Dini nchini Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Msikiti huko mjini Moshi, Tanzania.

Dini za wananchi wengi wa nchi ya Tanzania ni Uislamu, Ukristo na dini asilia za Afrika (dini za jadi). Nje ya hao wako wachache wanaofuata Uhindu, Usikh na dini nyingine na mara nyingi hawa ni wahamiaji katika nchi au wamezaliwa katika vikundi vyenye asili ya uhamiaji kutoka nje.

Siasa ya serikali na dola ni kutokuwa na dini rasmi. Katiba inatoa uhuru wa dini, na serikali inaheshimu haki hii kwa vitendo.

Dini za jadi[hariri | hariri chanzo]

Hadi vizazi vichache vilivyopita idadi kubwa ya wakazi wa eneo la Tanzania ya leo walifuata dini asilia za Kiafrika.

Wakati wa karne ya 19 Uislamu ulipatikana kwenye pwani hasa katika mazingira ya miji ya Waswahili na pia kwenye vituo vya biashara vya Waswahili kando ya njia ya misafara kuelekea nchi za Maziwa Makuu (Viktoria, Tanganyika n.k.) kutoka pwani.

Tangu katikati ya karne ya 19 wamisionari Wakristo wa kwanza walianza kufika kwenye pwani na kujenga vituo vyao barani.

Wakristo na Waislamu walikuta kote wafuasi wa dini za jadi. Polepole wengi wao walihamia upande wa dini hizo kubwa. Lakini desturi na ibada mbalimbali za jadi ziliendelea kufuatwa na sehemu ya Wakristo na Waislamu wapya hadi leo.

Uislamu katika Tanzania[hariri | hariri chanzo]

Asilimia tisini na saba ya wakazi wa funguvisiwa vya Zanzibar ni Waislamu. Kwa upande wa Tanzania bara, jumuia za Kiislamu huzingatiwa sana katika maeneo ya pwani, na baadhi ya Waislamu wanaoishi katika maeneo ya mijini huko bara.

Kati ya asilimia 80 na 90 ya idadi ya Waislamu nchini ni Sunni wa madhhab ya Shafi'i. Wasunni wachache wenye asili ya Asia ni Wahanbali, kuna pia wafuasi Maliki na Hanbali ambao wana asili ya Yemen.

Washia ni wachache, wengi wao ni wenye asili ya Asia au Uarabuni. Kundi linaloonekana zaidi ni Ismaili au wafuasi wa Aga Khan ambao ni kitengo cha Washia Sabi'a. Kitengo kingine cha Shia hii ni Bohra. Wafuasi wa Shia Ithnasheri (Imami) si wengi, lakini wanapata usaidizi kutoka Uajemi ambako imani yao ni dini rasmi.

Wafuasi wa Ibadiyya wana asili ya Oman.

Kundi la Ahmadiyya liko, wanajitahidi kupata waumini wapya lakini bila mafanikio makubwa.

Ukristo katika Tanzania[hariri | hariri chanzo]

Idadi ya madhehebu ya Kikristo inajumlisha Kanisa Katoliki, Waprotestanti wa aina mbalimbali (Walutheri,Wapentekoste, Waanglikana, Wamoravian, Wasabato, Wameno, Kanisa Jipya la Kitume n.k.), Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki wachache, mbali ya Wamormoni na Mashahidi wa Yehova ambao mara nyingi hawahesabiwi na madhehebu hayo kuwa Wakristo kwa sababu ya kutosadiki umungu wa Yesu.

Dini nyingine[hariri | hariri chanzo]

Kuna Watanzania wanaofuata Uhindu na Usikh, hasa wageni na raia wenye asili ya Asia.

Imani ya Baha'i nayo imeanzishwa katika maeneo kadhaa ya nchi.

Takwimu ya dini[hariri | hariri chanzo]

Sensa ya 1967[hariri | hariri chanzo]

Takwimu ya dini nchini Tanzania kwa sasa haipatikani kwa sababu maswali kuhusu dini yaliondolewa na serikali katika sensa baada ya mwaka 1967. Sensa ile ya tarehe 27 Agosti ilihesabu wafuasi wa dini za jadi kuwa 34.3%, Wakristo 33.5% na Waislamu 31.4%, mbali na wengineo 0.8%.[1]

Namba zenye athira ya kisiasa[hariri | hariri chanzo]

Tangu mwaka ule swali la takwimu ya kidini Tanzania limejadiliwa sana inaonekana ni swali lenye uzito wa kisiasa pamoja na upande wake wa kitaalamu.

Kwa miaka mingi makadirio ya kawaida yalikuwa Watanzania ni theluthi 1 wafuasi wa dini za jadi, theluthi 1 Waislamu na theluthi 1 Wakristo.[2]

Lakini ni wazi ya kwamba dadi ya wafuasi wa dini za jadi imeendelea kupungua. Baadhi ya viongozi na wanaelimu-jamii wanakadiria kwamba jumuia za Kikristo na Kiislamu zipo sawa tu kwa ukubwa, zote huhesabiwa kiasi cha asilimia 30 hadi 40 kwa idadi ya wakazi, na waliosalia ni waumini wa imani zingine, dini za jadi, na wale wasio na dini kabisa.

Lakini wataalamu wengine wanasema uwiano huo unashikiliwa kisiasa kwa sababu uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu ni jambo la siasa ya taifa kwa hiyo makadirio yanaelekea kutaja uwiano sawa kati ya pande hizi mbili.[3]

Mifano ya makadirio mbalimbali[hariri | hariri chanzo]

Kwa hiyo namba zote kuhusu takwimu ya dini nchini Tanzania ni makadirio tu hakuna namba za kutegemea. Vyanzo vinavyotaja namba vinatofautiana sana mara nyingi kufuatana dini ya wahariri.

  • "World Christian Encyclopedia" (toleo la pili, Oxford 2001) imekadiria kwa mwaka 2000 Wakristo kuwa 50.4 % (Wakatoliki 24.7%, Waprotestanti mbalimbali 16.5%, Waanglikana 7.9%, wasio na madhehebu maalumu 3.5%, madhehebu huru 1.9%, madhehebu yasiyokubali imani ya msingi ya Wakristo wengine wote 0.1%, wenye kufuata madhehebu mawili kwa wakati mmoja 4.2%), Waislamu 31.8%, wafuasi wa dini za jadi 16.1% na wengineo 1.8%. Pia imetabiria kwa mwaka 2025 uwiano kuwa 56.1, 32.8, 8.9 na 2.1%, na kwamba kufikia mwaka 2050 Wakristo na Waislamu watakuwa karibu 65 na 35% kati ya wakazi wa nchi.
  • Takwimu zinazoonyeshwa na Waislamu hudai kundi kubwa la Watanzania kuwa Waislamu wakiwa na asilimia 50 - 60 za watu wa nchi [5]
  • Kuna shirika za Kiislamu zinazotabiri Tanzania itakuwa nchi ya Waislamu wengi mnamo mwaka 2020 [6]

Pande zote zinarejea takwimu za kuongezeka za watu katika maeneo fulani wakiongeza makadirio yao juu ya matokeo kwenye namba za kidini. [7]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. International Religious Freedom Report 2007: Tanzania. United States Bureau of Democracy, Human Rights and Labor (14 Septemba 2007). This article incorporates text from this source, which is in the public domain.
  2. linganisha ukurasa wa gazeti The Citizen kuhusu Tanzania - Country Profile - TANZANIA - RELIGIONS http://www.thecitizen.co.tz/about-tanzania.html?start=8 Archived 24 Desemba 2010 at the Wayback Machine.
  3. Kuna taarifa zisizothebitshwa juu ya ripoti moja ya serikali ya mwaka 1990, ambayo haikusambazwa zaidi, ilionyesha Ukristo unavyozidi kuongezeka kasi kuliko Uislamu, kwa kupata wafuasi hasa kutoka dini za jadi ambazo kwa wakati huo zilikuwa zinaongoza tu katika mkoa wa Shinyanga. Mkoa wa Iringa ulionekana kuongoza kwa wingi wa Wakristo (91%) na uchache wa Waislamu (2%), mbali na wafuasi wa dini za jadi kuwa 7%. Mikoa ya Kiprotestanti ilikuwa hasa Mbeya na Dodoma. Wakatoliki walikuwa wengi hasa katika mkoa wa Rukwa na Kagera.
  4. [1]
  5. linganisha Tovuti ya Muslim Population Worldwide inadai asilimia 55 Waislamu mwaka 2008 na M. Amir Ali Muslim Population Statistics: Tanzania 50% = watu 18,722,696 na Lodi, Nordic Journal of African Studies 3(1): 88–98 (1994)- uk. 91
  6. Nakala iliyohifadhiwa. Jalada kutoka ya awali juu ya 2020-02-17. Iliwekwa mnamo 2010-12-06.
  7. Mfano wa makadirio ya wataalamu wanoona Wakristo mbele ni hivi Sababu ya ongezeko la kasi la Wakristo linatokana na wafuasi wa dini wa jadi, na hasa watoto wao, kuelekea zaidi Ukristo. Pia makabila ya pwani na ya jijini kuzaa kidogo kuliko wakazi wa mikoa ya bara, hasa Tanzania Magharibi ambayo katika sensa ya mwaka 2002 ilionyesha ongezeko kubwa zaidi.