Mapambano ya uhuru Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika ni yale yaliyofanyika katika Tanzania bara ya leo dhidi ya ukoloni.
Tanganyika, kama nchi yenye mipaka maalumu, ilianzishwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, ilipokuwa chini ya mamlaka ya Uingereza.
Kabla ya hapo ilikuwa sehemu ya koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, pamoja na nchi za leo Rwanda na Burundi.
Baada ya kuvamiwa na majeshi ya wapinzani wa Ujerumani wakati wa vita, Shirikisho la Mataifa lilikabidhi sehemu kubwa ya makoloni ya Kijerumani kwa Uingereza na nchi nyingine kama "eneo la kudhaminiwa". Serikali ya Uingereza iliamua kutumia jina "Tanganyika" kufuatana na jina la ziwa kubwa kwenye mashariki ya eneo.
Upinzani wa awali dhidi ya ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Kuanzishwa kwa koloni ya Kijerumani kulitekelezwa mara kwa mara dhidi ya upinzani wa jamii za wenyeji, wakati mwingine pia kwa msaada wa wenyeji. Jamii waliopinga kwa nguvu uenezi wa utawala wa Kikoloni walikuwa wakazi wa pwani katika vita ya Abushiri, Wahehe chini ya Mkwawa na pia sehemu za Wachagga. Upinzani huo wa awali ulikuwa na tabia ya kikabila. Lakini manmo 1905 makabila ya kusini-mashariki waliungana katika Vita ya Majimaji.
Hapo serikali ya Kijerumani ilijaribu kupunguza ukali wa utawala wake na kwa jumla koloni iliona kipindi cha utulivu hadi mwaka 1914.
Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ilileta balaa ya uharibifu na njaa iliyofuatwa na epidemiki ya homa ya mafua ya 1918. Hivyo mwisho wa utawala wa Kijerumani na kuanzishwa kwa utawala wa Kiingereza hakukuona upinzani kwa silaha tena ilhali watu walitulia kujenga maisha upya.
Kujipanga kwa maslahi ya wananchi
[hariri | hariri chanzo]Katika kuendeleza mapambano yao dhidi ya utawala wa Waingereza, wananchi walijiunga katika makundi mbalimbali ya kimaslahi ambapo wakulima wa mazao makuu ya biashara waliunda vyama vya ushirika kupigania bei nzuri ya mazao na unafuu wa pembejeo za kilimo. Vyama mashuhuri vilikuwa ni pamoja na KNPA ambacho baadae kilijulikana kama KNCU (Kilimanjaro Native Cooperative Union), VFCU (Victoria Federation of Cooperative union), Bukoba Bahaya Union, NgoniMatengo (NGQMAT) na Umoja wa Meru.
Vyama hivyo vilipata mafanikio ya kutosha katika kuongeza maslahi ya wanachama wao lakini havikupata uhuru wa kupanga na kuendesha shughuli zao bila kuingiliwa. Baadhi yake, vikiwemo KNCU na Bukoba Bahaya Union, pia vilijitahidi kuinua hali ya maisha ya wanachama wake kwa kujenga shule za sekondari na kuwalipia watoto wa wanachama gharama za masomo nchini, Ulaya na Marekani.
Wakati wa harakati za kupigania uhuru vyama hivi vilitoa mchango mkubwa wa kisiasa na hatimaye kuwa sehemu ya chama cha ukombozi cha TANU (Tanganyika African National Union).
Kundi lingine lilikuwa la vyama vya wafanyakazi: vyama mashuhuri vilikuwa vyama vya wafanyakazi wa bandari na reli. Mwaka 1955 umoja mkubwa zaidi wa TFL (Tanganyika Federation of Labour) ulianzishwa.
Aliyekuwa waziri mkuu wa pili wa Tanganyika huru na baadaye makamu wa pili wa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Rashid Mfaume Kawawa, ndiye aliyeongoza harakati hizo kama katibu mkuu.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mapambano ya uhuru Tanganyika kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |