Mikindani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwa maana nyingine, tazama Mikindani (Mombasa).


Mikindani
Nchi Tanzania
Mkoa Mtwara
Hori la Mikindani
Mikindani mjini, kanisa na ngazi ya kuelekea bomani (sasa Boma Hotel)

Mikindani ni mji wa kihistoria kwenye pwani ya Bahari Hindi katika Tanzania ya kusini-mashariki. Iko karibu na mji wa Mtwara na pamoja na mji huo mkubwa umeunganishwa kiutawala katika halmashauri ya manisipaa ya pamoja. Idadi ya wakazi ni mnamo 10,000.

Jina la mji limetokana na "minazi mikinda" ambayo ni jina la miti michanga aina ya mnazi.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Inaaminiwa ya kwamba hori ya Mikindani kulikuwa na makazi ya watu tangu karne ya 1 BK na kabla ya mwaka 1000 kulikuwa na makazi ya kudumu. Wakazi walilima mtama, walivua samaki na kukusanya wanyama kama kome na chaza. Walishiriki pia katika biashara ya Bahari Hindi; waliweza kupata vyungo na bidhaa nyingine kutoka ng'ambo lakini hasa walifinyanga wenyewe.[1].

Kuanzia mwaka 1100 hivi waliacha kupokea bidhaa kutoka nje; inawezekana uchumi wao ulibadilika kutokana na upanuzi wa nguvu ya Kilwa iliyopo kilomita 200 upande wa kaskazini ambao ulipanuka katika karne zile. Tofauti na miji mingine ya Waswahili wa karne hizo watu wa Mikindani hawakuanza kujenga nyumba za mawe. Hata hivyo, makazi yaliongezeka: kuna dalili ya upanuzi wa biashara na sehemu za bara ikiwa njia za biashara hiyo zilifuata mabonde ya mito inayoishia baharini. [2].

Mnamo mwaka 1500 hivi, baada ya kuporomoka kwa nguvu ya Kilwa, kuna dalili kwamba uchumi wa nje uliimarika tena. Misikiti ya kwanza ilipatikana baada ya mwaka 1500 na idadi ya bidhaa kutoka ng'ambo iliongezeka.

Wakati wa karne za 18 na 19 Mikindani iliendelea kuwa mji kabisa wenye nyumba za mawe kwa sababu sasa ilishiriki katika biashara ya watumwa na ya pembe za ndovu, pamoja na miji mingi ya wakati ule kama vile Bagamoyo na Kilwa Kivinje[3].

Mji ulikua wakati wafanyabiashara Waarabu kutoka Omani walipoanza kujenga nyumba zao hapa wakitumia bandari asilia. Hasa kuanzia karne ya 16 Mikindani ilikuwa bandari muhimu upande wa kusini wa Kilwa ikawa mwanzo wa biashara ya misafara ya watumwa na ndovu. Mji ulianza kuonekana kwenye ramani za bahari tangu mwaka 1796. Kiutawala mji ulikuwa chini ya liwali wa Sultani ya Zanzibar. Tarehe 24 Machi 1866 David Livingstone alifika mjini akianza hapa safari yake ya mwisho.

Mnamo 1870 Mikindani ilivamiwa na makabila ya barani ikajengwa upya. Waarabu na Waswahili walilima mashamba ya michikichi na mpira.

Ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa Agosti 1888 Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki ilikodi pwani ya Tanganyika kutoka Sultani wa Zanzibar. Ukali wa wakala wake ulisababisha mara moja vita ya Abushiri ambamo wenyeji wa pwani walijaribu kuwafukuza Wajerumani. Mapigano yalifikia pwani ya kusini katika Desemba 1888 na wakala Wajerumani walipaswa kukimbia. Wajerumani waliporudi mwaka 1890 viongozi wa mji walijisalimisha bila mapigano, hivyo mji ukahifadhiwa ukawa makao ya mtawala wa kikoloni.

Mikindani ilikuwa sehemu ya koloni jipya la Kijerumani katika Afrika ya Mashariki ikiwa ni sehemu ya Mkoa wa Lindi; ilikuwa na ofisi ndogo ya mkoa pamoja na kituo cha forodha. Iliunganishwa pia na waya ya simu kutoka Dar es Salaam. Mwanaisimu Mjerumani Carl Velten alikusanya habari za historia ya Mikindani iliyoandikwa na Salim bin Rashid bin Mohammed Elbarwani kutoka Lindi[4]. Kabla ya mwisho wa utawala wa Kijerumani kulikuwa na meli 48 zilizofika bandarini pamoja na jahazi 264 (mwaka 1908); idadi ya jahazi ilizidi kupungua kuwa 147 pekee mwaka 1912. Biashara yake ilikuwa hasa katani, ufuta na mpira[5]

Mwaka 1916 wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia majengo karibu na bandari yaliharibiwa kutokana na uvamizi wa Waingereza. Baada ya vita Mikindani ilikuwa makao makuu ya wilaya ya Mikindani chini ya Waingereza; hao walihamisha utawala wa wilaya kwenda Mtwara mwaka 1947 walipoanzisha mji huu mpya.

Uhuru[hariri | hariri chanzo]

Mikindani imeunganishwa kiutawala na Mtwara. Kwa heshima ya mji wa kihistoria jina la Mikindani imehifadhiwa katika jina la manisipaa ya pamoja kuwa "Mtwara-Mikindani".

Jengo la boma la Kijerumani limekuwa hoteli nzuri inayotembelewa na watalii.

Picha za Mikindani[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Pawlowicz, uk. 3f
  2. Pawlowicz, uk. 12-13
  3. Alpers, E. 1975. Ivory and slaves: changing pattern of international trade in East Central Africa to the later 19th century. Berkeley: University of California Press
  4. Habari za Mikindani; katika Velten, C.: Prosa und Poesie der Suaheli; Berlin 1907; online hapa uk. 273
  5. Kamusi ya Koloni za Kijerumani (1920), makala Mkindani

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mtwara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mikindani kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.