Nenda kwa yaliyomo

Dola la Tatu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Bendera ya Ujerumani wakati wa Dola la Tatu

Dola la Tatu (Kijer.: Drittes Reich) ilikuwa jina la kutaja Ujerumani wakati wa utawala wa Adolf Hitler na chama chake cha NSDAP (Chama cha Nazi) kati ya 1933 na 1945. Haikuwa jina rasmi lakini likatumiwa na Hitler mwenyewe na wenzake.

Hitler alichukua utawala juu ya Dola la Ujerumani akimaliza kipindi cha kidemokrasia cha Jamhuri ya Weimar na kuanzisha udikteta wake.

Kwa kutumia neno hili wafuasi wa Hitler walitaka kupanga utawala wao katika ufuatano wa madola makubwa katika Ujerumani. Katika itikadi hii "Dola la Kwanza" ilikuwa Dola Takatifu la Kiroma lilioanzishwa katika Ujerumani pamoja na sehemu za Italia kati ya karne ya 10 hadi 1804. "Dola la Pili" waliita dola la Ujerumani (bila Austria) tangu 1871 hadi 1918 lililotawaliwa na mfalme wa Prussia kama kaisari wa Ujerumani.

Madola haya mawili yaliporomoka na "dola la tatu" lilitakiwa kuchukua nafasi yao. Lakini walidai ya kwamba dola hili lingedumu wakaiita pia kwa jina la "Dola la Miaka 1000" (kijer.: Tausendjähriges Reich). Lakini utawala wao ukadumu miaka 12 pekee hadi 1945.