Lango:Afrika
Afrika ni bara la pili duniani kwa ukubwa, likiwa na eneo la kilometa za mraba zipatazo 30,370,000 na kwa idadi ya wakazi, hao wakiwa 1,225,080,510 (mwaka 2016). Asia ndiyo bara pekee la kushinda Afrika.
Neno "Afrika" limetokana na lugha ya Kilatini ya Roma ya Kale. Waroma kwa jina hilo hawakumaanisha bara lote bali eneo katika Tunisia ya leo tu. Asili yake ni kabila la "Afrig" lililoishi sehemu zile. Wakati huo Wagiriki wa Kale walitumia zaidi jina la Libya kwa ajili ya nchi kusini kwa Bahari ya Mediteraneo. Maeneo ya ndani kuelekea kusini mara nyingi yaliitwa kwa jina la "Ethiopia" linalomaanisha nchi ya watu weusiweusi (kwa Kigiriki "aithiops": aliyechomwa na jua). ![]() Patrice Lumumba (2 Julai 1925 – 17 Januari 1961) alikuwa mwanasiasa mwanamapinduzi wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwaka wa 1958 alikuwa miongoni mwa waanzishaji wa Chama cha Taifa la Kongo (kwa Kifaransa: Mouvement National Congolais). Mwaka wa 1960 alipata kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kuongoza harakati za kugombea uhuru toka kwa utawala wa kikoloni wa Wabelgiji. Baada ya miezi miwili tu ya kuwa Waziri Mkuu, Lumumba alipinduliwa na baadaye kutiwa ndani kabla ya kuuawa katika mazingira ya kutatanisha katika eneo la Katanga upande wa kusini wa Kongo.
![]() Eratosthenes wa Kirene (Kigir. Ερατοσθένης ο Κυρηναίος, 276 KK - 194 KK) alikuwa mtaalamu wa hisabati, jiografia, historia na lugha na mkurugenzi wa maktaba ya Aleksandria katika Misri. Anakumbukwa hasa kama mtu wa kwanza aliyekadiria mzingo wa dunia. Anasemekana aliibuni neno la jiografia. Erastothenes alizaliwa mnamo mwaka 276 KK mjini Kirene wa Libya. Kirene ilikuwa moja ya miji iliyoundwa na Wagiriki wa Kale huko Afrika. Alienda Athens kwa masomo yake alipofundshwa na wanafalsafa na wataalamu mashuhuri. Mnamo mwaka 255 alihamia Aleksandria iliyokuwa mji mkuu wa Misri. Akawa mwalimu wa mwana wa mfalme na mwaka 236 KK alikuwa mkurugenzi wa tatu wa maktaba ya Aleksandria iliyokuwa kitovu cha elimu cha kimataifa kwa sababu ya mkusanyiko mkubwa wa vitabu.
|