Edward Ngoyai Lowassa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Edward Lowassa)
Edward Ngoyai Lowassa
Mbunge
Bunge la Tanzania
Jimbo la uchaguzi Monduli (Arusha)
Tarehe ya kuzaliwa 26 Agosti 1953
Tarehe ya kifo 10 Februari 2024
Chama CCM (tangu 01/03/19)
Tar. ya kuingia bunge tangu 1990
Alirudishwa mwaka 2005
Waziri Mkuu wa Tanzania
Alingia ofisini 2005
Alitanguliwa na Frederick Sumaye
Dini Mkristo
Elimu yake Chuo Kikuu
Digrii anazoshika MA (Development Studies), University of Bath (Uing.)
Kazi mwanasiasa


Edward Ngoyayi Lowassa (26 Agosti 1953 - 10 Februari 2024) alikuwa mwanasiasa nchini Tanzania.

Alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 30 Desemba 2005 akajiuzulu tarehe 7 Februari 2008 kwa kashfa ya Richmond. Mwaka 2015 aligombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Maisha

Lowassa alikuwa mbunge wa Monduli katika Mkoa wa Arusha, alipotokea.

Alisoma shahada ya kwanza katika tamthilia kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, halafu shahada ya pili katika sayansi ya maendeleo ya jamii Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.

Nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika

Lowassa alikuwa mwanasiasa mkongwe mwenye uzoefu mbalimbali katika siasa za nchini Tanzania, kwa kuwa aliwahi kushika vyeo mbalimbali katika serikali kama vile:

  • Waziri mdogo wa mazingira na mapambano dhidi ya umaskini katika ofisi ya Makamu wa Rais (1988-2000)
  • Mkurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (1989-1990)
  • Waziri mdogo wa haki na mambo ya bunge katika ofisi ya Makamu wa Rais (1990-1993)
  • Mbunge wa Monduli tangu 1990
  • Katika Disemba 2005 alipitishwa na bunge kuwa waziri mkuu wa Tanzania

Uchaguzi mkuu 1995

Mwaka 1995 Edward Lowassa aliamua kuingia katika mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM. Wakati huo aliombwa na Umoja wa Vijana kupitia kikao cha baraza kuu la Taifa achukue fomu akiwa miongoni mwa wana CCM wanne ambao vijana waliamini wataweza kulisaidia taifa kupiga hatua za haraka kuelekea maendeleo endelevu, wengine wakiwa Salim Ahmed Salim, Laurance Gama na jaji mstaafu Mark Bomani.

Katika hatua ya kuchagua majina 3 kati ya majina 11 yaliyoomba nafasi hiyo, Lowassa akawa hakupendekezwa, lakini hakununa wala kususa bali aliamini kuwa mwanamapinduzi mwenzie Jakaya Mrisho Kikwete ataweza kutekeleza dhamira aliyokuwa nayo ya kuwaletea Watanzania maendeleo, hivyo alirudi kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana wa CCM ambao walihoji kwa nini ameenguliwa, na yeye kwa utii mkubwa kwa CCM aliwataka vijana na viongozi wengine waheshimu maamuzi ya chama na kumuunga mkono Kikwete. Ikumbukwe kuwa mwana-CCM mwingine aliyekuwa anakubalika kwa umma aliondoka mapema CCM kwa sababu ndogo tu ya kubadilishiwa wizara na kuamua kwenda chama cha NCCR-Mageuzi ambako aligombea urais kwa chama hicho na kuleta upinzani mkubwa.

Yapo maneno ya baadhi ya wanasiasa kwamba kutoteuliwa kugombea kwa Lowassa kulitokana na kuonekana anamiliki fedha nyingi akiwa na muda mfupi kwenye utumishi wa umma, lakini pia inasemekana kuwa wale waliohoji kukatwa kwa jina lake kwenye kikao cha Halmashauri kuu ya Taifa, majibu yalikuwa, CCM iliamua kupeleka majina matatu kwenye mkutano mkuu ili wachague moja katika uwakilishi huo wa majina: walipenda apatikane mtu mzima mmoja, mwenye umri wa kati mmoja na kijana mmoja, watu hao ni mzee David Msuya ambaye ni mtu mzima, Benjamin Mkapa ambaye umri wake ulikuwa wa kati na kijana ambaye ni Jakaya Kikwete.

Lakini maneno hayo ya baadhi ya wanasiasa hayakuishia hapo: wakadai baada ya Rais Mkapa kuchaguliwa, hakumteua Lowassa kwa kuwa aliagizwa na Mwalimu Nyerere asimteue mpaka achunguzwe kama uwezo kiasi wa fedha alionao unatokana na mapato halali, kama si halali asimteue. Mwaka 1997 Rais Mkapa akamteua Lowassa kuwa Waziri wa nchi, ofisi ya makamu wa Rais mazingira.

Sakata la Richmond

Tarehe 7 Februari 2008 Lowassa alijiuzulu baada ya kushtakiwa kuwa ameshiriki katika kashfa ya Richmond. Kamati ya bunge iliwahi kuchungulia mkataba baina ya kampuni ya TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company LLC kutoka Houston, Texas. Kamati ya wabunge watano chini ya mwenyekiti Harrison Mwakyembe ikaona mkataba huo ulikuwa mdanganyifu. Richmond ilipewa kazi ya kutengeneza megawati 100 za umeme kila siku baada ya ukame wa mwaka 2006 uliopunguza uwezo wa TANESCO kutoa umeme nchini kutokana na mitambo yake ya umememaji. Lakini mitambo ya dharura ya Richmond ilichelewa kufika nchini, pia haikufanya kazi jinsi ilivyotakiwa [1]. Hata hivyo serikali ikaendelea kulipa zaidi ya dola za Marekani 100,000 kila siku.

Kamati ya bunge ikaona ya kwamba Lowassa alishawishi azimio kuhusu mkataba na Richmond kwa kupuuza masharti ya kisheria na kinyume cha ushauri wa TANESCO. Baada ya kujadiliwa kwa taarifa ya kamati kwenye bunge, Lowassa akajiuzulu pamoja na Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagima waliowahi kuwa mawaziri wa nishati.[2]

Hata hivyo Lowassa alikanusha kuwa na hatia yoyote.

Mgombea urais mwaka 2015

Mwaka 2014 Lowassa alisimamishwa na kamati kuu ya CCM baada ya kushtakiwa ya kwamba aliwahi kuanzisha kampeni ya kuwa mgombea wa urais kabla ya kipindi kilichokubaliwa na chama hicho.

Mwezi Mei 2015 hatimaye aliweza kuanzisha kampeni yake rasmi lakini kamati kuu ya CCM ilimwondoa katika orodha ya majina yaliyopelekwa kwa uteuzi huo ndani ya chama.

Lowassa akaondoka katika CCM na tarehe 28 Julai 2015 alijunga rasmi na chama cha upinzani cha CHADEMA.

Siku chache baadaye aliteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya CHADEMA mnamo Oktoba 2015. Kadiri ya Tume ya Uchaguzi alishindwa kwa kupata asilimia 39.97 za kura zote na mgombea wa CCM John Pombe Magufuli aliyepata 58.46%.[3]

Baada ya 2015

Lowassa aliendelea kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chadema. Mwaka 2016 alitangaza ya kwamba hawezi kurudi kamwe CCM [4].

Kwenye Januari 2018 aliwahi kuwa na mazungumzo marefu na rais Magufuli. Tarehe 1 Machi 2019 alirudi kwenye chama chake cha awali CCM[5].

Viungo vya nje

  1. Taarifa ya ubalozi wa Marekai katika Tanzania, Date: 2008 February 9, 05:46 , kupitia wikileaks
  2. Mehler, Andreas; Melber, Henning; Van Walraven, Klaas (2009). Africa Yearbook: Politics, Economy and Society South of the Sahara in 2008. BRILL. p. 376. ISBN 90-04-17811-2.
  3. Jedwali la matokeo ya uchaguzi wa rais, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, tangazo rasmi, kupitia web archive, iliangaliwa Machi 2019
  4. Lowassa: Kuitwa gamba, fisadi kuliniondoa CCM, gazeti la Mwananchi, 6 Februari 2016, iliangaliwa Machi 2019
  5. Veteran Tanzanian politician Edward Lowassa returns to CCM, taarifa ya gazeti The East Africa, tar 1 Machi 2019