Jamhuri ya Watu wa Zanzibar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
Bendera ya Zanzibar

Bendera ya Zanzibar
Lugha ya Taifa Kiswahili
Mji Mkuu Zanzibar
Rais Dr. Ali Mohamed Shein
Eneo
km² 2.654
Wakazi
1,303,569
Dini Waislamu takriban 96-99%, Wakristo, Wahindu
Uhuru Kutoka Uingereza
  19.12.1963, Mapinduzi 12.01.1964
Fedha TSh
Visiwa vya Zanzibar (Unguja na Pemba)
Visiwa vya Unguja na Pemba (ramani haionyeshi umbali halisi kati ya visiwa)
Bandari ya Zanzibar

Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ingawa inajitawala katika mambo ya ndani.

Eneo lake ni sawa na funguvisiwa vya Zanzibar iliyopo mbele ya mwambao wa Afrika ya Mashariki karibu na Tanganyika au Tanzania bara. Inajumuisha visiwa vikubwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogovidogo, lakini si kile cha Mafia kilichopo kusini zaidi.

Hadi mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 sehemu hizi zilijulikana kama Usultani wa Zanzibar.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Historia[hariri | hariri chanzo]

Historia inaonyesha kwamba kwa kiasi cha miaka 20,000 kumekuwepo makazi ya binadamu katika visiwa vya Zanzibar.

Visiwa hivyo ni sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria ya ulimwengu wakati Waajemi wafanyabiashara walivigundua na kuvifanya ndiyo makao makuu kwa safari kati ya Mashariki ya Kati, India na Afrika.

Katika karne ya mwanzo BK Zanzibar pamoja na mwambao wa Afrika ya Mashariki vilikuwa katika ufalme wa Saba.

Katika kipindi cha karne ya 3 na ya 4, Wabantu walianza biashara na Waarabu waliokuja Afrika ya Mashariki.

Katika karne ya 7, Waarabu walikuja Zanzibar kibiashara pamoja na kusambaza dini ya Uislamu, Waarabu ndio waliyoipa jina ZANZIBAR kutokana na maneno ya Kiajemi ZINJI BAR yaani sehemu ya Watu Weusi.

Lugha ya Kiswahili imeanza kutumika kiasi cha karne ya 13 ikitokana na mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha za Kiafrika.

Katika karne ya 16 Wareno walikuja Zanzibar lakini utawala wao ulifuatiwa na kutokuwepo utulivu, lakini biashara ya utumwa iliwaweka watu pamoja.

Waarabu kutoka Oman walichukua utawala Zanzibar katika karne ya 17 na Zanzibar ilikuwa makao makuu ya utawala wa Waomani.

Miaka 1820-1870 Zanzibar ilifaidi matunda mazuri ya kiuchumi na maendeleo yaliyosababishwa na utawala wa kisultani na hivyo kupelekea Zanzibar kuwa na mwakilishi nchini Marekani na kupelekea kuenea kwa Dini ya Kiislamu.

Katika karne ya 19 Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Oman, mwaka 1830 Zanzibar ilikuwa inaongoza kwa kilimo cha karafuu, na hiyo kupelekea haja ya watumwa kuongezeka kutumika katika kilimo. Hatimaye watumwa walikuwa 90% za wakazi wote.

Mwaka 1885 kamisheni kutoka Uingereza na Ujerumani iliamua kuigawa Zanzibar kutoka katika utawala wa Kisultani na ndio ulikuwa mwisho wa utawala wa kujitegemea kwa Zanzibar. Mnamo mwaka 1886 sultani alikubali maridhiano hayo.

Mwaka 1890 Zanzibar ilikuwa chini ya uangalizi wa Waingereza rasmi, lakini uchaguzi wa mwanzo ulifanyika mwaka 1957, na miaka iliyofuata kukawepo fujo na machafuko kutoka kwa Waafrika wanaodai uhuru dhidi ya utawala wa kiarabu.

Mwezi Desemba mwaka 1963 Waingereza waliipa uhuru Zanzibar chini ya jumuiya ya madola, na tarehe 12 Januari 1964 Zanzibar ilifanya mapinduzi kujikomboa kutoka katika utawala wa kisultani.

Muda mchache baadaye iliungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA.

Siasa[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla mikoa mitano ya Tanzania imo ndani ya Zanzibar ikiwa mitatu iko Unguja na miwili Pemba.

Zanzibar inatawaliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Zanzibar ina bunge lake linaloitwa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar lenye wabunge 50 wanaochaguliwa kwa muda wa miaka mitano.

Mji mkuu na makao makuu ya serikali ni Jiji la Zanzibar ambalo liko kisiwa cha Unguja.

Mji mkuu wa kisiwa cha Pemba ni Chake Chake.

Jamhuri ya watu wa Zanzibar ilianzishwa baada ya mapinduzi ya 1964 yaliyomaliza Usultani wa Zanzibar.

Rais wa kwanza alikuwa Abeid Amani Karume hadi mwaka 1972.

Alifuatwa na Aboud Jumbe (1972-1984).

Rais wa tatu aliyemfuata alikuwa Ali Hassan Mwinyi (1984-1995) aliyeendelea kuwa pia rais wa Tanzania tangu 1985.

Rais Amani Abeid Karume ambaye ni mwana wa rais wa kwanza na alikuwa mgombea wa CCM alichaguliwa mara ya pili na wananchi wote tarehe 30 Oktoba 2005 katika kura iliyopingwa na chama cha upinzani CUF.

Rais aliyefuata ni Ali Mohamed Shein (2010-2015). Katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 alionekana kushindwa na mpinzani wake, lakini matokeo rasmi ya mwisho hayakutangazwa, ingawa nchi nyingi duniani zilishinikiza ifanywe hivyo.

Watu[hariri | hariri chanzo]

Watu wa Zanzibar ni wa asili mbalimbali, hasa watu wa asili ya Afrika Bantu, yakiwemo makabila ya Wahamidu na Watumbatu; halafu Waasia, awali kutoka India na nchi za Kiarabu.

Idadi ya wakazi wa Zanzibar ilikuwa 1,303,569 mwaka 2012, tarehe ya sensa ya mwisho, iliyoonyesha ongezeko la 3.1% kwa mwaka.

Karibu theluthi mbili ya watu wanaishi katika kisiwa cha Zanzibar (Unguja).

Mkoa wa mjini magharibi ndio wenye idadi kubwa ya wakazi, kiasi cha watu 205,870.

Pemba ina jumla ya makazi sawa. Mji mkubwa ni Chake Chake, ukiwa na idadi ya 19,283, mengine ni Wete na Mkoani.

Dini[hariri | hariri chanzo]

Dini ya Uislamu ina kiasi cha 97% za wananchi wote. Waliobaki ni hasa Wahindu na Wakristo, lakini Wahindu wengi walikimbia nchi au kuuawa wakati wa mapinduzi ya mwaka 1964. Wakristo walikuja wakati wa utawala wa Kireno na ukoloni wa Uingereza.

Kuna misikiti 51, ambayo waadhini wake hugongana wakati wa maombi, pamoja na mahekalu ya Hindu sita na makanisa kadhaa, yakiwemo Kanisa Kuu Katoliki na Kanisa Kuu la Anglikana katika mji wa Zanzibar Stonetown.

Hasa hilo la mwisho ni maarufu kwa sababu lilijengwa mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao.

Hata hivyo makanisa kadhaa yalichomwa moto katika miaka ya mwisho.

Afya[hariri | hariri chanzo]

Upande wa huduma ya afya, vifo vya watoto wachanga bado ni 83 kati ya wazaliwa 1000, na inakadiriwa kuwa utapiamlo huathiri moja katika tatu ya watu wa visiwa.

Matarajio ya maisha wakati wa kuzaliwa ni miaka 48, wakati maambukizi ya VVU / UKIMWI ni madogo sana kwa Zanzibar kuliko Tanzania kwa ujumla (0.6% ya idadi ya watu dhidi ya wastani wa kitaifa wa 8%).

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Uchumi wa Zanzibar unategemea kilimo na utalii. Mazao yanayouzwa nje ni hasa karafuu, basibasi, mdalasini na pilipili.

Uchumi wa Zanzibar ni uchumi duni kabisa ambao mwananchi wa kawaida anaishi chini ya dola moja kwa siku au kutokuwa na uhakika wa kupata chochote.

Wastani wa mapato ya kila mwaka ya US $ 250 na ukweli kwamba karibu nusu ya wakazi wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Lakini kuna tofauti kubwa katika kiwango cha maisha kati ya wakazi wa Pemba na Unguja, tena kati ya wakazi wa mijini na vijijini.

Hilo linatokana na viongozi wa vyama kutoonesha mori katika kutatua matatizo au kuweka mbinu za kuleta maendeleo, badala yake ni kujadili siasa kwa muda mwingi.

Zanzibar ni nchi yenye matumaini katika uchumi lakini, kutokana na migogoro ya kisiasa, imekuwa katika hali duni kabisa, na mabalozi wa Marekani na nchi nyingine walisisitiza mara nyingi umuhimu wa kuwepo ushirikiano katika siasa ili kuiwezesha Zanzibar kuinuka katika hali ya kiuchumi.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]


 
Mikoa ya Tanzania
Bandera Tanzania
Arusha | Dar es Salaam | Dodoma | Geita | Iringa | Kagera | Katavi | Kigoma | Kilimanjaro | Lindi | Manyara | Mara | Mbeya | Morogoro | Mtwara | Mwanza | Njombe | Pemba Kaskazini | Pemba Kusini | Pwani | Rukwa | Ruvuma | Shinyanga | Simiyu | Singida | Songwe | Tabora | Tanga | Unguja Kaskazini | Unguja Kusini | Unguja Mjini Magharibi
Sciences de la terre.svg Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.


Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.