Mkataba wa Helgoland-Zanzibar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mkataba wa Helgoland-Zanzibar
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Mapatano baina Uingereza na Ujerumani kuhusu Afrika na Helgoland (kifupi mkataba wa Helgoland-Zanzibar) yalifanywa kati ya Ujerumani na Uingereza tarehe 1 Julai 1890. Pande zote mbili zilielewana juu ya mipaka ya makoloni yao au maeneo walimotaka kuwa na athira kuu katika Afrika.

Mkataba ulihusu maeneo katika Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kusini-Magharibi (leo Namibia) na Afrika ya Magharibi (Togo ya leo) pamoja na kisiwa cha Helgoland mbele ya pwani ya Ujerumani katika Bahari ya Kaskazini.

Shabaha ya mkataba[hariri | hariri chanzo]

Shabaha kuu ya mkataba wa 1890 ilikuwa kuondoa hatari za migongano kati ya Ujerumani na Uingereza na kutunza uhusiano mzuri.

Tangu kufika kwa Ujerumani kama mkoloni kwenye bara la Afrika mwaka 1884 Uingereza ulitafuta mapatano ya amani na nchi hii. Serikali ya Ujerumani chini ya chansella Bismarck ilijitahidi pia kutovurugisha uhusiano na Uingereza. Baada ya kuanzishwa kwa koloni ya Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki kwenye sehemu za Tanganyika, kulikotokea kiasili dhidi ya nia ya Bismarck, serikali hizi mbili zilikubaliana mapatano ya 1886 kati ya Ujerumani na Uingereza juu ya Afrika ya Mashariki kuhusu maeneo walipotaka kuwa na kipaumbele na maeneo waliyokubali kuwa ya Zanzibar.

Udhaifu wa Zanzibar ulizidi kuonekana katika miaka iliyofuata ambako Sultani alikodi haki zake kwenye pwani la Afrika Mashariki kwanza kwa kampuni ya Kiingereza mwaka 1887 upande wa kaskazini halafu kwa kampuni ya Kijerumani upande wa kusini mwaka 1888. Katika vita ya upinzani wa wenyeji dhidi ya kampuni ya Kijerumani, Sultani alishindwa kufanya lolote. Hivyo Ujerumani na Uingereza waliendelea kugawana maeneo yake. Ujerumani walikubali ulinzi wa Uingereza juu ya maeneo yote yaliyobaki rasmi chini ya Sultani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba. Sultani aliambiwa kukubali kuza maeneo yake ya pwani (yaliyokuwa baadaye Tanganyika) kwa Ujerumani na kukubali ulinzi wa Uingereza juu ya maeneo yake yaliyobaki.

Leo von Caprivi alikuwa chansella mpya wa Ujerumani tangu Machi 1890 akimfuata Otto von Bismarck. Caprivi alitaka kujenga uhusiano mwema hasa na Uingereza.

Wakati huohuo uhusiano ule ulikuwa mashakani kidogo kutokana na matendo ya Karl Peters aliyejaribu kupanua eneo la Shirika la Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki hadi Uganda, kinyume cha mapatano ya 1886 kati ya Ujerumani na Uingereza juu ya Afrika ya Mashariki.

Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

Uingereza ulikubali koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika, Rwanda, Burundi za leo). Waingereza waliahidi kumshawishi Sultani wa Zanzibar ili awaachie Wajerumani haki za Zanzibar huko Tanganyika.

Ujerumani ulifuta mipango yake katika Uganda na Zanzibar ambako Mjerumani Karl Peters aliwahi kusaini mapatano ya ushirikiano na Kabaka na Sultani.

Pia uliwaachia Waingereza Usultani wa Witu uliokuwa tayari chini ya ulinzi wa Ujerumani tangu mwaka 1885 na madai yake kwenye pwani ya Kenya katika eneo la funguvisiwa ya Lamu na pwani ya Somalia hadi Kismayu.

Mengineyo ni kwamba mkataba ulieleza mipaka baina ya maeneo chini ya athari ya Uingereza na athari ya Ujerumani. Hapa kuna pia kipengele kuhusu mipaka kwenye Ziwa Nyasa kilichounda msingi kwa kutoelewana baina ya Malawi na Tanzania kuhusu mipaka kwenye ziwa hili tangu uhuru.[1]

Afrika ya Kusini-Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Pande zote mbili zilipatana kuhusu utawala wa Kijerumani katika eneo ambalo likawa Namibia baadaye. Wajerumani walikubali kutovuka mstari wa mto Oranje upande wa kusini na kukubali utawala wa Waingerezea juu ya Botswana.

Wajerumani walipewa pia njia ya kufikia Mto Zambezi katika kanda lililoitwa baadaye Kishoroba cha Caprivi.

Afrika ya Magharibi[hariri | hariri chanzo]

Pande zote mbili zilipatana kuhusu mipaka kati ya makoloni yao ya Togo ya Kijerumani na "Pwani ya dhahabu ya Kiingereza" (leo Ghana) halafu kati ya Kamerun na "eneo la Kiingereza linalopakana" (leo Nigeria).

Ulaya[hariri | hariri chanzo]

Uingereza uliachia Ujerumani kisiwa cha Helgoland katika Bahari ya Kaskazini. Kisiwa hicho kiliwahi kuchukuliwa na Uingereza wakati wa vita dhidi ya Napoleon Bonaparte mwaka 1807 ikawa koloni la Kiingereza. Kisiwa kilidaiwa na Ujerumani kwa sababu kihistoria ni sehemu ya jimbo la Frisia ya Kaskazini lililokuwa sehemu ya Ujerumani baada ya kuhamishwa mara kadhaa kati ya Ujerumani na Denmark.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Article I ilisema: "In East Africa, Germany's sphere of influence is demarcated thus: ...2. To the south by the line that starts on the coast of the northern border of Mozambique Province and follows the course of the Rovuma River to the point where the Messinge flows into the Rovuma. From here the line runs westward on the parallel of latitude to the shore of Lake Nyasa. Turning north, it continues along the eastern, northern, and western shores of the lake until it reaches the northern bank of the mouth of the Songwe River...."

Vyanzo na viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]