Otto von Bismarck

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Otto von Bismarck

Otto von Bismarck (1 Aprili 181530 Julai 1898) alikuwa mwanasiasa mashuhuri wa Ujerumani katika karne ya 19.

Akiwa waziri mkuu wa Prussia alijenga umoja wa Ujerumani katika vita tatu dhidi ya Denmark (1864), Austria (1866) na Ufaransa (1870/71).

Kama Chansella wa Dola la Ujerumani aliongoza siasa ya nchi hadi 1890 alipoachishwa na Kaisari kijana Wilhelm II.

Maisha yake ya awali[hariri | hariri chanzo]

Bismarck mwaka 1836

Jina lake kamili lilikuwa Otto Eduard Leopold von Bismarck-Schönhausen. Alizaliwa katika familia ya kitemi wa cheo cha chini katika ufalme wa Prussia, mama yake alikuwa wa asili ya kiraia.

Alisoma sheria na kilimo kwenye chuo kikuu baada ya kumaliza elimu ya sekondari, halafu akajiunga na jeshi kwa utumishi wake wa lazima.

Baada ya kifo cha baba mwaka 1845 akachukua utawala wa mashamba ya familia yake.

Mwaka 1847 akafunga ndoa na Marie von Thadden akazaa naye watoto watatu: Marie (1847–1926), Herbert (1849–1904) na Wilhelm (1852–1901).

Mwanasiasa, mbunge na balozi wa Prussia[hariri | hariri chanzo]

Bismarck-Monument, Hamburg

Wakati wa mapinduzi ya kwanza ya kidemokrasia katika Ujerumani (1848/49) alijiunga na siasa akawa mtetezi wa haki za mfalme na mpinzani wa wanademokrasia. Akachaguliwa katika Bunge la Prussia.

Mwaka 1851 mfalme wa Prussia alimteua kuwa mwakilishi wa Prussia katika halmashauri ya Shirikisho la Kijerumani huko Frankfurt - wakati ule Ujerumani ilikuwa shirikisho lisilo na nguvu ya madola 38 yaliyojitegemea. Madola makubwa katika shirikisho hili yalikuwa Austria na Prussia. Bismarck alikuwa pia na vipindi vifupi vya utumishi kama balozi wa Prussia huko St. Petersburg na Paris.

Waziri mkuu wa Prussia[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1862 aliteuliwa na mfalme Friedrich Wilhelm IV kuwa waziri mkuu wa Prussia. Shabaha yake kuu ilikuwa kuongeza uwezo wa nchi. Aliimarisha jeshi la Prussia dhidi ya upinzani wa wabunge wengi. Jeshi hilo lilipewa nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika vita dhidi ya Denmark ya mwaka 1864. Matokeo ya vita yaliongeza mashindano kati ya Prussia na Austria juu ya kipaumbele ndani ya Shirikisho la Kijerumani.

Matokeo yake yalikuwa vita ya mwaka 1866. Prussia, pamoja na madola kadhaa madogo, ilishinda Austria na jeshi la Shirikisho la Kijerumani. Shirikisho lilivunjika, Prussia ilimeza madola kama Hannover na Hesse yaliyokuwa yameshikamana na Austria ikawa dola kabisa ndani ya Ujerumani. Austria ilijiondoa katika siasa ya Kijerumani na idadi kubwa ya madola ya Kijerumani ilijiunga na Prussia katika shirikisho la Ujerumani ya Kaskazini.

Bismarck alilenga sasa kukamilisha kipaumbele cha Prussia katika Ujerumani. Alitumia nafasi ya magongano na Ufaransa juu ya uchaguzi wa mfalme mpya wa Hispania. Kaisari Napoleon III wa Ufaransa alitaka Mfaransa achaguliwe lakini Bismarck alimsukuma mgombea Mjerumani. Katika vita ya maneno ya kidiplomasia chansella aliweza kumwaibisha mtawala wa Ufaransa. Napoleoni III alitangaza hali ya vita dhidi ya Prussia lakini madola ya Ujerumani ya Kusini, kama falme za Bavaria na Wuerttemberg, yalijiunga na Prussia.

Bismarck (sare nyeupe) akimtangaza mfalme wa Prussia kuwa Kaisari wa Ujerumani Wilhelms I tarehe 18 Januari 1871 katika jumba la kifalme la Versailles, Ufaransa.

Vita hii ilikuwa mara ya kwanza ya kwamba Wajerumani wote -isipokuwa Austria- walishikamana pamoja tangu muda mrefu sana. Bismarck alitumia nafasi ya ushindi wa jeshi la Wajerumani kuwakusanya viongozi wa madola yote ya Ujerumani katika jumba la Kifalme la Ufaransa huko Versailles. Mfalme wa Prussia Friedrich Wilhelm IV alitangazwa kuwa Kaisari Wilhelm I wa Ujerumani - cheo hiki hakikutumika katika Ujerumani tangu mwaka 1806. Dola la Ujerumani liliunganisha madola yote ya Ujerumani ya kale, isipokuwa Austria, chini ya mfalme wa Prussia aliyekuwa sasa pia na cheo cha Kaisari wa Ujerumani.

Bismarck alikuwa mkuu wa serikali kama Chansella wa Ujerumani.

Bismarck akivaa sare ya kijeshi

Bismarck na ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Bismarck alikuwa kiongozi wa Ujerumani wakati nchi za Ulaya ziliendelea kujipatia pande kubwa za dunia kama koloni. Mwanzoni alipinga makoloni kwa Ujerumani. Aliona gharama kubwa za kupata, kujenga na kutetea koloni akaona ya kwamba faida yoyote ya kuwa nazo hailingani na gharama hizo.

Tangu miaka ya 1870 iliongezeka idadi ya watu katika Ujerumani waliodai koloni kwa sababu mbalimbali. Wengine walidai koloni kama ishara ya nchi kubwa na muhimu, wengine walikuwa wafanyabiashara waliotafuta ulinzi wa manowari za Kijerumani kwa ajili ya biashara yao dhidi ya wenzao wa mataifa mengine. Bismarck aliona ya kwamba hali ya Ujerumani haitegemei kuwepo kwa bendera yake katika pembe za dunia, bali uhusiano na majirani makubwa katika Ulaya hasa Uingereza, Ufaransa na Urusi. Tamko maarufu alipotembelewa na mgeni aliyetaka kumhamasisha kuunda koloni katika Afrika likawa "Ramani yako ya Afrika ni ya kuvutia sana. Lakini ramani yangu ya Afrika iko Ulaya. Ufaransa iko upande wa kushoto, Urusi upande wa kulia, katikati tuko sisi".[1]

Alipenda kuwahamisha Wafaransa kujipatia koloni kwa matumaini ya kwamba watatumia nguvu zao Afrika na kusahau fikra za kulipiza kisasi baada ya kushindwa na Ujerumani katika vita ya 1870/71.

Tangu mwaka 1880 Bismarck alitegemea bungeni vyama vya kisiasa vilivyotaka kuunda makoloni, hivyo alilegea na polepole kukubali kuanzishwa kwa makoloni kadhaa. Mwanzoni alitoa tu nyaraka za ulinzi kwa makampuni yaliyopatana kukodi maeneo na watawala wa Afrika na wa Pasifiki.

Baada ya makampuni hayo kushindwa kuendesha maeneo hayo alikubali pia kuingilia moja kwa moja, kwa mfano baada ya Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki kushindwa katika vita ya Abushiri mwaka 1889. Kwa hiyo Ujerumani ikajiunga na mataifa mengine ya Ulaya katika ugawaji wa Afrika kwa sababu za siasa ya ndani.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Volker Ullrichs (Otto von Bismarck, toleo la nne, Rowohlt, Reinbek 1998) uk 101