Hamed bin Mohammed el Murjebi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Tippu Tip)
Hamed bin Mohammed el Murjebi

Picha ya Hamed bin Mohammed el Marjebi (Tippu Tip), House of Wonders Museum, Mji Mkongwe, Zanzibar
Amekufa 14 Juni 1905
Nchi Tanzania
Majina mengine 'Tippu Tip
Kazi yake Mwandishi


Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Hamad bin Muhammad bin Juma bin Rajab el Murjebi (amejulikana zaidi kwa jina la Tippu Tip; 183714 Juni 1905) alikuwa mfanyabiashara mashuhuri katika Afrika ya Mashariki na ya Kati wakati wa karne ya 19.

Alikutana na wapelelezi mashuhuri kama David Livingstone, Henry Morton Stanley na Hermann von Wissmann.

Kwa miaka kadhaa alikuwa gavana wa Kongo ya Mashariki kwa niaba ya mfalme wa Ubelgiji.

Alitunga tawasifu kuhusu maisha yake.

Mfanyabiashara

Baba yake alikuwa mfanyabiashara Mwarabu Muhammed bin Juma, mama yake Bint Habib bin Bushir, alikuwa Mwarabu wa tabaka la watawala toka Muscat.

Hamed aliingia katika shughuli za biashara tangu umri wa miaka 12 akafaulu katika biashara ya misafara kati ya Zanzibar na Kongo.

Akiwa na umri mdogo, Hamad aliongoza kundi la wanaume 100 kwenda Afrika ya Kati kutafuta watumwa na pembe za ndovu.[1] Baada ya kuvamia maeneo mengi alirudi Zanzibar kuimarisha vyanzo vyake na kukusanya watu wa kumsaidia ili arudi bara.[2] Hapa alipokea jina la Tippu Tip. Kwa mujibu wake mwenyewe, jina hilo lilitokana na mlio wa bunduki yake wa 'tiptip. [3]

Alipanga misafara ya mahamali waelfu akipeleka bidhaa kutoka Bagamoyo kupitia Tabora hadi Ujiji kwa Ziwa Tanganyika na ndani ya Kongo. Bidhaa alizobeba alizitumia kujipatia pembe za ndovu na watumwa; watumwa walisaidia kubeba pembe za ndovu njia ya kurudi hadi pwani. Hamed alitajirika sana. Athira yake ilipanuka katika Kongo ya Mashariki hadi alitawala eneo kubwa sana.

Kukutana na wapelelezi Wazungu

Hamed akapata jina huko Ulaya kwa sababu alikutana na wasafiri na wapelelezi Wazungu kama David Livingstone, Veney Cameron, Henry Morton Stanley, Eduard Schnitzer (Emin Pascha), Hermann von Wissmann na Wilhelm Junker ambao mara nyingi walipata misaada muhimu kutoka kwake.[4] Kati ya mwaka 1884 na 1887 alikuwa mtu mwenye mamlaka katika sehemu kubwa za Mashariki ya Kongo.

Gavana wa Mfalme wa Ubelgiji

Wabelgiji walipoanza kujenga ukoloni wao Kongo walimkuta kama mtawala wa Kongo ya Mashariki wakapatana naye na kumpa cheo cha gavana ya Mkoa wa Chutes Stanley ("maporomoko ya Stanley", leo Kisangani) mwaka 1887 alichoshika kwa miaka michache.

Mwanzoni mwa 1887, Stanley aliwasili Zanzibar na kumtaka Hamad awe gavana wa Wilaya ya Stanley Falls kwenye Dola Huru la Kongo, iliyokuwa koloni binafsi la mfalme wa Ubelgiji. Mfalme Leopold II wa Ubelgiji na Sultani Barghash bin Said wa Zanzibar walikubaliana na tarehe 24 Februari 1887, Hamad alikubali. Wakati huohuo alikubali kuongoza safari za Stanley ili kwenda kumuokoa Mjerumani Emin Pasha (E. Schnitzer), gavana wa Kiosmani wa Equatoria (eneo la Misri ya Kiosmani, Sudan Kusini ya leo).

Nyumba ya Tippu Tip in Mji Mkongwe, Zanzibar.

Kurudi Zanzibar

Mabadiliko ya ukoloni yaliharibu biashara yake akarudi Zanzibar 1890/1891 alipobaki bila misafara mipya hadi kifo chake mwaka 1905.

Hamed amejipatia nafasi katika historia ya Afrika ya Mashariki kwa kuandika yeye mwenyewe tawasifu au kumbukumbu ya maisha yake. Katika lugha ya Kiswahili ndio mfano wa kwanza wa tawasifu. Pia ni mfano wa pekee wa kumbukumbu ya kimaandishi ya matokeo ya siku zile zisizoandikwa na Mzungu lakini na mwenyeji. Aliandika kwa lugha ya Kiswahili akitumia mwandiko wa Kiarabu. Mfasiri katika Ukonsuli wa Ujerumani kwenye kisiwa, Heinrich Brode alinakili muswada wake kwa herufi za Kilatini na kuongeza tafsiri ya Kijerumani iliyochapishwa huko Berlin katika sehemu mbili mwaka 1902 na 1903 [5], [6] .

Brode alitumia kazi hiyo kutunga kitabu chake juu ya Hamed kilichochapishwa mwaka 1905 na kutafsiriwa kwa Kiingereza mwaka 1907[7].

Vita ya Waarabu katika Kongo na kuporomoka wa urithi wa Tippu Tip

Baada ya kuondoka kwake Hemed katika Kongo, vita ya Waarabu katika Kongo ilianza. Waarabu na Waswahili wa Kongo Mashariki walipigana na serikali ya kikoloni ya Dola Huru la Kongo ilhali pande zote mbili zilitumia askari Waafrika wengi walioongozwa na viongozi wa nje, ama Waarabu /Waswahili au Wazungu.

Tippu Tip alipoondoka Kongo, uwezo wa Dola Huru la kikoloni la Mfalme Leopold bado ulikuwa hafifu sana katika sehemu za mashariki. Mamlaka ilikuwa mkononi mwa Waarabu au Waswahili waliofanya biashara ya pembe za ndovu na watumwa kwenda Zanzibar. Kati yao walikuwa Sefu bin Hamed, mwana wa Tippu Tip, na mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Rumaliza katika maeneo upande wa magharibi ya Ziwa Tanganyika.

Mwaka 1892 Sefu bin Hamed alishambulia Wabelgiji waliofanya biashara ya pembe za ndovu iliyokuwa hatari kwa biashara ya Waswahili. Serikali ya koloni ya Dola Huru la Kongo ilituma kikosi chini ya kamanda Francis Dhanis kwenda sehemu za mashariki. Dhanis alifaulu mapema kushawishi kiongozi Mwafrika Ngongo Lutete aliyewahi kushirikiana na Sefu ahamie upande wake. Jeshi lake lilikuwa na silaha bora na nidhamu bora kati ya askari wake, likafaulu kumshinda Sefu mara kadhaa hadi ifo chake kwenye Oktoba 1893. Kutoka hapa Dhanis aliendelea kumshambulia Rumaliza na hatimaye kumlazimisha akimbie katika eneo la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Kwa njia hii Wabelgiji walifaulu kuvunja nguvu ya Waarabu na Waswahili katika Kongo Mashariki. Kisiasa hakuna kitu kilichobaki na juhudi za Hemed bin Mohammed el Murjebi kujenga milki yake katika Kongo, ila tu kiutamaduni Hemed na wenzake walifaulu kueneza lugha ya Kiswahili katika sehemu zile.

Kifo

Hamad alifariki kutokana na ugonjwa wa malaria tarehe 13 Juni 1905 katika nyumba yake kwenye Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Jina lake linajulikana kama mfano wa mabaya ya biashara ya watumwa iliyoharibu maeneo makubwa huko Kongo kabla ya mwanzo wa ukoloni. Yeye mwenyewe aliona watumwa ni sehemu tu ya biashara yake akitajirika hasa na biashara ya pembe za ndovu.

Marejeo

  1. Hinde 1897, p. 8
  2. Hinde 1897, p. 9
  3. Ferant, Leda (1972). Tippu Tip and the East African slave trade. Hamilton. p. 42. Retrieved 24 November 2017. For two months Tippu Tip's caravan camped in Chungu's territory and punitive parties were sent out looking for Samu and his men. According to Tippu Tip this was the time he was given his nick-name because guns went 'tiptip, in a manner too terrible to listen to'. 
  4. Stanley, H. M., 1899, Through the Dark Continent, London: G. Newnes, Vol. One (ISBN 0486256677), Vol. Two (ISBN 0486256685)
  5. Sehemu ya Kwanza online hapa, pdf uk. 676 (Kiswahili-Kijerumani); Autobiographie des Arabers Schech Hamed bin Muhammed el Murjebi, genannt Tippu Tip. Transscribirt und übersetzt von Dr. II. Brode. Mittheilungen des Seminars für Orientalische Sprachen zu Berlin Dritte Abtheilung V 1902, Afrikanische Studien 1902,uk 175
  6. Sehemu ya Pili online hapa, pdf uk. 560 (Kiswahili-Kijerumani); Autobiographie des Arabers Schech Hamed bin Muhammed el Murjebi, genannt Tippu Tip (Schluss). Transscribirt und übersetzt von Dr. II. Brode. Mittheilungen des Seminars für Orientalische Sprachen zu Berlin Dritte Abtheilung VI 1903 Afrikanische Studien, uk 1
  7. Tippoo Tib, The story of his career in Central Africa, narrated from his own accounts by Dr. Heinrich Brode, London, Edward Arnold 1907, online hapa

Vyanzo

  • Bennett, Norman Robert. Arab vs. European: Diplomacy and war in Nineteenth-Century East Central Africa. New York: Africana Publishing Company, 1986.
  • Brode, Heinrich. Tippoo Tib: The Story of His Career in Zanzibar & Central Africa. Translated by H. Havelock with preface by Sir Charles Elliot. London: Arnold, 1907 (Online version).
  • Edgerton, Robert B. (2002). The Troubled Heart of Africa: A History of the Congo. New York: St. Martin's Press. ISBN 0-312-30486-2.
  • Hinde, Sidney Langford (1897). The Fall of the Congo Arabs. 
  • Maisha ya Hamed bin Mohammed el Murjebi yaani Tippu Tip kwa maneno yake mwenyewe, kimefasiriwa na W.H. Whitely (toleo la Kiswahili - Kiingereza), East Africa Literature Bureau 1974
  • Roland Oliver; Roland Anthony Oliver; Anthony Atmore (2004). Africa since 1800. Cambridge University Press. ISBN 0-521-83615-8. 
  • Sheriff, Abdul. Slaves, Spices & Ivory in Zanzibar: Integration of an East African Commercial Empire into the World Economy, 1770-1873. London, Nairobi, Tanzania, Athens,OH: James Currey, Heinemann Kenya, Tanzania Publishing House, Ohio University Press, 1987.