Nembo ya Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nembo ya Tanzania

Nembo ya Tanzania ni ngao ya askari inayoshikwa na watu wawili.

Ngao ina sehemu nne: juu sehemu ya dhahabu, chini yake bendera ya taifa, halafu sehemu nyekundu na chini kabisa sehemu ya buluu-nyeupe;

a) robo ya juu inaonyesha mwenge wa uhuru juu ya rangi ya dhahabu inayokumbusha juu ya utajiri wa madini ya nchi

b) robo ya pili ni bendera ya Tanzania

c) rangi nyekundu inamaanisha ardhi nyekundu ya Afrika na kilimo kama msingi wa maisha ya watu.

d) milia ya buluu na nyeupe katika robo ya nne inamaanisha mawimbi ya bahari na maziwa kwenye mipaka ya nchi pamoja na bahari inayozunguka Zanzibar kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Juu ya sehemu hizo kuna mkuki na majembe mawili yanayokumbusha juu ya utetezi wa uhuru na umuhimu wa kazi katika ujenzi wa taifa.

Ngao yote imeviringishwa na mapembe ya ndovu yanayomaanisha utajiri wa wanyamapori na hifadhi za taifa.

Ngao inalala juu ya mlima Kilimanjaro ambayo ni mlima mkubwa wa Tanzania.

Watu wawili wanaoshika ngao ni mwanamume na mwanamke kama dalili ya ushirikiano wa jinsia zote mbili taifani. Wanasimama juu ya mpamba na mkarafuu ambayo yote inatoa mazao muhimu ya kibiashara ya Tanzania Bara kwa pamba na Zanzibar kwa karafuu.

Kanda njano ya maandishi chini ya ngao huonyesha kaulimbiu ya taifa "Uhuru na Umoja".

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]