Nenda kwa yaliyomo

Mkutano wa Berlin wa 1885

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mkutano wa Berlin wa mwaka 1885.

Mkutano wa Berlin wa 1885 (kwa Kijerumani: "Kongokonferenz" yaani "mkutano juu ya Kongo") ulikuwa mkutano wa kimataifa kuhusu athira ya nchi za Ulaya katika Afrika uliofanyika kati ya tarehe 15 Novemba 1884 na 26 Februari 1885 huko Berlin, mji mkuu wa Ujerumani.

Kwenye mkutano huo Afrika haikugawiwa lakini mapatano kati ya nchi kubwa za Ulaya yaliandaa ugawaji wa Afrika uliofuata[1][2][3].

Matokeo yake yalikuwa "Azimio la Berlin" (Kongoakte; General Act of the Berlin Conference) lililokuwa na kanuni za kuratibu uhusiano kati ya madola ya Ulaya yakija kukutana katika Afrika.

Utangulizi[hariri | hariri chanzo]

Kufifia kwa ukoloni mwanzo wa karne ya 19[hariri | hariri chanzo]

Kwa sehemu kubwa ya karne ya 19 mataifa ya Ulaya hayakutafuta utawala katika Afrika. Vituo mbalimbali vilivyoanzishwa katika karne za 17 na 18 kwenye pwani za Afrika zilikwama tena kwa sababu gharama hazikulingana na faida.

Hasa kupigwa marufuku kwa utumwa katika milki ya Uingereza kulipunguza faida za makoloni hayo yailiyokuwa madogo na zaidi vituo vya kibiashara na vya kijeshi kwa ajili ya mawasiliano baharini. Biashara ya watumwa iliendelea bado kuelekea makoloni ya Kireno ya Brazil na nchi za Kiislamu.

Mataifa ya Ulaya hayakujaribu sana kupanua utawala wao barani. Sifa za koloni zilipungua kwa jumla kwa sababu nchi mbalimbali zilipoteza makoloni yao baada ya kuasi kwa walowezi huko Amerika ya Kaskazini dhidi ya Uingereza (ndio mwanzo wa Marekani), huko Amerika ya Kusini dhidi ya Hispania (ndio mwanzo wa mataifa mapya ya Amerika Kusini) na uasi wa watumwa wa Haiti dhidi ya Ufaransa.

Watu wengi waliuliza maswali juu ya faida ya kuwa na koloni kama wachache walitajirika lakini umma ilipaswa kugharimia vita na majeshi ya kutetea koloni.

Kuangalia upya Afrika[hariri | hariri chanzo]

Lakini katika sehemu ya pili ya karne ya 19 Afrika ilianza kuvuta upya wafanyabiashara wa Ulaya kwa sababu mapinduzi ya viwandani yalihitaji mafuta yaliyotokana na mawese ya kutia grisi mashine za viwandani. Mafuta hayo yalipatikana katika nchi za Guinea hasa eneo la delta ya mto Niger.

Serikali za Ulaya zilijaribu kuhakikisha kipaumbele na faida kwa wafanyabiashara kutoka kwao. Hali hii ilianzisha mashindano kati ya nchi hizo.

Kuanzia mwaka 1869 mfereji wa Suez ulifunguliwa na kufupisha safari kati ya Ulaya na Asia. Uingereza, Ufaransa na Italia zilishindana kukamata vituo vya kijeshi kando la mlangobahari wa Bab el Mandeb kwa nia ya kuhakikisha athira yao juu ya njia hiyo ya mawasiliano.

Safari za Henry Morton Stanley katika beseni ya mto Kongo ziliondoa mabaka meupe kwenye ramani za Afrika. Mfalme Leopold II wa Ubelgiji alimwajiri Stanley aliyejenga misingi ya utawala wa Leopold huko Kongo. Wakati huohuo taarifa za Stanley juu ya eneo la Kongo iliwasha tamaa za kujipatia malighafi za eneo hili.

Mashindano juu ya utawala wa Afrika[hariri | hariri chanzo]

Katika miaka tangu 1880 nchi mbalimbali za Ulaya zilianza kuvamia sehemu za bara la Afrika kwa sababu tofautitofauti. Sababu muhimu ilikuwa maendeleo makubwa ya teknolojia katika nchi za viwandani yaliyosababisha uwezo wao wa kijeshi kupita uwezo wote wa jamii ambazo hazikufikia bado hali hii. Kwa lugha nyingine: gharama za kuvamia nchi isiyo ya viwandani zilipungua haraka. Mwendo huo ulisababisha mashindano kati ya nchi zilizoendelea na hofu ya nchi nyingine kupata kipaumbele.

Chanzo[hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha mkutano ulikuwa fitina kati ya Ureno na Shirika la Kimataifa la Kongo la mfalme Leopold II wa Ubelgiji juu ya utawala wa mdomo wa mto Kongo.

Ureno ilikumbuka mkataba wake wa karne zilizopita na ufalme wa Kongo na kudai pwani yote pamoja na mdomo wa mto mkubwa ni yake. Leopold II alitegemea njia ya mto kwa mawasiliano yake, alihitaji kanda la eneo hadi baharini.

Uingereza ulisimama upande wa Ureno. Chansela Bismarck wa Ujerumani alikuwa tayari kupatanisha nchi hizo na kuongeza msimamo wake wa kidiplomasia.

Habari za mkutano ziliharakisha jitihada za kusimamisha bendera za Ulaya kwenye ardhi ya Afrika. Mwaka 1884 uliona wimbi la matangazo ya maeneo ya Afrika kuwa eneo lindwa la Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia. Mara nyingi sababu ya kutangaza madai au eneo lindwa ilikuwa hofu ya nchi nyingine kusimamisha bendera yake palepale.

Wapelelezi na wafanyabiashara walijitahidi kuweka msingi wa koloni kabla ya mkutano wa Berlin kwa tumaini la kwamba maazimio yake yatathibitisha madai yao.

Kati ya wapelelezi waliokazia jitihada alikuwa Mjerumani Karl Peters, aliyezunguka katika Afrika ya Mashariki[5]dhidi ya ushauri wa serikali yake, akikusanya sahihi za machifu waliotia sahihi mikataba naye bila kuelewa walichofanya.

Kabla ya mkutano na wakati wa mkutano wenyewe Peters aliweka msingi wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani ya baadaye.

Washiriki[hariri | hariri chanzo]

Nchi zifuatazo zilishiriki mkutano chini ya uenyekiti wa Chansella Bismark:

Agenda[hariri | hariri chanzo]

Agenda za mkutano zilikuwa na vipengele vifuatavyo:

 1. Uhuru wa biashara katika beseni la mto Kongo
 2. Biashara ya utumwa
 3. Azimio kuhusu nchi katika beseni ya Kongo kutokuwa upande wowote
 4. Usafiri kwa maji kwenye mto Kongo
 5. Usafiri kwa maji kwenye mto Niger
 6. Kanuni za kutwaa sehemu za Afrika kwa njia inayokubalika kati ya mataifa makubwa ya Ulaya

Maazimio[hariri | hariri chanzo]

 1. Kuhusu uhuru wa biashara katika beseni la mto Kongo mkutano ulikubali mipaka ya eneo la beseni ya Kongo, uhuru kwa nchi zote kufanya biashara hapo na kuingiza bidhaa bila ushuru au malipo ya forodha. Haki za wananchi wenyeji zilitakiwa kulindwa. Kila taifa lenye mamlaka katika eneo hilo lilipewa wajibu wa kulinda haki za wenyeji na kufanya juhudi za kuboresha hali ya maisha yao, kuzuia biashara ya watumwa na kuhakikisha uhuru wa dini, hasa kwa wamisionari Wakristo lakini pia kwa dini zote zilizofuatwa katika eneo hili.
 2. Kuhusu biashara ya watumwa mataifa yote yalipaswa kuzuia biashara hiyo na kuadhibu wote waliotenda kinyume
 3. Kuhusu eneo la Kongo kutokuwa upande wowote mataifa yote yalitakiwa kuepukana na hatua za kivita kati yao ndani ya beseni ya Kongo.
 4. Kuhusu usafiri kwa maji washiriki walipatana kutumia kanuni za Mkutano wa Vienna 1815 zinazoipa meli za mataifa yote haki ya kupita na kutumia mito ambayo ni njia za kimataifa.
 5. Kuhusu kanuni kwa kutwaa sehemu za Afrika washiriki walipatana kuwa a) kila nchi inayotaka kutangaza mamlaka juu ya sehemu za pwani za Afrika inapaswa kuwaarifu mataifa mengine[6] na b) mamlaka inaweza kukubalika kuwa kama iko hali halisi yaani kama nchi inayodai mamlaka juu ya sehemu fulani inaweza kuhakikisha uhuru wa biashara na usalama wa kusafiri.

Matokeo[hariri | hariri chanzo]

Hali halisi vipengele vingi vya mapatano ya Berlin havikutekelezwa. Lakini azimio la Berlin ilitambua Shirika la kimataifa la Kongo la mfalme Leopold II.

Mapatano yaliyotokea kando ya mkutano (bila kutajwa ndani ya azimio) yalipandisha cheo cha shirika hilo hadi kuwa kama serikali halisi. Uingereza ilitaka kuzuia upanuzi wa Ufaransa katika eneo la Kongo. Bismark aliona afadhali mfalme dhaifu wa Ubelgiji apate nafasi huko kuliko mataifa makubwa yaliyohofiwa kufunga mlango wa utajiri wa Kongo kwa wafanyabiashara toka nchi nyingine.

Hali hii ilifungulia nafasi kwa ujanja wa mfalme Leopold II aliyeendelea kutangaza maeneo ya shirika yake kuwa "Dola huru la Kongo" lililokuwa mali yake binafsi. Hii ilikuwa chanzo cha utawala wa kinyama na unyonyaji wa Kongo uliokuwa kipindi kibaya cha ukoloni kushinda nchi zote. Mamilioni ya wakazi wa Kongo walilazimishwa kukusanya malighafi, hasa mpira, na mamilioni walikufa.

Mengineyo ni kwamba mkutano ulisababisha kuongezeka kwa juhudi za mataifa ya Ulaya kugawa Afrika kati yao. Mnamo 1895 zilibaki nchi za kujitawala Ethiopia, Liberia pamoja na jamhuri za makaburu Dola Huru la Oranje na Transvaal pekee. Jamhuri mbili za makaburu zilitwaliwa na Uingereza kwa njia ya vita baina ya miaka 1899 na 1902. Miaka 15 baada ya mkutano Afrika yote iligawiwa tayari kati ya mataifa ya Ulaya isipokuwa nchi za Liberia na Ethiopia.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

 1. Katzenellenbogen, S. (1996). "It didn't happen at Berlin: Politics, economics and ignorance in the setting of Africa's colonial boundaries.". Katika Nugent, P.; Asiwaju, A. I. (whr.). African Boundaries: Barriers, Conduits and Opportunities. London: Pinter. ku. 21–34.
 2. Craven, M. (2015). "Between law and history: the Berlin Conference of 1884-1885 and the logic of free trade". London Review of International Law. 3: 31–59. doi:10.1093/lril/lrv002.
 3. Crowe, S.E. (1942). The Berlin West African Conference, 1884–1885. London: Longmans Green.
 4. iliyokuwa baadaye Kongo ya Kifaransa, leo Jamhuri ya Kongo
 5. maeneo ya Tanzania bara ya leo
 6. kwa shabaha ya kuepukana na kugongana kwa madai ya mataifa tofauti juu ya eneo lilelile

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkutano wa Berlin wa 1885 kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.