Bendera ya Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Bendera ya Tanzania
Bendera ya Zanzibar mwaka 1964
iliyotangulia kuundwa kwa bendera ya Tanzania
Bendera ya Jamhuri ya Tanganyika 1961 hadi 1964 iliyotangulia kuundwa kwa bendera ya Tanzania

Bendera ya Tanzania ni ya mstatili unaokatwa pembe kwa pembe na kanda nyeusi yenye milia za njano (dhahabu) kando.

Pembetatu ya juu ina rangi ya majani, pembetatu ya chini ni ya buluu.

Bendera hii imepatikana tangu 30.06.1964 kutokana na muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Bendera ya Tanganyika ilikuwa na rangi ya kijani ikiwa na kanda nyeusi katikati yenye milia za njano (dhahabu) kando. Buluu imepatikana kutokana na bendera ya Zanzibar ya 1964 ikimaanisha bahari. Hata hivyo toka mwaka 2005, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianza kutumia rasmi bendera ya Zanzibar. Hii ni mara ya kwanza toka kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar kwa kisiwa cha Zanzibar kuwa na bendera yake yenyewe.

Rangi zinasemekana kuwa na maana zifuatazo: Kijani kwa ajili ya mashamba, kilimo na misitu. Kijani ni pia rangi ya bendera ya chama cha TANU kilichokuwa chama tawala tangu uhuru. Buluu kwa ajili ya bahari na visiwa. Nyeusi ni rangi ya watu Waafrika. Njano (dhahabu) inakumbusha juu ya utajiri wa madini.