande zote mbili za karatasi, kazi iliyoshindikana katika mfumo wa zamani.

Usambazaji wa matbaa ya Gutenberg

[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni teknolojia mpya ya Gutenberg ilisambaa polepole. Mahitaji ya pesa yalikuwa mengi, mafundi walihitajika kuandaa kalibu, kuchemsha aloi na kuimwaga katika kalibu, halafu kupanga herufi kwa maneno, mistari na ukurasa wote. Kulikuwa na haja ya kuandaa akiba kubwa ya herufi kwa uchapaji wa kitabu kizima. Mwanzoni bei bado ilikuwa juu hata ililingana na bei ya muswada zilizonakiliwa kwa mkono.

Hata hivyo mafundi wengine walimfuata Gutenberg na sanaa ya uchapaji ilienea Ulaya.

Mnamo 1470 kulikuwa na matbaa 17 na hadi mwaka 1490 idadi iliongezeka kuwa 204. Hadi mwaka 1500 ni 252 matbaa na 62 za hizi zilikuwepo ndani ya Dola Takatifu la Kiroma. Wastani wa kila toleo ulikuwa nakala 150 hadi 250 hivi. Sehemu kubwa ilitolewa kwa lugha ya Kilatini, lakini polepole chapa kilitumiwa pia kwa lugha za kieneo.[6][7][8]

Athari za matbaa ya Gutenberg katika jamii na utamaduni

[hariri | hariri chanzo]

Uchapaji kwa herufi za kusogezeka ulikuwa na athari kubwa katika jamii na utamaduni wa Ulaya halafu duniani kote. Mnamo mwaka 1500, yaani miaka 50 baada ya Gutenberg kuanza kazi, matbaa za Ulaya zilikuwa zimetoa tayari nakala milioni 20 ya miandiko mbalimbali.

Kitabu kilichokuwa jambo haba sana kilianza kupatikana kwa wingi. Elimu kwa njia ya kujisomea iliyopatikana kwa wanafunzi wachache pekee ilisambaa haraka sana. Mawazo na habari zilizowahi kupitishwa kwa mdomo pekee hasa zilichapishwa sasa zikapatikana haraka kwa watu wengi.

Waandishi kadhaa walikuwa mashuhuri haraka. Vitabu vya Eramus wa Rotterdam viliuzwa kwa nakala 750,000 wakati wa maisha yake (1469–1536). Mafundisho ya Martin Luther yalisambazwa haraka, katika miaka michache baina ya 1518 na 1520 pekee nakala 300,000 za vijitabu vyake vilichapishwa na kuuzwa. Bila matbaa matengenezo ya Kiprotestanti yasingepata nguvu iliyokuwa nayo.

Hapo si ajabu kwamba watu wenye mamlaka waliona teknolojia mpya kuwa hatari. Viongozi wa Kanisa Katoliki na wa serikali walijaribu kusimamia na kutawala matumizi ya matbaa. Katika miaka ya kwanza hali ya kisiasa katika Ujerumani na Italia ilikuwa muhimu. Nchi zote mbili zilikuwa sehemu za Dola Takatifu la Kiroma ambalo hali halisi halikuwa na serikali kuu. Miji mingi ndani yake ilijitawala na swali la kuruhusu kazi ya matbaa ilikuwa juu ya serikali ya kila mji. Ndiyo sababu teknolojia ya matbaa ilienea na kukomaa katika nchi hizi mbili mwanzoni na baadaye haikuwezekana kuifuta tena hata katika nchi nyingine. Hata hivyo serikali za nchi kadhaa zilifaulu kulazimisha udhibiti mkali wa vitabu - ila tu nchi nyingine ziliendelea haraka zaidi kwa sababu ilionekana ya kwamba usambazaji wa mawazo ulisaidia sana maendeleo ya uchumi na utamaduni.

Ndiyo pia sababu mojawapo muhimu kwa nchi za Ulaya kufikia hali ya juu duniani na kuzipita nchi za Waislamu na Asia. Hadi wakati wa Gutenberg utamaduni wa Waislamu na nchi za Asia Mashariki uliongoza duniani katika uzalishaji wa bidhaa nyingi, utajiri na mafanikio mengi.

Lakini serikali ya sultani Beyazid II katika Milki ya Osmani mwaka 1485 ilikataza uzalishaji wa vitabu kwa matbaa kwa Waislamu. Amri hiyo ilirudiwa mwaka 1515 na Sultani Selim. [9] Vibali vilitolewa kwa matbaa pekee zilizohudumia jumuiya za wasio Waislamu kama Wayahudi na Wakristo. Kitabu cha kwanza kilichopigwa chapa huko Konstantinopoli kilitolewa mwaka 1497 kwa lugha ya Kiebrania kikiwa na maelezo ya Torati. [10] lakini uchapaji wa herufi za Kiarabu ulipigwa marufuku hadi mwaka 1729.

Matbaa ya kuzunguka na nguvu ya mvuke

[hariri | hariri chanzo]
Matbaa ya Hoe, mnamo 1864

Kimsingi teknolojia ya Gutenberg ilifuatwa na kuendelezwa kwa karne mbili hadi kubuniwa na mashine ya uchapaji ya kuzunguka. Hapo kurasa za chapa zilipangwa juu ya mcheduara uliozunguka na karatasi ilipitishwa chini ya mzunguko wake. Wino ulipakwa mfululizo juu ya herufi na karatasi iliingizwa ama karatasi kwa karatasi au mfululizo kutoka msokoto wa karatasi. Mashine hizi ziliendeshwa kwa nguvu ya mashine ya mvuke, baadaye injini za umeme.

Teknolojia hiyo ilibuniwa na Mjerumani Friedrich Koenig hadi mwaka 1818. Alihamia London akishirikiana na Mwingereza Thomas Bensley. Mwaka 1843 mbinu hiyo iliboreshwa tena na Mwingereza Richard March Hoe. Hii iliwezesha hasa magazeti kutolewa kwa nakala elfuelfu na kwa bei nafuu.

Mabapa ya uchapaji katika mashine kubwa ya offset ya kuchapia gazeti

Uchapaji wa offset na mwisho wa herufi za kusogezeka

[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa karne ya 20 njia mpya ya uchapaji ilibuniwa iliyozidi kuboreshwa na hatimaye kuchukua nafasi ya herufi za kusogezeka. Leo hii vitabu na magazeti mengi kabisa duniani hutengenezwa kwa uchapaji wa offset.

Hapo picha ya ukurasa wote inachomwa kwenye bapa la metali (mara nyingi alumini). Uso wa alumini unaandaliwa ili sehemu zinazotakiwa kuchapwa zipokee wino, lakini sehemu ambazo hazitakiwi kuonekana zinapokea unyevu wa maji na hivyo wino haushiki hapo. Bapa linabanwa katika mashine ya uchapaji, wino kupakwa kwenye bapa kwa kila mzunguko wa mashine, na picha ya ukurasa uliochomwa kwenye metali linanakiliwa kwenye blanketi la mpira linalozunguka pia. Kutoka mpira wino unabanwa juu ya karatasi na picha ya ukurasa ulioandaliwa sasa ni ukurasa uliochapishwa.

Awali picha ya ukurasa ilipigwa kwa kamera halafu kupelekwa kwenye bapa ya uchapaji. Leo hii ukurasa unaandaliwa katika kompyuta na kupelekwa moja kwa moja katika mashine ya uchapaji.

Matbaa za herufi ya kusogezeka bado zinatumiwa mahali pachache na wasanii na mafundi wanaotengeneza michapo ya pekee au ya kisanii.

Uchapaji wa tarakimu

[hariri | hariri chanzo]

Katika miaka ya nyuma uchapaji kwa kutumia printa ndogo pamoja na kompyuta umezidi kuwa muhimu. Gharama za nakala ni ya juu kuliko offset lakini gharama za maandalizi ya chapo ni ndogo.

Printa za leza zinapuliza unga wa wino juu ya karatasi na rangi inashika sehemu ambako printa imeonyesha uga la sumaku kuwa mahali pa herufi au picha, baadaye unga unafungwa imara kwenye karatasi kwa njia ya joto.

Dereva za uchapaji

[hariri | hariri chanzo]

Unapoweka printa kwa tarakilishi yako, huwa kwa kawaida waitishwa kuweka dereva za uchapaji (printer drivers) . Hizo ni programu ambazo zinakusaidia kuwasiliana na mashine ile. Kulingana na maelezo ya Wikipedia ya Kiingereza, dereva za uchapaji hugeuza data ili iwe kati hali au mfumo ambao printa itaweza kupiga chapa bila ya tatizo lolote. Kazi ya dereva hizo ni kuwezesha tarakilishi kupiga chapa bila kuzingatia muundo wa printa yenyewe. Programu hizi huenda ukapewa wakati unanunua mashine yako ya printa au ukapata kwa wavuti za mitandao zinazoshughulika na mambo ya chapa.

  1. Robinson. Andrew 1995. The story of writing. Thames & Hudson, London.
  2. Christin, Anne-Marie (ed) A history of writing. Flammarion, Paris.
  3. Gaur, Albertine 1992. A history of writing. 3rd ed.
  4. Diringer, David 1968. The alphabet: a key to the history of mankind.
  5. Kitabu cha kwanza kilichochapishwa kwa herufi za kusogezeka kilitolewa nchini Korea kinajulikana kwa jina la Jikji.Memory of the World, unesco.org, iliangaliwa Novemba 2009
  6. Idadi kutoka Wittmann, Reinhard: Geschichte des deutschen Buchhandels, S. 27
  7. Lefebre L & Martin H-J. 1990. The coming of the book. new ed, London.
  8. Martin H-J. 1994. The history and power of writing. Chicago.
  9. "Matbaa", katika The Encyclopaedia of Islam, Fascicules 111-112 : Masrah Mawlid, Brill 1989, uk.795, google booksearch 20-04-2015
  10. The First Book Printed in the Ottoman Empire
  • Saunders, Gill; Miles, Rosie (Mei 1, 2006). Prints Now: Directions and Definitions. Victoria and Albert Museum. ISBN 1-85177-480-7.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  • Lafontaine, Gerard S. (1958). Dictionary of Terms Used in the Paper, Printing, and Allied Industries. Toronto: H. Smith Paper Mills. 110 p.
  • Nesbitt, Alexander (1957). The History and Technique of Lettering. Dover Books.
  • Steinberg, S.H. (1996). Five Hundred Years of Printing. London and Newcastle: The British Library and Oak Knoll Press.
  • Gaskell, Philip (1995). A New Introduction to Bibliography. Winchester and Newcastle: St Paul's Bibliographies and Oak Knoll Press.
  • Elizabeth L. Eisenstein, The Printing Press as an Agent of Change, Cambridge University Press, September 1980, Paperback, 832 pages, ISBN 0-521-29955-1
  • Marshall McLuhan, The Gutenberg Galaxy: The Making of Typographic Man (1962) Univ. of Toronto Press (1st ed.); reissued by Routledge & Kegan Paul ISBN 0-7100-1818-5
  • Tam, Pui-Wing The New Paper Trail, The Wall Street Journal Online, February 13, 2006 Pg.R8
  • Tsien, Tsuen-Hsuin (1985). "Paper and Printing". Joseph Needham, Science and Civilisation in China, Chemistry and Chemical Technology. 5 part 1. Cambridge University PressKigezo:Inconsistent citations {{cite journal}}: Cite journal requires |journal= (help); Invalid |ref=harv (help)CS1 maint: postscript (link)
  • Woong-Jin-Wee-In-Jun-Gi No. 11 Jang Young Sil by Baek Sauk Gi. Copyright 1987 Woongjin Publishing Co., Ltd. Pg. 61.

On the effects of Gutenberg's printing

Early printers manuals The classic manual of early hand-press technology is

A somewhat later one, showing 18th century developments is
  • Stower, Caleb (1808). "The Printer's Grammar" (toleo la London: Gregg Press, 1965, reprint). {{cite journal}}: Cite journal requires |journal= (help); Invalid |ref=harv (help)

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: