Tundu Antiphas Mughwai Lissu
Tundu Antiphas Mughwai Lissu (alizaliwa Mahambe, wilaya ya Ikungi, Tanzania, 20 Januari 1968) ni mwanasiasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania.
Tundu Lissu alizaliwa na wakulima. Alisoma Shule ya Sekondari Ilboru ya Arusha na kuhitimu mwaka 1983, halafu alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.[1].
Alichaguliwa kuendelea kuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi wa mwaka 2015[2].
Tungu Lissu husifika kwa tabia yake kuikosoa serikali kwa kiasi kikubwa akitumia taarifa na takwimu nyingi. Kumekuwa na matatizo chungunzima yaliyowekwa wazi na mbunge huyu na alishawahi kusema hatanyamaza kuikosoa serikali, labda afe.
Alisema hivyo kwa sababu mara kadhaa alikamatwa na polisi na kutiwa ndani hadi alipokubaliwa kuweka dhamana.
Mnamo tarehe 7 Septemba 2017 majira ya saa saba mchana alipigwa risasi 38, lakini 16 tu katika hizo ndizo zilizompata katika sehemu za mkononi, miguuni na tumboni.[3][4] Tukio hilo lilitokea nyumbani kwake Dodoma Area D. Baada ya kupata matibabu ya awali, Lissu alisafirishwa hadi jijini Nairobi kwa matibabu zaidi.[5]
Baada ya hapo alisafirishwa hadi Ubelgiji alipoendelea kufanyiwa upasuaji hadi kufikia operesheni 22.
Tukio hili limelaaniwa vikali na viongozi na watu mashuhuri mbalimbali nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na Rais John Magufuli aliyeandika kwa masikitiko katika ukurasa wake wa Twitter kwa kulaani tendo hilo lisilo la kibinadamu.[6]
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF anayetambuliwa na vyombo vya dola, Profesa Ibrahim Lipumba, naye ameonesha kukerwa na tukio la kutandikwa risasi kwa Lissu. Kwa uchungu, Lipumba amevitaka vyombo vya dola kuwatafuta wahusika wa tukio na wapelekwe katika vyombo vya sheria mara moja.[7]
Hata hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na upelelezi.
Lissu alikaa Ubelgiji kwa mayibabu lakini pia kwa wasiwasi kuhusu usalama wake nchini Tanzania hadi mwaka 2020 alirudi kwenye mwishoni mwa Julai ili agombee urais.
Januari 2023, Tundu Lissu alitangaza kuwa amerejea Tanzania baada ya miaka mitano ya uhamishoni nchini Ubelgiji.[1].
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Hon. Tundu Antiphas Mughwai Lissu Imeandaliwa Agosti 2024
- ↑ Tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaImeandaliwa Mei 2017
- ↑ Habari ya Lissu katika BBC mnamo 7 Septemba, 2017.
- ↑ Tundu Lissu apigwa risasi Dodoma Gazeti la Mwananchi
- ↑ Lissu apelekwa Nairobi kwa matibabu - Mwananchi mnamo 7-09-17.
- ↑ Nimepokea kwa masikitiko taarifa za Lissu Rais John Pombe Magufuli mnamo 7-09-2017.
- ↑ Lipumba akerwa Lissu kupigwa risasi - Gazeti la Mwananchi mnamo 07-09-2017.
Makala hiyo kuhusu mwanasiasa wa Tanzania bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |