Nenda kwa yaliyomo

Tamthilia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ukumbi wa maonyesho Colon.
Mchoro unaonyesha namna watu wanavyocheza tamthilia.

Tamthilia (pia: Tamthiliya au Tamthilia-Mchezo, kutoka neno la Kiarabu تمثیل ) ni moja kati ya sehemu za utunzi wa hadithi au fasihi simulizi (ngano au hadithi) ambayo mara nyingi tunaona katika kumbi za maonyesho au kupitia televisheni, au tunasikia kupitia redio.

Tamthilia au mchezo mara nyingi huwa mazungumzo baina ya watu, na kwa kawaida huwa mchezo hatuutazami katika televisheni tu, bali hata kuna watu wengine hufuatilia kwa kupitia maandiko yenye tamthiliya hizo na kuzielewa vyema.

Watu tunaowaona wanafanya tamthilia ni waigizaji; katika ukumbi wa maonyesho husimama juu ya jukwaa na kuanza kutoa burudani yao huku watu wakiwaangalia (watazamaji) wanaweza wakawaona vyema kabisa.

Mwongozaji anawasaidia waigizaji kufanya kazi zao vyema, au anawaeleza namna ya mchezo jinsi unavyotakiwa kuchezwa.

Sifa bainifu ya tamthilia[hariri | hariri chanzo]

Tamthilia ya leo hugawanyika katika sehemu/matendo ambayo yana vijisehemu (maonyesho). Kila onyesho huendeleza hoja kuu za tendo. Muungano wa matendo hujenga mtiririko wa maudhui na fani kwa kubainisha wahusika, mtindo na dhamira.

Tamthilia huhusisha mijadala na mazungumzo kati ya wahusika wawili na zaidi. Mazungumzo katika tamthilia huwa mafupi na yanajenga dhamira ya msanii mtunzi. Tofauti na mazungumzo ya kawaida, katika tamthilia huwa ya kasi na hufuata mkondo maalumu wa mawazo tofauti na yale ya kawaida ambayo hubadili mikondo.

Mijadala katika tamthilia hujenga migogoro ambayo ndiyo tegemeo la uigizaji. Wahusika wa tamthilia hujidhihirisha kwa maneno, mawazo na matendo yao na pia kwa jinsi mtunzi anavyowasawiri. Sifa zao hujionyesha jukwaani; kwa mfano: unene, utajiri, ufukara, ujasiri, woga n.k.

Tamthilia hutegemea sana ukamilifu wa mandhari jukwaani ili hadhira iiamini. Mapambo ya jukwaani sharti yalingane na dhamira ili yafanikishe uigizaji. Mapambo na mandhari: taa, giza, kicheko, kilio, kinaya, sauti mbalimbali hupatia tamthilia uhai kila inapoigizwa.

Jukwaa ndio uwanja wa kudhihirisha tamthilia nzima. Mpangilio wa jukwaa hufanikisha au kutatiza uigizaji. huweza kurahisisha/kutatiza uelewa wa tamthilia. Waigizaji wakinyimwa nafasi ya kuigiza kutokana na udogo wa jukwaa huenda uigizaji ukakwamishwa. Uteuzi, mpangilio na matumizi ya jukwaa ni sehemu muhimu katika uigizaji, ili kuwezesha ufanisi wa uigizaji, waandishi wa tamthilia hutoa mielekezo na maagizo.

Hadhira na waigizaji huletwa pamoja na uigiazaji. bila hadhira uigizaji haujakamilika, mwandishi huwa amelenga watu wanaokusanyika katika thieta ili wajionee maigizo. Hadhira huwa ni kiwakilishi cha jamii pana ambayo msanii hulenga hisia zao. Baadhi ya tamthilia hushirikisha hadhira kwenye dhana ya kando, kimatendo kama vile kuimba, kijibu maswali. Hadhira hujumuishwa kihisia kila mara. Bila hadhira, ari na hamasa ya uigizaji itakuwa haipo.

Brecht akichangia nadharia ya ukengeushi alisema kuna pengo kati ya hadhira na waigizaji. Kila kundi liko katika dunia yake; kwa mfano waigizaji hutenda mambo yao kama kwamba hakuna anayewaona au kuwasikia.

Tamthilia ya leo imebadilika kiwakati na kiutunzi ndiposa hadhira na wagizaji wakawa katika ulimwengu sawia na kushirikiana. Tamthilia huhusishwa na uigizaji. Tamthilia ya leo hujumuisha nyimbo, ngoma, hadithi, uzungumzi nafsia, kuchanganya ndimi n.k.

Nafasi ya uigizaji hutegemea wahusika. Licha ya kuwa viumbe wa msanii, wao huongozwa na fasiri za mwelekezi wa uigizaji na kufahamu kwao wanachoigiza na uigizaji wenyewe. Tamthilia moja inaweza kuigizwa tofautitofauti kwa kutegemea:

 • Wakati
 • Mazingira
 • Uelekezi

Ndiposa Pickening na Hoeper wakasema tamthilia ni kiuzi tu ilhali maigizo hubadilika na wakati.

Muundo wa tamthilia ya kisasa umeazima kutoka tamthilia za Kiingereza ambazo ziliathiriwa na tamthilia ya Ugiriki. Muundo huo huwa na sehemu tano:

 1. Utangulizi: Maelezo ya miktadha ya matukio hutolewa. Maelezo yataonyesha migogoro ambayo inajengeka. Hutanguliza wahusika na huandhaya matukio.
 2. Utata: Hapa mambo huvurugika, hali hubadilika. Ukinzani ukadhihirika wazi.
 3. Kipeo: Ni kilele cha ukinzani, kihisia na kimatendo, mambo ya kuonyesha hisia kama mapigano, ugomvi, utengano, msimamo thabiti n.k. Masimulizi fulani na kufuata mkondo mpya wa mabadiliko ili kupata suluhisho.
 4. Msuko: Kipindi cha utulivu, migogoro hutulia.
 5. Matokeo: Suluhisho hutarajiwa au hupatikana. Hutoa nafasi ya kuendeleza dhamira ya mabadiliko.
 6. Mbinu za uelekezaji: Ufasili wa tamthilia. Kuhusisha matini zote kitamthilia (maneno ya wahusika na maelekezi ya jukwaa). Waigizaji wafaao, wakati ufaao na eneo la drama. Uelewa wa kiwango cha uigizaji na jamii. Ushirikiano wa matendo na maneno. Kuifahamu hadhira yake. Mandhari ya kuaminika. Mkabala mwema baina ya mwelekezi na waigizaji. Kutofautisha lugha ya kidrama na mazungumzo halisia. Kutathmini athari za uigizaji kwa hadhira.

Aina za tamthilia[hariri | hariri chanzo]

Kuna aina nyingi za tamthilia, lakini kuna michezo ambayo inaonekana kuwa muhimu kupita yote:

 1. Trejidia - huu ni mchezo wa huzuni tu, kwa sababu ya mikosi na nuksi, kwa sababu ya mbabe hayuko ngangali, au kwa sababu za kimila au imani fulani.
 2. Komedia - huu ni tamthilia chekeshi: hukusudiwa kuonyesha vituko vya kuchekesha na unaishia na vichekesho tu. Vitu vilivyo katika mchezo huu ni vya kuchekesha; unavunja mbavu. Ujenzi wa wahusika si muhimu, matukio hayawekewi sababu maalumu za kuridhisha. Msuko wake hauna utungamano mzuri. Tamthilia nyingi zenye mgongano wa lugha huwa chekeshi.
 3. Domestiki drama au Igizo la kawaida - huu ni mchezo wa maisha ya kawaida, familia na marafiki.
 4. Trejikomedia - huu ni mchezo mchanganyiko wa vitu vyote viwili, vichekesho na huzuni halikadhalika.
 5. Melodrama - huu mara nyingi ni vichekesho na unaishia na furaha. Ndani yake kunakuwa na maadui - watu wabaya - lakini mbabe hushinda. Msisimko wake unakuwa mkali sana. Ni kinyume cha trejidia/tanzia. Mwisho/hatima ya mhusika huwa ni ushindi. Matokeo yake huwa ya kusisimua hasa kwa hadhira.
 6. Simboliki - huu unahusu fikra za uigizaji au mchezo. Watu wachezao katika mchezo si muhimu. Simboliki pia waweza kuitwa kwa jina la kitaalamu kama "expressionistic". Ni kuhusiana zaidi na waongozaji na watunzi wakiwa wanatoa fikra zao katika mchanganuo tofauti.
 7. Tamthiliya za kihistoria - mhusika anaibua matukio ya kihistoria; k.m. Rise and Fall of Idi Amin Dada.
 8. Tamthiliya tatizo - zinaangazia tatizo linalowakumba wanajamii wakati fulani, kwa mfano, ufisadi. Mifano ya tamthiliya hizi ni k.v. Kigogo (Pauline Kea) na Mstahiki Meya (Timothy Arege).

Mabadiliko na maendeleo ya tamthiliya za Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

Kwa kutumia muundo wa Shakespeare, waandishi waliandika tamthiliya kwa lugha ya Kiswahili na zilihusisha masuala ya Kiafrika. Wakati wa ukoloni, drama ilikuwa kwa ajili ya Wazungu na Waafrika wachache waliojua Kizungu. Baadaye, waandishi wazalendo waliotaka kuwasiliana na umma, iliwabidi watunge tamthiliya yao kwa lugha ya Kiswahili. Baadaye, licha ya tamthiliya kuzingatia matumizi ya lugha ya Kiswahili, walianza kuzitazama, kuchunguza na kuzifanyia majaribio.

Tamthiliya za awali, k.v. Wakati Ukuta na Heshima Yangu, hazikuwa na utohozi wa matumizi ya fani za sanaa za maonyesho ya jadi. Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1960, na mwanzoni mwa miaka ya 1970, tamthiliya zilianza kuonyesha mwelekeo mpya. Pia, falsafa na imani za Kiafrika kabla ya ubepari zilianza kudidimia kidogo.

Historia ya tamthiliya za Kiswahili[hariri | hariri chanzo]

Syango na Mazrui (1992) walipanga historia ya tamthiliya za Kiswahili katika vipindi vinne:

Tamthiliya za kwanza kuchapishwa zilikuwa kati ya miaka 1950-1960[hariri | hariri chanzo]

Baadhi ya tamthiliya hizo ni kama vile: Nakupenda Lakini... (Henry Kuria, 1957), Afadhali Mchawi, na pia Mgeni Karibu (Graham Hyslop, 1957), Nimelogwa Nisiwe na Mpenzi (Ngugi 1961). Zilizungumzia masuala ya jamii chache zikiwa za upelelezi. Tamthiliya nyingine zilizungumzia masuala ya kutovunja sheria zikirejelea wakoloni. Pia zilibainisha mgongano baina ya jamii za makabila tofautitofauti. Nyingi zilikuwa na lengo za burudani. Pia ziliendelea kudunisha hadhi ya Waafrika ingawa ni za Kiswahili. Mwaka 1960 ndipo Little Theatres zilianzishwa kwa burudani ya Wazungu.

Tamthiliya baada ya 1960[hariri | hariri chanzo]

Tamthiliya hizi zilijaa maudhui ya kimapenzi, migogoro ya kitamaduni, maudhui ya kikoloni. Tamthiliya hizi ni kama vile: Wakati Ukuta na Kwenye Ukingo wa Thim (Hussein Ibrahim), Pambo (Peninah Muhando), na Tazama Mbele (Kitsau Jay).

Tamthiliya za mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970[hariri | hariri chanzo]

Maudhui yalikuwa: masuala ya ukoloni, historia ya Waafrika katika mapinduzi, haki za wanyonge. Kwa mfano: Mzalendo Kimathi (Ngugi), Mkwawa wa Hehe.

Tamthiliya za kuanzia 1970[hariri | hariri chanzo]

Zilikuwa na mwamko mpya. Zilichunguza jamii za Afrika Mashariki kwa mkondo mpya. Zilizungumzia: ukoloni mamboleo, uongozi, siasa na matatizo mengine kama vile ufisadi, unyanyasaji, uporaji n.k. Kwa mfano; Aliyeonja Pepo (Faruk Topan), Mashetani (Ibrahim Hussein), Kilio cha Haki (Alamin Mazrui).

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya fasihi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tamthilia kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.