Kampuni ya Kifalme ya Kiingereza kwa Afrika ya Mashariki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Kampuni ya Kifalme ya Kiingereza kwa Afrika ya Mashariki (Imperial British East Africa Company (IBEAC)) ilikuwa shirika iliyoanzisha koloni ya Afrika ya Mashariki ya Kiingereza kuanzia 1888. Koloni hii ilikuwa utangulizi wa taifa la Kenya.

Biashara ya Mackinnon[hariri | hariri chanzo]

Kampuni ilianzishwa baada ya mkutano wa Berlin wa 1885 kwa kusudi la kufanya biashara katika maeneo ya Afrika ya Mashariki. Kiongozi wa kwanza alikuwa William Mackinnon aliyetafuta usaidizi wa serikali yake kwa mipango yake. Mackinnon aliwahi kujenga biashara kubwa kote kwenye Bahari Hindi akaelewana vema na Sultan Bargash wa Zanzibar aliyeongea naye juu kumkodishia maeneo ya Sultani Afrika bara hadi Kongo. Mackinnon aliamini ya kwamba biashara ya Afrika bara ilikuwa na nafasi kubwa. Awali serikali ya Uingereza ilikataa kukubali mipango hii hadi Wajerumani walingia kati na kuanzisha Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.

Uganda[hariri | hariri chanzo]

Sasa Waingereza walishtuka na wapinzani wa koloni mpya walidhoofika. Mkataba kati ya Ujerumani na Uingereza wa 1886 ulichora mstari wa mpaka kati ya maeneo ya athira za nchi zote mbili katika Afrika Mashariki - mpaka wa Kenya na Tanzania ya leo. Mapatano haya yalikuwa msingi wa Mckinnon kuandikisha kampuni yake ya Afrika ya Mashariki kwa madhumini ya kuanzisha biashara barani. 1887 kampuni ilikodisha maeneo ya bara ya Zanzibar kaskazini eneo la Kijerumani kwa miaka 50. Tar. 6 Septemba 1888 kampuni iliandikishwa London na kupewa barua ya ulinzi wa serikali ya Uingereza.

Mashindano juu ya Uganda kati ya Ujerumani na Uingereza uliharakisha uenezi wa kampuni. 1890 Mjerumani Karl Peters alifanya mkataba na Kabaka Mwanga II wa Buganda ulioweka Buganda chini ya ulinzi wa Ujerumani lakini bila idhini ya serikali ya Berlin. Mapatano haya yalisababisha kusainiwa kwa mkataba wa Helgoland-Zanzibar ulioweka Uganda chini ya Uingereza. Kampuni ya Mckinnon ilipewa kazi ya kutekeleza ulinzi juu ya Buganda kwa niaba ya London iliyosita bado kuanzisha koloni kamili.

Kushindwa kwa kampuni[hariri | hariri chanzo]

Kampuni ilona nafasi kubwa ya biashara ya Uganda ikaona lazima kuwa na reli kati ya Kampala na Mombasa. Lakini upana wa eneo lililokabishiwa pamoja na gharama za kujenga reli hii zilishinda uwezo wa kampuni. Mwakilishi wa kampuni kanali Frederick Lugard (1858-1945) akajikuta ndani ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Buganda. Kampuni ikakosa uwezo wa kugharamia juhudi za Lugard. Baada ya kifo cha Mckinnon 1893 kampuni ilikwama. 1895 serikali ya Uingereza ilichukua utawala wa Uganda pamoja na maeneo kati ya Mombasa na Uganda na kampuni ikaacha haki zake kwa fidia ya £ 250,000.

Vyanzo[hariri | hariri chanzo]