Nenda kwa yaliyomo

Angela Merkel

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Dk. Angela Dorothea Merkel (amezaliwa Hamburg, 17 Julai 1954) ni mwanafizikia na mwanasiasa wa Kijerumani aliyekuwa Chansela wa Ujerumani tangu tarehe 22 Novemba 2005 hadi 8 Desemba 2021.

Familia na elimu[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa 1954 mjini Hamburg katika familia ya Horst na Herlind Kasner. Baba yake alikuwa mchungaji wa Kanisa la Kilutheri, mama alikuwa mwalimu. Mwaka uleule familia ilihamia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani (ambayo ilikuwa Ujerumani ya Mashariki, kabla ya pande zote mbili za Ujerumani kuungana tena kuwa moja) ambapo aliishi huko hadi Muungano wa Ujerumani ulipofanyika mnamo mwaka wa 1990. Tangu mwaka 1957 familia iliishi mjini Templin katika kaskazini ya nchi ambako mchungaji Kasner alikuwa mkuu wa chuo cha theolojia. Mama yake Angela alizuiliwa kufanya kazi ya ualimu kwa sababu serikali ya kikomunisti haikutaka mke wa mchungaji kuwa shuleni. Angela ana wadogo wawili.

Alisoma shule ya sekondari kwake Templin alipofaulu hasa katika masomo ya Kirusi na hisabati. Aliingia pia katika Umoja wa Vijana wa Chama cha Kikomunisti FDJ[1]. Alipomaliza shule kwenye mwaka 1973 wastani ya maksi zake ilikuwa A+.

Mwaka 1973 hadi 1978 alisoma fizikia kwenye Chuo Kikuu cha Leipzig. Mwaka 1977 alifunga ndoa na mwanafunzi mwenzake Ulrich Merkel lakini ndoa hii ilitalikiwa mwaka 1982: ni hapa alipopata jina lake maarufu. Tangu 1978 aliajiriwa kwenye Taasisi Kuu kwa Kemia ya Kifizikia katika Berlin ya Mashariki. Hapa alimaliza tasnifu ya Uzamivu mwaka 1986 iliyokubaliwa kwa heshima kuu "magna cum laude". Aliendelea na kazi kweye taasisi ya kemia ya kichanganuzi.

Mwaka 1984 alikutana kwenye Taasisi ya Taaluma ya Sayansi ya Berlin na mwanakemia Joachim Sauer akaolewa naye mwaka 1998. Angela hajazaa watoto bali alilea watoto wa Sauer akiendelea kutumia jina la Merkel.

Siasa[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa masomo na kazi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani Angela hakuingia katika chama cha kikomunisti wala chama kingine lakini alihudhuria katika kazi ya umoja wa vijana wa chama hiki.

Baada ya kuporomoka kwa ukomunisti na anguko la ukuta wa Berlin mwaka 1989-1990 Merkel alijiunga na chama kilichoundwa upya Demokratischer Aufbruch (DA - "uamsho wa kidemokrasia") akianza kazi kwenye ofisi ya chama hicho na baadaye kuwa afisa mawasiliano wa chama; baada ya kuingia kwa chama hiki katika serikali huru ya kwanza ya Ujerumani ya Mashariki alikuwa makamu wa afisa mawasiliano wa serikali.

Mwaka 1990 chama chake kiliamua kujiunganisha na chama cha magharibi CDU (Chama cha Kikristo cha Kidemokrasia cha Ujerumani) kilichokuwa chama cha chansela Helmut Kohl aliyeendelea kumwangalia na kumsadia katika siasa maana wanasiasa wa magharibi walitafuta wananchi wa mashariki ambao hawakuwa wanachama wa chama cha kikomunisti jinsi walivyokuwa karibu wote wenye madaraka kabla ya kuporomoka kwa utawala wake katika mwaka 1989. Mwisho wa 1990 Merkel aligombea kwenye uchaguzi wa bunge kwa niaba ya CDU katika jimbo la Mecklenburg-Pomerini Magharibi akachaguliwa. Baada ya uchaguzi chansela Kohl alimpa wizara ndogo kwa wanawake na vijana. Mwaka uleule alichaguliwa kuwa makamu wa mwenyekiti wa chama cha CDU kama mwakilishi mmojawapo wa mashariki ya Ujerumani. 1994 alichaguliwa tena kuwa mbunga akapewa wizara ya Ujenzi na Mipango ya Miji.

1998 CDU ilishindwa katika uchaguzi wa bunge ikatoka serikalini. Sasa Merkel aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa chama. Aliendelea kuwa mwenyekiti wa CDU katika mwaka 2000 lakini hakuongoza chama kwenye bunge. Uongozi huu alichukua baada ya chama kilishindwa tena katika kura ya 2002.

Baada ya uchaguzi wa 2006 vyama vilivyotawala yaani SPD na Green vilikosa kura za kutosha lakini CDU ilikuwa na wabunga wachache wengi kuliko SPD. Hapa Merkel alifaulu kupatana na viongozi wa SPD kuunda serikali ya umoja chini ya uogozi wake.

Hivyo Merkel amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa Kansela kunako tar. 22 Novemba 2005 katika serikali ya mseto wa vyama viwili vya kisiasa vya Kijerumani, yaani kati ya CDU/CSU na SPD.

Mwaka 2009 alitangaza ya kwamba alielekea kuaachana na SPD akitafuta ushirikiano na chama cha FDP (liberali). Uchaguzi wa bunge wa Septemba 2009 ulirudisha chama chake cha CDU tena kama chama kikubwa akaendelea kuunda serikali mpya pamoja na FDP. Katika kipindi hiki kulikuwa na maazimo mawili yaliyoendelea kuwa na umuhimu kwa baadaye

  • mwezi wa Mei 2010 Ujerumani ilikubali mpango wa nchi za Umoja wa Ulaya kusaidia uchumi wa Ugiriki kwa kuikopesha bilioni 80 za Euro baada ya nchi hii kushindwa kupipa madeni yake. Msaada huu kwa Ugriki na nchi kadhaa nyingine zilizotumia hela ya Euro ilipaswa kurudishwa ikaunda uchungu kati ya sehemu ya wananchi waliosikia hapa Ujerumani unalipa madeni ya mataifa mengine yasiyojali kanuni za kiuchumi.
  • Merkel aliwahi kurahisisha masharti ya kuendesha matanuri nyuklia lakini baada ya ajali ya kinyuklia ya Fukushima (Japani) serikali ya Merkel ilisimamisha matanuri nyuklia ya zamani mara moja na kuamua mpango wa kusimamisha matanuri nyuklia zote hadi mwaka 2022 na kubadilisha uzalishaji wa umeme wa Ujerumani kufanywa kwa nishati mbadala pekee.

Katika uchaguzi wa 2013 Merkel alifaulu kuboresha matokeo ya kura kwa ajili ya chama chake cha CDU lakini chama kidogo cha FDP kilishindwa kupata asilimia 5 za kura kikatoka bungeni. Merkel aliunda upya serikali ya mseto na SPD akaendelea kuongoza nchi. Mwaka 2015 aliamua kufungua mipaka ya Ujerumani kwa idadi kubwa ya wakimbizi hasa kutoka Syria, Irak na Afghanistan waliokuwa njiani wakitembea kutoka Uturuki kuelekea Ulaya ya Magharibi katika hali gumu. Alisifiwa na wengi kwa hatua hii lakini alipingwa pia vikali ndani ya nchi baada ya kufika kwa takriban milioni 1 wageni katika muda mfupi. Kwa jumla alibahatika ya kwamba hali ya kiuchumi ya Ujerumani ilikuwa vizuri lakini hakuchukua hatua za kuondoa hali gumu ya wananchi wasio na elimu ya kufaa kwa mahitaji ya uchumi na kudumu maisha yao kwa mapato madogo kulingana na mazingira ya Ujerumani.

Katika uchaguzi wa Oktoba 2017 vyama vya serikali ya mseto vilipotea kura nyingi hata kama CDU bado ilitoka kuwa chama kikubwa zaidi.

Mwezi wa Oktoba 2018 Merkel alitangaza kwamba hagombei tena uwenyekiti wa chama na kwamba hatagombea upya nafasi ya chansela kwenye uchaguzi mkuu ujao uliopangwa kwa Oktoba 2021. [2]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Takriban asilimia 80 wa vijana katika Ujerumani ya Mashariki walikuwa wanachama; watoto wa familia za Wakristo mara nyingi walikataa kujiunga. Lakini nafasi za kusoma A-level shuleni na baadaye kwenye Chuo Kikuu zilitegema uanachama.
  2. https://www.bbc.com/news/world-europe-46020745 Angela Merkel to step down as German chancellor in 2021, tovuti ya BBC tar. 29. 10. 2018

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Angela Merkel kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.