Takwimu
Takwimu (kutoka Kiarabu; kwa Kiingereza: statistics) ni elimu ya data.
Data ni habari juu ya watu, nchi, uchumi, matukio au hali ya vitu mbalimbali. Takwimu inakusanya na kuangalia habari nyingi za aina hiyo ikijaribu kuzitafsiri katika namba zinazoweza kulinganishwa.
Baadaye takwimu inajaribu kutambua utaratibu ndani ya namba hizo ambazo mara zinadokeza sababu gani namba ni vile zilivyo.
Mfano wa faida ya takwimu
[hariri | hariri chanzo]Kwa mfano, inawezekana kukusanya habari juu ya tiba ya ugonjwa kwa kutumia dawa fulani. Inawezekana kuuliza ndugu na majirani watakaosema kama wamesikia nafuu baada ya kutumia dawa hii au nyingine. Mara nyingi maoni yatatofautiana. Kwa kukusanya habari za watu wengi wanaotumia dawa mbalimbali inawezekana kupata picha ni dawa gani yenye uwezo zaidi.
Kwa njia hii imeonekana ya kwamba madawa ya uchawi hayana uwezo wa kutibu UKIMWI. Inawezekana pia kuona tofauti kati ya madawa yanayouzwa madukani. Inaonekana pia kwamba dawa fulani ya mitishamba ina matokeo mazuri tofauti na nyingine, na hapa mara nyingi utafiti wa kisayansi wa undani zaidi hufuata.
Kukusanya data kuhusu matumizi ya madawa, kuzipanga na kufanya tathmini ni mfano wa kazi ya takwimu.
Kwa hiyo takwimu ni elimu ya kukusanya data, kuzipanga, kuzitathmini na kutoa maelezo juu yake.
Aina za takwimu
[hariri | hariri chanzo]Takwimu zinafanywa kuhusu mambo mengi. Mifano michache ni pamoja na:
- Takwimu ni tawi la hisabati; hapo mbinu tofautitofauti za kupanga na kutathmini data zinachunguzwa pamoja na nafasi za welekeo ambazo ni muhimu kwa kubashiri kutokana na data zilizopo.
- Takwimu za kitaifa au takwimu zinazojumlisha data zinazokusanywa na ofisi za serikali; katika nchi za Kenya na Tanzania kuna "National Bureau of Statistics"
- Takwimu ya wananchi ni chombo muhimu katika demografia inayoonyesha jinsi gani idadi ya watu katika nchi na sehemu zake inabadilika pamoja na mabadiliko ya umri, jinsia n.k. Mbinu kuu ya fani hii ni sensa.
- Takwimu ya afya na magonjwa inachunguza hali ya afya kati ya wananchi na uenezji wa magonjwa
- Takwimu ya uchumi inakusanya na kuchunguza habari za uchumi wa nchi au matawi yake
- Takwimu katika sayansi kama fizikia, meteorolojia, kemia au biolojia inakusanya data ya vipimo na majaribio na hivyo kupata habari za undani juu ya fani hizo pamoja na ubashiri wa majaribio mapya.
- Takwimu ya bima ni muhimu kwa kukadiria gharama zinazoweza kutokea na hivyo bei iliyo lazima kwa huduma za bima
Historia ya takwimu
[hariri | hariri chanzo]Mwanzo
[hariri | hariri chanzo]Vyanzo vya takwimu vilitokea pale ambako watu fulani walikuwa na mali zaidi, jinsi walivyoweza kukumbuka wakiagiza kuorodhesha mali hii. Orodha za aina hiyo zilikuwa muhimu kwa watawala wa madola ya kale walioshika kumbukumbu ya mavuno katika sehemu mbalimbali ya milki ili kuwa na msingi kwa madai ya kodi kutoka kwa wananchi wa sehemu fulani.
Takwimu yenyewe ilianza na sensa yaani hesabu ya watu katika milki au mji. Sensa za kwanza zinajulikana kutoka Misri ya Kale (mnamo mwaka 2700 KK)[1], China ya Kale (mnamo mwaka 2000 KK), mji wa Mari katika Mesopotamia (mnamo 1700 KK).
Mji wa Athens katika Ugiriki ya Kale ilihesabu wananchi[2], ilishika orodha ya watu waliohamia mjini na kuondoka pamoja na orodha ya bidhaa zilizoingizwa katika eneo la mji.
Roma ya Kale ilikuwa na cheo cha censor aliyechaguliwa na wananchi na kazi yake ilikuwa kutunga na kutunza orodha za wakazi pamoja na mali yao na kuamulia kiwango cha kodi ambacho kila mmoja alidaiwa. Hesabu hizo zilikuwa pia muhimu kwa mipango ya kijeshi watawala walipotaka kujua kuna wanaume wangapi kati ya wananchi wanaofaa kuitwa jeshini wakati wa vita.
Kati ya sensa mashuhuri duniani ni sensa katika Dola la Roma wakati wa Kaisari Augusto inayotajwa katika Injili ya Luka kwenye Agano Jipya la Biblia ya Kikristo [3]
Juhudi za kuhesabu idadi ya watu, mali na bidhaa ziliendelea katika sehemu nyingi za dunia. Lakini sensa ya aina hii katika eneo kubwa daima ni kazi kubwa pia yenye gharama inayohitaji mfumo imara wa serikali katika eneo husika.
Takwimu ya kisasa
[hariri | hariri chanzo]Mwanzo wa takwimu ya kisasa unatazamwa kutokea wakati wanahisabati walianza makadirio kutokana na namba zilizoweza kukusanywa kirahisi zaidi na kuzirejea kwa wananchi kwa jumla.
Hapa mara nyingi makadirio ya Mwingereza John Graunt yanatajwa kama hatua ya kwanza aliyetumia orodha ya vifo mjini London kukadiria idadi ya wakazi wa mji huu mnamo mwaka 1662. Alijua ya kwamba kila mwaka mjini London kulikuwa na takriban mazishi 13,000. Kutokana na orodha hizi aliona ya kwamba kila mwaka kulikuwa na vifo 3 kati ya familia 11. Alichungulia vitabu vya ubatizo na mazishi ya makanisa ya London akaona kila familia kwa wastani ilikuwa na watu 8. Kutokana na namba hizi alikadiria jumla ya wakazi wa London kuwa takriban 384,000 wakati wake.
Wanahisabati wengine katika Ulaya walivutwa na makadirio yake Graunt na wataalamu kama Blaise Pascal na Christiaan Huygens waliweka misingi ya nadharia ya welekeo inayoruhusu kupanga idadi kubwa ya data na kutoa tathmini kutoka hapa.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Ian Shaw: The Oxford History of Ancient Egypt. Oxford University Press, 19. Februar 2004, ISBN 978-0-19-280458-7, uk. 4–5.
- ↑ Missiakoulis, Spyros (2010). "Cecrops, King of Athens: the First (?) Recorded Population Census in History". International Statistical Review. 78 (3): 413–418. doi:10.1111/j.1751-5823.2010.00124.x.
- ↑ Leo hii wataalamu wa historia walio wengi wanaona haikuwa sensa ya dola lote maana kakuna taarifa nyingine juu ya sensa ya milki yote; kwa hiyo inaaminiwa Luka mwinjili alirejea sensa ya kieneo labda katika Syria ya Kiroma.