Nenda kwa yaliyomo

Etimolojia ya neno Zanzibar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Etimolojia ya Neno Zanzibar)

Etimolojia ya neno "Zanzibar" inaonyesha ya kuwa ni jina la kale sana. Hakuna hakika kabisa kuhusu asili ya neno hilo. Etimolojia ni elimu ya asili ya maneno na uhusiano yake na maneno mengine.

Asili za Kiarabu na Kiajemi

Zanzibar ina uhusiano na maneno mawili ya Kiarabu. Neno la kwanza ni "zanj- ﺯﻧﺞ" lililomaanisha watu weusi au nchi ya watu weusi[1]. Katika historia kuna kipindi cha vita ya Wazanj waliokuwa watumwa Waafrika katika Irak karibu na mji wa Basra walioasi dhidi ya mabwana wao Waarabu kati ya 869 and 879 BK wakijaribu kujipatia uhuru[2]. Neno "zanj" linaandikwa "zang زنگ" kwa Kiajemi[3] na zamani taarifa nyingi za Wazungu zilitumia umbo la "Zanguebar" kwa matamshi ya Kiajemi wakitaja Zanzibar[4].

Neno la pili ni "bar - ﺑﺮ " linalomaanisha "nchi kavu"[5] - ni asili ya neno la Kiswahili "bara".

Historia ya jina

Bila shaka wakazi asilia walikuwa na jina au majina yao kwa ajili ya mwambao wa Afrika ya Mashariki na visiwa. Lakini hatuna ushuhuda kuhusu majina yale yaliyotumiwa karne nyingi zilizopita. Katika taarifa ya wasafiri na wataalamu Wagiriki na Waarabu tunakuta majina yanayofanana na Zanzibar.

Ptolemaio (aliishi mnamo mwaka 200 BK) alitaja rasi ya "Zingis" au "Zingisa" ((Ζίγγις ή Ζήγγισα) ambayo inaaminiwa kuwa Zanzibar[6]; wasafiri wa baadaye walitumia jina tunalojua kutoka kwa Waarabu, kwa mfano Marco Polo aliyetaja "Zamzibar"[7]. Hatujui kama wale wageni walitumia jina walilopokea kutoka wenyeji.

Azania, Zanj na Zanguebar

Kwa mahitaji yetu inatosha kusema ya kwamba kuna jina la kale kwa ajili ya mwambao wa Afrika ya Mashariki lililowahi kutajwa kwa umbo tofauti katika karne za kale kama vile Zingis, Zingium, Azania, au nchi (=bar) ya „Zanj“ (kiarabu) au ya „Zangi“ (kiajemi). Wajemi na Waarabu wote walitaja pia watu weusi kwa neno hili. „Zangibar“ au „zanjbar“ ni „nchi ya watu weusi“.

Wareno walianza baadaye kutofautisha kati ya bara na kisiwa wakiandika jina la kisiwa mbele ya pwani la „Zanguebar“ kama „Zanzibar“ yaani kwa namna inayolingana zaidi na matamshi ya Kiarabu lakini waliendelea kusema "Zanguebar" wakimaanisha bara.

Tazama pia

Marejeo

  1. Wolbert Smith, An 8th Century Chinese Fragment, in Raunig, Walter (2005). Afrikas Horn: Akten der Ersten Internationalen Littmann-Konferenz 2. bis 5. Mai 2002 in München. Otto Harrassowitz Verlag. p. 130. ISBN 3-447-05175-2. "ancient Arabic geography had quite a fixed pattern in listing the countries from the Red Sea to the Indian Ocean: These are al-Misr (Egypt)—al-Muqurra (or other designations for Nubian kingdoms)—al-Habasha (Abyssinia) - Barbara (Berber, i.e. the Somali Coast) - Zanj (Azania, i.e. the country of the "blacks"). Correspondingly almost all these terms (or as I believe: all of them!) also appear in ancient and medieval Chinese geography."
  2. Zanj Revolt
  3. linganisha زنگي , Reza Nazari, Jalal Daie, Persian - English Dictionary, 2018, ISBN 1547026057 na 9781547026050
  4. Mfano: Miss MANWARING: The Slaves of Zanguebar; and Other Poems, Birmingham 1826
  5. Hans Wehr, Dictionary of Modern Wtitten Arabic, uk. 49 "barr land (as opposed to sea), terra firma, mainland; open country; "
  6. William Vincent, The Commerce and Navigation of the Ancients in the Indian Ocean, Volume 2, London 1807, uk. 147
  7. Vincent uk. 146