Eneo la kudhaminiwa
Eneo la kudhaminiwa lilikuwa eneo lililokabidhiwa na umma wa kimataifa mikononi mwa nchi iliyotakiwa kulisimamia. Katika karne ya 20 maeneo ya kudhaminiwa yalikuwa aina ya pekee ya ukoloni. Utawala wa mkoloni ulitekelezwa rasmi kwa niaba ya nchi huru zote za Dunia. Hali hii ya pekee ilikuwa na umuhimu hasa wakati wa uhuru wa nchi hizo.
Maeneo hayo yalianzishwa mwaka 1919 katika Mkataba wa Versailles uliounda Shirikisho la Mataifa lililokuwa mtangulizi wa Umoja wa Mataifa wa leo.
Nchi tawala za maeneo ya kuadhiminiwa zilipokea maeneo yale chini ya masharti ya katiba ya Shirikisho la Mataifa zikatakiwa kutoa taarifa za kila mwaka na kuyaandaa kwa uhuru wa kisiasa.
Hali halisi maeneo ya kudhaminiwa yalitendewa kama makoloni ya kawaida kwa miaka mingi.
Baada ya mwaka 1945 Shirikisho la Mataifa lilikwisha na usimamizi mkuu ulipitia mikononi mwa Umoja wa Mataifa. Wakati ule jina la maeneo ya kudhaminiwa kwa lugha ya Kiingereza likabadilishwa, kutoka "mandate" au "mandated territory" kuwa "trust territory", lakini maana ya maneno haya ni yaleyale.
Maeneo yote yamepata uhuru. Mfano wa pekee ni Israel na Palestina ambako hadi leo hakuna utaratibu wa kudumu katika eneo la kudhaminiwa la zamani.
Kuanzishwa kwa maeneo ya kudhaminiwa
[hariri | hariri chanzo]Maeneo ya kudhaminiwa yalianzishwa mwaka 1919 katika Mkataba wa Versailles. Mkataba uliweka utaratibu mpya wa kimataifa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Nchi zilizoshindwa katika vita hii, hasa Dola la Ujerumani, Austria-Hungaria na Milki ya Osmani (Uturuki) zilipotea maeneo makubwa. Sehemu ya maeneo haya yalipewa nafasi ya kuwa nchi huru moja kwa moja, kwa mfano nchi kama Hungaria, Romania au Chekoslovakia.
Mengine yalitazamwa kutokuwa bado tayari kwa uhuru, hasa makoloni ya Ujerumani na maeneo ya Waarabu chini ya Milki ya Osmani. Yaligawiwa kwa jumla kati ya Uingereza na Ufaransa; Ubelgiji na Japani zilipata pia maeneo madogo.
Katiba ya Shirikisho la Mataifa juu ya maeneo ya kudhaminiwa
[hariri | hariri chanzo]Kifungu 22 cha katiba ya Shirikisho la Mataifa lilieleza:
"Makoloni na maeneo ambayo, kutokana na matokeo ya vita iliyopita, si tena chini ya mataifa yaliyowahi kuyatawala, yakikaliwa na mataifa ambayo si bado tayari kujisimamia katika mazingira magumu ya dunia ya kisasa yatatazamiwa kuwa udhamini wa ustaarabu wa kimataifa... Njia bora ya kutekeleza nia hii itakuwa kukabidhi malezi ya mataifa hayo mikononi mwa mataifa yaliyoendelea... ambayo ni tayari kukubali ulezi huu kama wakabidhi kwa niaba ya shirikisho la mataifa."
Katiba ikaendelea kutofautisha kati ya maeneo kama ifuatayo:
"Jumuiya kadhaa zilizokuwa chini ya Milki ya Uturuki zimefikia kwenye ngazi ambako zinaweza kukubaliwa kama mataifa ya pekee, lakini bado chini ya usimamizi wa nchi mlezi hadi wakati zitakapoweza kusimama pekee zao. Jumuiya hizi zinapaswa kusikilizwa kuhusu chaguo la nchi mlezi."
"Mataifa mengine, hasa ya Afrika ya Kati, yako katika hali ya kwamba mlezi atawajibika kutawala maeneo yao kwa masharti ya kuhakikisha uhuru wa dhamiri na wa dini, kutunza usalama na maadili mema na kuzuia dhuluma kama biashara ya watumwa, silaha na vileo."
""Halafu kuna maeneo, kama vile Afrika ya Kusini-Magharibi na visiwa kadhaa vya Pasifiki ya kusini, ambayo yatasimamiwa na mlezi kulingana na sheria zake kama sehemu ya eneo lake kwa sababu yana wakazi wachache mno au ni madogo mno au yako mbali mno na vitovu vya ustaarabu. Hata hivyo utawala huu unapaswa kuangalia masharti yaliyotajwa hapo juu kuhusu masharti yanayotunza wakazi wazalendo."
Vipengele hivi vilianzisha muundo wa maeneo ya kudhaminiwa kwenye ngazi za A), B) na C). Maeneo ya kudhaminiwa ya A) yalipata kiwango cha utawala wa ndani tangu mwanzo, yakapewa uhuru kati ya 1932 na 1946.
Maeneo ya kudhaminiwa ya kundi A)
[hariri | hariri chanzo]Maeneo haya yalikuwa sehemu za Milki ya Osmani yasiyokaliwa na Waturuki.
Chini ya ulezi wa Uingereza:
- Mesopotamia iliendelea kupata uhuru kama ufalme wa Irak (1932)
- Palestina iligawiwa katika maeneo ya
- Ng'ambo ya Yordani iliyoendelea kupata uhuru kama ufalme wa Yordani (1946) na
- Palestina yenyewe ambamo sehemu kubwa ilipata uhuru 1949 kama nchi ya Israel wakati sehemu zilizobaki ziliendelea kuwa maeneo ya Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina.
Chini ya Ulezi wa Ufaransa:
Maeneo ya kudhaminiwa ya kundi B)
[hariri | hariri chanzo]Nchi hizi zilikuwa zote koloni za Ujerumani katika Afrika.
Chini ya ulezi wa Ufaransa hadi uhuru mwaka 1960:
Chini ya ulezi wa Uingereza:
- Tanganyika (uhuru 1961)
- sehemu ndogo ya Kamerun
- sehemu ndogo ya Togo
Sehemu ya kiingereza ya Kamerun iligawiwa tena; wakazi wa kusini walipiga kura kujiunga na Kamerun ya Kifaransa baada ya uhuru mwaka 1960, lakini watu wa kaskazini walipendelea kujiunga na Nigeria.
Sehemu ya kiingereza ya Togo iliunganishwa Ghana mwaka 1956.
Chini ya Ulezi wa Ubelgiji:
Maeneo ya kudhaminiwa ya kundi C)
[hariri | hariri chanzo]Kundi hili lilijumlisha maeneo mengine yaliyokuwa chini ya Ujerumani pamoja na
- Afrika ya Kusini-Magharibi ikatawaliwa na Afrika Kusini kama sehemu ya nchi hii ikapata uhuru kama Namibia mwaka 1990.
- Guinea Mpya ikatawaliwa na Australia pamoja na koloni lake la Papua zikapata uhuru pamoja kama Papua Guinea Mpya mwaka 1975
- Samoa Magharibi ikatawaliwa na New Zealand ikapata uhuru kama Samoa mwaka 1962
- Nauru ikatawaliwa na Australia, Uingereza na New Zealand pamoja, ikapata uhuru wake mwaka 1968
- visiwa vifuatavyo vilitawaliwa na Japani hadi mwaka 1945 na baadaye zilisimamiwa na Marekani:
- Visiwa vya Mariana ya Kaskazini - viliamua mwaka 1978 kubaki kama eneo linaloshirikishwa na Marekani
- Visiwa vya Marshall - vikapata uhuru mwaka 1979
- Palau - ikapata uhuru mwaka 1981
- Funguvisiwa la Karolini lililopata uhuru kama Shirikisho la Mikronesia mwaka 1986
Marshall, Palau na Mikronesia vyote vina mikataba ya ushirikiano na Marekani.
Athira ya hali ya kisheria kwa maisha ya koloni
[hariri | hariri chanzo]Maeneo ya kudhaminiwa ya B) yalitendewa kama makoloni ya kawaida. Lakini masharti ya udhamini yalikuwa muhimu kwa maazimio ya serikali ya kikoloni hasa baada ya 1946.
Katika Tanganyika upinzani wa Umoja wa Mataifa mwaka 1946 ulizuia mipango ya kuunganisha Tanganyika na Kenya uliyopingwa wakati ule na wenyeji wengi kwa sababu Kenya ilijadiliwa kuwa koloni la walowezi Wazungu hasa.
Vilevile maswali ya kamati ya UM yalikuwa na athira katika suala la ardhi ya Waafrika na kupanua ardhi mikononi mwa walowezi Wazungu. Masharti ya udhamini yalidai ya kwamba Uingereza kama mlezi utatunza ardhi ya wazalendo. Hata hivyo Uingereza ulitumia sheria iliyoangalia ardhi isiyolimwa kama mali ya serikali iliyoweza kukabidhiwa kwa walowezi. Sheria hii haikuheshimu utaratibu wa kilimo cha kijadi ambako mashamba yalihamishwa kila baada ya miaka kadhaa. Kwa njia ya sheria hizo serikali za kikoloni zilitwaa sehemu kubwa ya ardhi ya kimapokeo ya vijiji. Kwa hiyo Uingereza ilikuwa na njia za kupita masharti ya udhamini.
Mwaka 1951 serikali ya kikoloni iliwafukuza wakazi wa kijiji cha Engare Nanyuki katika nchi ya Wameru kwa sababu ilipanga kuanzisha mashamba kwa walowezi. Wameru walituma wawakilishi New York kulalamika mbele ya Umoja wa Mataifa. Sehemu kubwa ya wanachama wa UM walisimama upande wa Wameru; upinzani huo ulikuwa na athari muhimu katika maazimio ya Waingereza kutopanua mno mashamba ya Wazungu katika Tanganyika.