Chama cha Kijamaa-Kidemokrasia cha Ujerumani
Chama cha Kijamaa-Kidemokrasia cha Ujerumani Sozialdemokratische Partei Deutschlands | |
---|---|
Headquarters | Willy-Brandt-Haus D-10911 Berlin |
Ideology | Ujamaa wa kidemokrasia |
International affiliation | Socialist International |
European affiliation | Party of European Socialists |
European Parliament Group | Progressive Alliance of Socialists and Democrats |
Official colors | Red |
Chama cha Kijamaa-Kidemokrasia cha Ujerumani (kwa Kijer. Sozialdemokratische Partei Deutschlands au SPD, Kiing. Social Democratic Party of Germany) ni chama cha siasa nchini Ujerumani kilichoundwa mnamo 23 Mei 1863. SPD ni kimoja kati ya vyama vya kisiasa muhimu zaidi katika Ujerumani ya sasa, pamoja na Chama cha Kidemokrasia cha Kikristo (CDU).
Historia
[hariri | hariri chanzo]SPD ilianzishwa kama "Shirika la Wafanyakazi wa Kijerumani" (Allgemeiner Deutscher Arbeiterverein, ADAV) mnamo 23 Mei 1863 huko Leipzig. Mwanzilishi alikuwa Ferdinand Lassalle. Mnamo 1875 ADAV ilijiunga na Chama cha Wafanyakazi wa Kidemokrasia ya Jamii ( Sozialdemokratische Arbeiterpartei ) (SDAP), ambayo ilianzishwa mnamo 1869 huko Eisenach na August Bebel na Wilhelm Liebknecht.
Jina jipya lilikuwa Chama cha Wafanyakazi cha Kijamaa cha Ujerumani (Sozialistische Arbeiterpartei Deutschlands, SAP).
Tangu mwaka 1890 kilichukua jina lake la sasa.
Katika miaka kuanzia 1875 hadi 1890 kilipigwa marufuku na Otto von Bismarck.
Baada ya kuruhusiwa tena SPD ilikuwa mara kwa mara chama kikubwa zaidi bungeni lakini haikushirikishwa katika serikali yoyote. Wabunge wake, hasa Karl Liebknecht, walipinga siasa ya ukoloni ya Ujerumani.
Baada ya kuanzishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914, SPD iliona farakano. Wabunge walio wengi walikubali makisio ya pekee kwa ajili ya jeshi wakiamini Ujerumani ilishmabuliwa, ilhali kundi dogo zaidi lilikataa makisio wakipinga kushiriki vita vyovyote. Kundi hilo lilianzisha chama cha USPD ("SPD ya kujitegemea") kilichopinga vita.
Mwisho wa vita mnamo mwaka 1918, mapinduzi yaliondoa utawala wa kifalme na SPD ikaongoza serikali kadhaa.
Wakati wa mdororo mkuu wa uchumi baada ya mwaka 1929, vyama adui wa demokrasia vilipata nguvu katika Ujerumani. Mwaka 1933 SPD kilikuwa chama pekee katika bunge kilichokataa kukubali "sheria ya mamlaka" (Ermächtigungsgesetz) iliyokuwa msingi wa kisheria kwa udikteta wa Adolf Hitler.
Baadaye Hitler alipiga tena SPF marufuku na kuwakamata wanachama wengi, wengine walikimbia nje ya nchi.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, SPD ilirudi. Katika Ujerumani ya Mashariki watawala Wasovyeti walilazimisha maungano ya SPD na chama cha Kikomunisti na kukamata wanachama waliopinga.
Katika Magharibi mwa Ujerumani SPD iliendelea kama chama kikubwa zaidi ya mrengo wa kushoto.
SPD iliongoza serikali kadhaa za majimbo huko Ujerumani Magharibi, lakini kila wakati ilikuwa chama kikuu cha upinzani katika bunge la shirikisho.
Iliingia katika serikali mara ya kwanza mnamo 1966 chini ya chansela Kurt Georg Kiesinger wa chama cha CDU.
Mnamo 1969 mwenyekiti wa SPD Willy Brandt aliweza kuunda serikali pamoja na chama kidogo cha kiliberali FDP. Chini ya uongozi wake, Ujerumani ya Magharibi iliweza kujenga upatanisho na Poland na kutambua mipaka mipya iliyowahi kutokea baada ya Vita Kuu ya Pili ambako Ujerumani ilipungukiwa maeneo makubwa. Brandt alifuatwa 1974 na mwana SPD mwingine, Helmut Schmidt katika uongozi wa serikali.
Miaka 1982 hadi 1998 SPD iliondoka katika serikali ikawa tena chama cha upinzani.
Kati ya 1998 na 2005 SPD iliweza kurudi katika uongozi wa serikali chini ya chansela Gerhard Schröder aliyeshiriki na chama cha kiekolojia cha Green Party.
Tangu Novemba 2005 hadi mwaka 2021 SPD ikawa mshirika mdogo katika ushirikiano na CDU chini ya chansela Angela Merkel .
Katika miaka hii kura za SPD katika chaguzi kwenye shirikisho na majimbo ziliendelea kupungua. Lakini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 SPD ilikuwa tena chama kikubwa kwa kupata kura zaidi kidogo kuliko CDU.
Siasa
[hariri | hariri chanzo]Kihistoria SPD ilikuwa chama cha wafanyakazi nchini Ujerumani kilichofuata shabaha ya ujamaa ambapo viwanda vikubwa vitawekwa mikononi mwa serikali. Mnamo 1959 SPD iliachana rasmi na itikadi ya Umaksi ikakubali uchumi wa soko (ambapo watu na kampuni zinaweza kutawala mali ya kila aina na kulenga faida yake kwenye soko la uchumi) ikidai kwamba nguvu ya uchumi wa binafsi inatakiwa kujenga manufaa ya jamii yote. Hivyo ni kazi ya dola kuwasaidia wanyonge kwa misaada ikiwa hawana kazi, ni wagonjwa au wazee). Kampuni zinaweza kupata ruzuku ili kuzisaidia ziendelee katika hali ngumu ili wafanyakazi wasikose ajira na mishahara.
Kujisomea
[hariri | hariri chanzo]- Carl E. Schorske, German Social Democracy, 1905-1917: The Development of the Great Schism (Harvard University Press, 1955).
- Vernon L. Lidtke, The Outlawed Party: Social Democracy in Germany, 1878-1890 (Princeton University Press, 1966).
- Abraham J. Berlau, The German Social Democratic Party, 1914-1921 (Columbia University Press, 1949).
- Erich Matthias The Downfall of the Old Social Democratic Party in 1933 pages 51–105 from Republic to Reich The Making of the Nazi Revolution Ten Essays edited by Hajo Holborn, (New York: Pantheon Books, 1972).
Tovuti za Nje
[hariri | hariri chanzo]- Party official website in English Archived 2006-07-11 at the Wayback Machine
- official website of the party's youth organisation Ilihifadhiwa 28 Septemba 2021 kwenye Wayback Machine.
- Is the Left Still on the Left? Archived 2006-06-01 at the Wayback Machine — Dirk Maxeiner and Michael Miersch on the German left