Nenda kwa yaliyomo

Uislamu nchini Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Msikiti mkuu wa Kilwa ni kati ya misikiti ya zamani zaidi Afrika Mashariki.
Uislamu kwa nchi

Uislamu nchini Tanzania ni mojawapo kati ya dini kubwa zaidi.

Idadi ya wafuasi katika Tanzania haijulikani kikamilifu na makadirio yako kati ya theluthi moja[1] na nusu [2] ya Watanzania wote kwa sehemu ya Tanganyika na 97 - 99% ya jumla ya wakazi wa Zanzibar.[3] Takwimu zote zinazohusu dini katika Tanzania zinatia shaka. [4]

Historia

Tanzania, nchi inayounganishwa na eneo la bara linaloitwa Tanganyika na visiwa vya Zanzibar

Ushahidi hasa wa uwepo wa awali wa Uislamu katika Afrika Mashariki ni uanzishwaji wa misikiti katika kisiwa cha Shanga na Pate kwenye machimbo ya dhahabu, fedha na shaba ambapo sarafu zake ziliokotwa zenye tarehe za kuanzia 830 wakati wa machimbo hayo kwenye miaka ya 1980.

Historia ya Uislamu nchini Tanzania imeanza kunako miaka ya 960-1000 AD, wakati Ali ibn al-Hassan Shirazi alikuwa mmoja kati ya watoto saba wa kiume wa Shah wa Shiraz, Uajemi, mama yake akiwa ni mtumwa wa Kihabeshi. Kufuatia kifo cha baba yake, Ali alitimuliwa na kunyimwa urithi na ndugu zake. Kachukua jahazi lake kupitia Hormuz, Ali ibn al-Hassan Shirazi, na kikundi kidogo cha wafuasi wakafanikiwa kufanya mapumziko yao ya kwanza mjini Mogadishu, bohari la kibiashara katika pwani ya Afrika Mashariki.

Miji ya Afrika Mashariki, iliyotaliwa na Usultani wa Kilwa.

Wakaendesha jahazi lao kuelekea pwani ya Afrika, Ali ibn al-Hassan Shirazi kasema anataka kununua kisiwa cha Kilwa kutoka kwa mfalme wa Kibantu aliyeitwa 'Almuli' na kuunganisha sehemu ndogo ya daraja la nchi kavu ambalo linaonekana wakati wa maji madogo. Mfalme yule alikubali kuiuza Kilwa kwa bwana Ali ibn al-Hassan Shirazi kwa nguo zenye rangirangi na hariri kwa lengo la kupendezesha kisiwa hicho. Mara baada ya kuinunua Kilwa, Washirazi wale wakaanza kuchimba daraja mpaka wa nchi kavu, na Kilwa ikawa kisiwa na baadaye yakawa makao makuu ya Usultani wa Kilwa.

Wakati wa umaarufu wake wa nguvu kunako miaka ya 1300-1400, Usultani wa Kilwa ukamiliki au ukadai umiliki wa miji ya bara kama vile Malindi, Sofala na nchi za visiwa kama vile Mombasa, Pemba, Unguja, Mafia, Comoros na Inhambane - kwa lengo la kutawala ambapo sasa hivi hutajwa kama Pwani ya Waswahili.

Jengo ambalo la zamani na bado lipo zima Afrika Mashariki ni Msikiti wa Kizimkazi huko mjini kusini mwa Unguja tangu mwaka 1107. Inaonekana ya kwamba Uislamu ulikuwa unaenea haraka zaidi katika maeneo ya Bahari ya Hindi kunako karne ya 14. Wakati Ibn Battuta katembelea Afrika Mashariki mnamo 1332, ameripoti kujisikia kama yupo nyumbani kwa sababu ya Uislamu ulioenea katika maeneo hayo.

Kawaida ya idadi kubwa ya wakazi wa pwani ilikuwa Waislamu, na Kiarabu ilikuwa lugha ya kufundishia na vilevile ya kibiashara. Bahari yote ya Hindi ilipata kuonekana kama vile bahari ya Kiislamu. Waislamu walishika hatamu katika biashara na uanzishwaji wa makazi katika pwani ya Kusinimashariki mwa Asia, India na Afrika Mashariki.

Uislamu ulienea hasa kwa njia ya shughuli za kibiashara katika pwani ya Afrika Mashariki, si kwa ushindi na uenezi wa mabavu kama jinsi ilivyokuwa huko Kaskazini mwa Afrika, na ikabaki kama pwani ya ajabu kwa muda mrefu.

Wakati wa uvamizi wa mabavu wa Wareno katika maeneo ya pwani yaliyotokea mnamo karne ya 16, Uislamu ulikuwa tayari umeshajikita vya kutosha, karibia kila familia ilikuwa imeungamana na Uarabu, Uajemi, Uhindi na hata kuungana kisiasa na Kusinimashariki mwa Asia na baadhi ya sehemu za kaskazini na mashariki mwa Bahari ya Hindi.

Mwishoni mwa karne ya 17 na mwanzoni mwa karne ya 18, Waislamu wa pwani waliweza kuwatimua Wareno kwa msaada wa Oman. Waomani wakaongeza athira ya kisiasa hadi hapo mwishoni mwa karne ya 19 ambapo Wazungu walipoanza kuwasili katika pwani ya Afrika Mashariki.

Wakati Oman inatawala pwani hiyo kisiasa, uenezi wa Uislamu uliongezeka pia ndani ya Afrika Mashariki. Mawasiliano ya kibiashara na watu wa ndani, hasa Wanyamwezi, na kuanza kupewa umuhimu kwa sehemu kama za Tabora katika maeneo yenye Wanyamwezi na Ujiji katika Ziwa Tanganyika ikawa kitovu kikuu cha uongezaji wa biashara ya utumwa na pembe za ndovu.

Machifu wengi, hata sehemu za Uganda, walisilimu na kuanza kushirikiana na Waislamu wa pwani. Biashara ya utumwa haikusaidia kueneza Uislamu tu, bali pia lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Waswahili.

Kabla ya kuanzishwa kwa Afrika Mashariki ya Kijerumani kunako miaka ya 1880 athira za Waswahili zilikuwa na kikomo, hasa waliishi katika maeneo yao tu waliyoyazoea.

Tazama pia

Marejeo

  1. 35% kufuatana na Pew research center Archived 1 Machi 2019 at the Wayback Machine., iliangaliwa February 2019
  2. 55% kufuatana na tovuti ya Kiislamu muslimpopulation.com, iliangaliwa February 2019
  3. "Vikundi vingi vya kidini vinasita kukadiria demografia ya kidini, lakini viongozi wa dini walio wengi wanakadiria wananchi kuwa 50% Wakristo na 50% Waislamu. Utafiti wa Pew Forum wa 2010 umekadiria Wakristo kuwa takriban 61%, Waislamu 36 % na wafuasi wa dini nyingine kuwa 3%" - ripoti ya Pew Forum kwa mwaka 2012:[1] (Kiingereza)
  4. "Swali la asilimia la Waislamu na Wakristo ni jambo la kisiasa nchini Tanzania kama katika nchi nyingine kadhaa za Afrika. Takwimu zinazotolewa na shirika za Kikristo na Kiislamu zinaonyesha upendeleo haziwezi kutegemewa."Abdulaziz Y. Lodhi and David Westerlund. "African Islam in Tanzania". Iliwekwa mnamo 25 Mei 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link) (Kiingereza)

Viungo vya Nje