Zanj
Zanj (Kiarabu na Kifarsi زنج) ni neno lililotumiwa na waandishi Waislamu wa zamani kutaja watu weusi kutoka Afrika ya Mashariki na pia kwa maana ya kijiografia kutaja eneo la Afrika ya Mashariki.
Zanj kijiografia
[hariri | hariri chanzo]Wanajiografia Waislamu walihesabu pwani takriban kati ya Mogadishu na kisiwa cha Pemba kuwa "Zanj". Kusini yake waliita nchji ya Sofala na kaskazini yake nchi ya Berbera kufuatana na mabandari ya nyakati ziule zilizojulikana kwao.
Uwezekano mkubwa ni neno hili Zanj latokana na jina la kijiografia la awali "Azania" likatumiwa baadaye kutaja hasa kisiwa cha Zanzibar.
Baadaye Zanj imejulikana kama nchi ya Waswahili.
Zanj kama watu
[hariri | hariri chanzo]Waandishi Waarabu wa kale waliita hasa watu weusi kutoka Afrika ya Mashariki kwa jina hili la "Zanj". Waliwatofautiana na Waafrika weusi wengine kama Wanubia (taz. Nubia) au Wahabash (taz. Uhabeshi). Walitazamiwa kuwa watu wenye hali na maendeleo ya duni kulingana na wenyeji wengine wa Afrika iliyojulikana kwa Waarabu.
Watu wa Zanji walipelekwa kama watumwa kaskazini katika nchi za Waislamu.
Watumwa wa Zanj katika Iraki
[hariri | hariri chanzo]Katika historia ya Kiislamu jina la Zanj lajulikana hasa kutokana na watumwa wa Zanj katika Iraki ya kusini.
Katika karne ya 9 BK watumwa wengi Waafrika walipatikana katika mazingira ya mji wa Basra. Waarabu walianza kubadilisha maeneo ya kinamasi katika kusini kuwa mashamba makubwa ya miwa. Maeneo haya yalifunikwa na ganda la chumvi. Chumvi hii ilipaswa kundolewa hadi ardhi yenyewe ilipatikana. Kazi ilifanywa na watumwa weusi waliopaswa pia kuchimba mifereji ya kuondoa maji na kulima.
Watumwa hawa waliitwa kwa ujumla "Zanj" kwa maana walikuwa hasa Waafrika hata kama wengine walikuwa Wanubia au Wahabeshi. Idadi kubwa ya wakazi wa Irak kusini walikuwa watumwa weusi wakati ule.
Uasi wa Zanj 869 - 883
[hariri | hariri chanzo]Maisha ya watumwa yalikuwa ngumu mno wakitendewa vibaya na mabwana na kuanzia Septemba 869 BK walianza kuasi dhidi ya hali hiyo.
Wakiongozwa na Mwajemi Ali bin Muhammad walichukua silaha na kupigania uhuru wao. Huyu Ali alidai ya kwamba alitoka katika ukoo wa Ali ibn Abu Talib akajitangaza kuwa mahdi na kudai ni yeye atakayekamilisha Uislamu wa kweli.
Wazanj walifaulu mara kadhaa kushinda jeshi za Khalifa wa Baghdad wakateka mji wa Basra mwaka 871. Wakajenga miji yao na Mukhtara ikawa mji mkuu wa mahdi.
Mwishowe Baadaye jeshi la khalifa lililoimarishwa kwa vikosi kutoka Misri likafaulu katika mwezi wa Agosti 883 kuteka al-Mukhtara na kumaliza uasi. Ali alikatwa kichwa na Wazanj wasiouawa wakarudishwa utumwani.
Baadaye Waarabu hawakuweka tena watumwa wengi hivi mahali pamoja kwa hofu ya uasi mpya.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Tovuti kuhusu uasi wa Wazanj na Ali Ilihifadhiwa 14 Desemba 2007 kwenye Wayback Machine.