Tanganyika (nchi)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Bendera ya koloni ya Tanganyika
Bendera ya Jamhuri ya Tanganyika 1961 hadi 1964

Tanganyika ni jina la kihistoria kwa ajili ya sehemu kubwa ya Tanzania isiyo chini ya serikali ya Zanzibar. Mara nyingi huitwa "Tanzania bara" ingawa kuna visiwa pia, hasa Mafia na Kilwa.

Tanganyika ilikuwa koloni ya Uingereza kuanzia 1919 na nchi huru kati ya 1961 hadi 1964. 1964 iliungana na Zanzibar na kuwa sehemu ya Jamhuri ya Maungano ya Tanzania.

Chanzo katika koloni ya Kijerumani[hariri | hariri chanzo]

Maeneo yaliyoitwa baadaye "Tanganyika" yaliunganishwa mara ya kwanza tangu mwaka 1886 kama koloni ya Ujerumani iliyoitwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Kabla ya kufika kwa ukoloni kulikuwa na madola madogo mbalimbali na maeneo madogo ya kikabila. Kanda la pwani pamoja na njia za misafara kuelekea Ziwa Tanganyika vilikuwa chini ya athira ya Usultani wa Zanzibar.

Tangu 1885 Karl Peters kwa niaba ya Shirika la Ukoloni wa Kijerumani (Gesellschaft für Deutsche Kolonisation) alianza kufanya mikataba na watawala wa kienyeji katika maeneo ya Usagara, Nguru, Useguha und Ukami iliyoweka msingi kwa madai yake ya kuchukua utawala mkuu wa maeneo haya. Uenezeaji wa Wajerumani uliendelea hasa baada ya kushinda upinzani katika vita ya Abushiri na vita dhidi ya Wahehe.

Koloni ile ya kijerumani ilikuwa kubwa zaidi kuliko Tanganyika ya baadaye maana ilijumlisha pia maeneo ya Rwanda na Burundi pamoja na sehemu ndogo ya Msumbiji.

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 - 1918) koloni hii ya Kijerumani ilitekwa na jeshi za Uingereza na Ubelgiji. Mkataba wa Versailles wa 1919 ulikuwa na kanuni za kuchukua koloni zote za Ujerumani na kuzikabidhi kwa mataifa washindi wa vita. Sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani iliwekwa chini ya utawala wa Uingereza, kasoro maeneo ya Rwanda na Burundi yaliyokabidhiwa mkononi mwa Ubelgiji.


Tanganyika Territory ya Kiingereza baada ya kuondoka kwa Wajerumani[hariri | hariri chanzo]

1919 sehemu kubwa ya koloni ya Kijerumani ilikabidhiwa rasmi mkononi mwa Uingereza kama eneo lindwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa kulingana na kifungo 22 cha mkataba wa Versailles. Mwaka 1922 Shirikisho la Mataifa lilithebitisha hatua hii na kuamua masharti ya kukabidhi.

Waingereza walihitaji jina jipya kwa ajili ya koloni mpya na tangu Januari 1920 wakaamua kuiita "Tanganyika Territory" kwa kutumia jina la ziwa kubwa upande wa mashariki ya eneo. [1]

Uhuru na Muungano na Zanzibar[hariri | hariri chanzo]

Tanganyika imepata uhuru wake tar. 09.12.1961 (taz.: Historia ya Tanzania).

Mwaka 1964 imeunganishwa na Zanzibar kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leo hii neno "Tanganyika" latumiwa wakati mwingine kutaja sehemu ya Tanzania isiyo Zanzibar.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Linganisha makala "Tanganyika Territory" katika Encyclopedia Britannica, 12th edition, vol 32, uk 676